Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. ASHA OMAR RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kusimama katika Bunge hili Tukufu. Ikiwa leo ni mara yangu ya mwanzo, ninachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kipekee nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniamini na kuniteua na leo hii ni Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba na leo nimesimama hapa ndani ya Bunge Tukufu. Nichukue fursa hii kuwashukuru kwa dhati kubwa ndani ya moyo wangu, Wapiga kura wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, akinamama, kwa kuniamini na kuthubutu kunisimamisha hapa leo katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kwa moyo wa dhati ninampongeza Mheshimiwa mama yangu kipenzi cha Watanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hotuba yake nzuri iliyojaa maono, iliyojaa fikra. Hotuba hii imemaliza kila kitu, mama kwa kweli, hapa amefanya kazi na anatekeleza; kweli mama ni mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na wanawake wa UWT Mkoa wa Kaskazini Pemba wanampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake iliyotaradadi na iliyojaa muono wote wa Watanzania. Ninachukua nafasi hii kuchangia yale niliyoyaona katika hotuba ya Mheshimiwa Rais; Mheshimiwa Rais ni mwanamke pekee aliyeweza na mwenye muono wa mbali. Vilevile amejikita kama mama katika uongozi huu, lakini hakukaa kama Rais tu, ameona kama ni mama ambaye anathubutu kubeba, kuwasilisha na kusimamia majukumu yote ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja naenda kwenye sekta ya afya. Mheshimiwa Rais alipozungumzia suala la afya hapa alitumaliza sote wananchi na hadi ikafika siku ya uchaguzi kila kitu kikakaa sawa. Mheshimiwa Rais ameboresha huduma za afya katika mikoa yetu, tukiangalia sasa hivi katika mikoa yetu tuna hospitali za wilaya ambapo tunapata huduma tofauti na huko nyuma tulivyokuwa na vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameboresha huduma iliyo bora na sahihi mpaka kusababisha sasa hivi vifo vya akinamama na watoto wachanga vimepungua kwa asilimia kubwa, jamani hakuna kama mama. Huyu mama tumpongeze na lazima ukweli wake usemwe, jamani, mama tumzungumzie vizuri na apewe maua yake. Mama amethubutu kama mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuboresha huduma ya afya tukapata huduma nzuri akinamama na watoto, amehakikisha mnyonge maskini wa chini akienda katika vituo vya afya anapata huduma iliyo sahihi sawasawa na mtu aliye na kipato cha juu, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais. Imefika hadi sasa hivi kwenye sekta ya afya akifika mgonjwa pale, kama kalazwa siku mbili anatamani aongeze siku kwa huduma nzuri anayoipata. Jamani mama anaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye sekta ya maji ni kila kitu. Maji ni afya na mama ndiyo kalizungumza kwenye kitabu chake hiki cha hotuba na ameboresha miradi na kuisimamia. Ameweka muda iweze kufanya kazi na watu wote wapate maji kwa sababu, bila maji hakuna lolote, maji ni uhai, maji ni kila kitu. Maji haya haya ni kwamba, Mheshimiwa Rais ametugusia sisi akinamama wakati tunapokwenda kwenye huduma zetu, ama kikazi ama kiafya, mama unakwenda pale ukiwa na matumaini, ukiwa na imani kwamba, huduma pale unayoipata ni bora na sahihi, lakini huku nyumbani ukirudi huduma ya maji inapatikana muda wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Mawaziri wanaoshughulikia sekta hii ya maji, wasimamie vizuri, wamkamate mama mkono. Hili suala, kama alivyolisema mama, lifanyike kwa uadilifu na wananchi wapate maji kwa wakati sahihi, wa mijini na vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika huyu ni mama, amejitoa kwa Watanzania. Huyu mama anaweza na ni wa kumpigia mfano. Tutake tusitake tumzungumze mama kwa utekelezaji wake mzuri, tutake tusitake, tusimame tumsemee mama kwa muono wake wote wa kuwaona Watanzania, kuwajali wanawake na kuwajali vijana na wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya mengi tena ya kupigiwa mfano, anastahiki kupewa tuzo. Ni mwanamke bora, ni mwanamke shupavu aliyejitolea, halali usiku, halali mchana, muda wote anatafakari nchi yake inakwenda vipi? Iende vipi? Wananchi wake watakaa vipi? Ilimradi wananchi hawa anaowasimamia wawe katika hali ya salama na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi na wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba wanasema, mcheza kwao hutunzwa, huyu mama ni lazima atunzwe. Vilevile, wamenituma nimpe salamu mama, wanamwombea dua, wanamwombea kwa Mwenyezi Mungu mama huyu kila anapokaa Mungu amlinde, amsimamie, ampe maisha marefu, ampe maisha mazuri na awe na uthubutu wa hali ya juu kabisa kusimamia wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ninamalizia kwa kusema muungwana ni vitendo na vitendo vya mama tumeviona. Ninaomba kuunga hoja ya Hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)