Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Christina Solomon Mndeme (5 total)

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali la nyongeza. Katika Zahanati ya Imalakaseko iliyopo Kata ya Goweko, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora, Serikali ilitoa shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto lakini wodi hiyo bado haijakamilika. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa wodi hiyo ya mama na mtoto katika zahanati ya Imalakaseko, Kata ya Goweko, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui? Ahsante. (Makofi)



NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amegusia hasa katika zahanati ya Imalakaseko, Halmashauri ya Uyui. Kwanza Serikali imeshatenga shilingi milioni 80 kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Pia, ninamwelekeza Mkurugenzi kuendelea kutenga fedha za ndani Halmashauri ya Uyui ili kuweza kukamilisha ujenzi wa zahanati hii. (Makofi)
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa Ziwa Victoria kutoka Kata ya Nkinga kwenda Kata ya Simbo Wilaya ya Igunga, kwa sababu mradi huu ulitakiwa ukamilike tangu mwezi Aprili, 2025 lakini mpaka sasa hivi haujakamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata za Chabutwa, Simbo, na Mwisi Wilaya ya Igunga wanapata shida sana, wakiwemo wanawake na wasichana. Ni lini mradi huu utakamilika ili mama huyu aweze kutuliwa ndoo kichwani na dhamira ya Mheshimiwa Rais iweze kutekelezwa kwa vitendo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na maelezo na swali ambalo ameuliza Mheshimiwa Mndeme, ameendelea kuwapambania sana wananchi, na hasa akina mama wa Tabora. Hata kabla ya leo, juzi Mheshimiwa aliweza kuwasilisha changamoto hiyo ya wananchi wa Mkoa wa Tabora hususan katika eneo la Igunga, na sisi tuliipokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, tunaendelea kuifanyia kazi. Tunafahamu kabisa kwamba mradi huu ulitakiwa kukamilika mwaka 2025 na kwa bahati mbaya kulitokea changamoto kidogo, tunaendelea kuzifanyia kazi. Tukishakamilisha, tunaamini kwamba wakandarasi wataenda kuutekeleza mradi na kuukamilisha kama ambavyo imekusudiwa.
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa, Serikali imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, na kwa kuwa kiwanda cha nyuzi cha Tabora, (TABOTEX) kimesimama miaka mingi sana bila kufanya kazi, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba kiwanda hiki cha nyuzi Tabora kinafufuliwa na kuanza kufanya kazi ili kiweze kutoa ajira kwa Wanatabora na Watanzania kwa ujumla na kukuza uchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninachukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kutoka Mkoa wa Tabora. Ninajua michango yake mingi nimekuwa nikiifuatilia, amekuwa akichangia sana kwenye suala la uwekezaji, na jinsi ya kuwezesha kinamama katika suala la uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hiki kiwanda cha nyuzi cha Tabora ambacho kimesimama kama tutakifufua kitakuwa na tija sana kwa uchumi wa Taifa. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali tumeweka mkakati wa kutathmini viwanda vyote ambavyo vimesimama na baada ya tathmini hiyo tutaandaa mpango mkakati wa kuvifufua ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji. Ahsante sana.
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuboresha Sekta ya Afya. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, zimekuwepo changamoto ambazo huwapata baadhi ya wakinamama ambao baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali kukosa uelewa thabiti wa kuendelea na malezi ya mtoto njiti mara wanaporudi nyumbani. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu ya malezi kwa wakinamama wanapokuwa wamerudi nyumbani ili aendelee kumlea vizuri mtoto anapokuwa nyumbani ili kupunguza uwezekano wa kutokea vifo vya mtoto njiti anapokuwa nyumbani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, kuna utafiti wowote umefanyika ili kupunguza hili tatizo la watoto kuzaliwa kabla ya muda na kama utafiti huo umefanyika, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu hii kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kutoka Tabora kwa jinsi ambavyo anawapigania wanawake wa Tabora ili waendelee kupata watoto waliozaliwa njiti na kuwa salama. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, ninaomba kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali imeweka mwongozo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakinamama hawa wanapokwenda nyumbani ili elimu hii itolewe kwa mtiririko.
Mheshimiwa Spika, watoto hawa wanaozaliwa njiti ikumbukwe kwamba viungo vyao ambavyo vinawasaidia wao kuishi ikiwemo ini, mifupa, Ngozi, vyote navyo vimezaliwa vikiwa havijakomaa. Hivyo, msingi wa elimu hii ni kuwasaidia waweze kujua jinsi ya kuwakinga, waweze kuwalinda na wale watoto wawe salama ikiwemo kwanza kabisa, kuwasaidia kuwapatia joto.

Mheshimiwa Spika, elimu tunayowapatia ni kuendelea kufanya mamakangaroo ambapo mama huyu anatakiwa kumlea huyu mtoto wakati wote huku amemweka kifuani na akiendelea kupata joto la mama kwa kushikana ngozi kwa ngozi.

