Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Athumin Omary Mapalilo (1 total)

MHE. ATHUMIN O. MAPALILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, mikopo hii ni muhimu sana kwa wananchi wetu, na walio wengi hawawezi kutumia mifumo hii ya ukopeshaji, hasa wale walioko kijijini, je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kuwatumia Maafisa Watendaji wa Vijiji ili waweze kuwasaidia, hasa kundi la wanawake, kuweza kufikia fursa hizi za mikopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mtwara, kwamba Serikali inatambua changamoto hiyo, pamoja na kwamba, mfumo huu wa WEZESHA unatumika na simu yoyote; simu janja na simu za kawaida, lakini bado kuna changamoto ya uelewa kwa baadhi ya wanufaika au walengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshatoa maelekezo kwamba, Watendaji wa Vijiji, Maafisa Maendeleo katika ngazi za kata na Maafisa Ustawi wa Jamii wawe sehemu ya kuwezesha kutoa elimu na hamasa kwa walengwa, ili waweze kupata elimu na ku-access mikopo hii kupitia maeneo yao. Kwa hiyo, suala hili linafanyika na tutaendelea kuliboresha zaidi ili watendaji waweze kuwasaidia vikundi hivi wapate nafuu na uwezo mzuri zaidi wa kupata mikopo hiyo.