Mheshimiwa Spika, vilevile, tunaendelea kumfundisha huyu mama umuhimu wa kumnyonyesha ziwa la mama ambalo lina faida zaidi ya chakula. Mtoto huyu amezaliwa akiwa kinga yake pia ipo chini. Kwa hiyo, kwa kumnyonyesha ziwa la mama inamsaidia pia huyu mtoto aweze kupata kinga ili aepukane na magonjwa. Pia, kwa vile huyu mtoto njiti amezaliwa bila ya kuwa na kinga, tunamfundisha mama aendelee kumtenga huyu mtoto na watu wengine ili asiweze kupata maambukizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tunamfundisha huyu mama jinsi ya kuendelea kumpatia huyu mtoto chanjo pale muda utakapofika ili asiweze kupata maambukizi. Tunaendelea kumwambia huyu mama amlete mtoto kliniki kwa kufuata tarehe tulizompangia ili tuweze kuendelea kumpa elimu zaidi, na vile vile kuendelea kumpatia huyu mtoto huduma muhimu.

Mheshimiwa Spika, mwisho siyo kwa umuhimu, tunamfundisha dalili zote hatarishi ikiwemo kama kubadilika rangi mtoto, kuwa manjano, maana ini pia halijakomaa ikiwepo dalili ya mtoto kushindwa kupumua kwa sababu mapafu pia hayajakomaa na dalili yoyote ya hatari ambayo akiiona tu basi afike hospitalini haraka ili aweze kupata ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Mbunge alitaka kujua kama kuna utafiti wowote umefanyika. Zipo tafiti nyingi zimefanyika Kitaifa na Kimataifa, lakini pia Shirika la Afya Duniani, limefanya tafiti na kuona kwamba watoto wanaozaliwa njiti wanaongezeka kila mwaka na tafiti zimeonesha kwamba watoto hawa wanaongezeka kila mwaka kwa 10% mpaka 15% kwa watoto wanaozaliwa. Mfano, watoto wanaozaliwa Tanzania kwa mwaka ni kati ya watoto 1,900,000 mpaka 2,200,000. Kwa hiyo, tuna watoto 250,000 mpaka watoto 300,000 kwa mwaka ambao ni njiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la (b) kwamba kama tumefanya tafiti, je tumetoa elimu? Serikali kupitia Wizara ya Afya, tumeendelea kutoa elimu kwa wamama wote wajawazito pale wanapofika kliniki. Maana matatizo yanayosababisha watoto kuzaliwa kabla ya wakati, yapo ambayo yanaweza kuzuilika ikiwemo maambukizi ambayo yanaweza kuleta homa kama vile Malaria, UTI, Pneumonia na mengine ikiwemo kiasi kidogo cha damu kwa mama mjamzito kinaweza kuleta kuzaliwa mtoto njiti, magonjwa sugu kama vile kisukari na shinikizo la damu kuwa juu.

Mheshimiwa Spika, hivyo ni visababishi ambavyo mama akifika mapema, basi tunampa elimu ili tumtibu vizuri ili asiweze kujifungua mtoto ambaye hajatimia. Vipo visababishi ambavyo huwezi kuvizuia kama vile kuwa na mimba ya watoto mapacha. Tunawashauri wamama wafike mapema ili tuwape uangalizi wa karibu ili kuzuia wasiweze kujifungua watoto njiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naanza kwa kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya na hususan kuhakikisha kwamba suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi linatekelezwa ipasavyo. Naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa malengo haya ambayo yanakwenda kumuongezea kipato mwananchi kuanzia ngazi ya kaya mpaka Taifa na hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuiuliza Serikali swali hili, katika malengo haya mazuri ya Serikali ya kuwakopesha wajasiriamali hususan wanawake na hasa wanawake wa Mkoa wa Tabora.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mikopo hii wanayopewa wanawake wajasiriamali, wanazalisha bidhaa zenye kukidhi haja na soko lililopo sasa hivi nchini na nje ya nchi ili sasa bidhaa zao zile wanazozalisha ziweze kuwa na tija na kukidhi soko la ndani na soko la nje ili waweze kuinua kipato chao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ufuatiliaji wa mikopo hii, je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba mikopo inayotolewa inafuatiliwa na kweli inakwenda kuzalisha kwa tija?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji majibu ili sasa wanawake hawa waweze kuzalisha kwa tija na hususan wanawake wa Mkoa wa Tabora ili kipato chao kiweze kukua kuanzia ngazi ya familia na Taifa. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwapigania wananchi hasa akinamama wa Mkoa wa Tabora, anataka tuhakikishe tunapeleka tabasamu. Ninapokea pongezi ambazo amezitoa na hiyo ndiyo nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha anatukomboa kiuchumi wapambanaji wetu akinamama wa Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwishatoa maelekezo kwamba maafisa maendeleo wetu hawana kazi tu ya kukusanya fedha na kuzipeleka kwenda kwenye mikopo, wanayo kazi ya kutoa elimu ya tija ya kutosha na kufuatilia marejesho ili tuweze kuwakopesha na wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)