Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew (4 total)

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jibu la Serikali limeonesha matumaini ya kukamilika upembuzi yakinifu wa mradi huu wa kuyatoa maji Mto Rufiji; na kwa kuwa ni maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan; na kwa kuwa Serikali hii imejaliwa ubunifu wa kutafuta vyanzo mbadala wa kutekeleza miradi.
Je, Serikali ipo tayari kuanza kutafuta chanzo mbadala kwa mfano ilivyoruhusu Mamlaka ya Maji Tanga kuwa na hati fungani ya kijani, lakini pia ilivyoruhusu Mfuko wa Barabara (TARURA) kuwa na Samia Bond; je, Serikali ipo tayari nayo kutekeleza mradi huu kwa kutumia hati fungani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali ilinunua magari ya kuchimba visima; na kwa Mkoa wa Pwani imefanyakazi nzuri kati ya visima 900 tumepata visima 35 na vimetoa maji vikiwepo visima 10 vya Wilaya ya Bagamoyo, lakini bado baadhi ya Kata zina changamoto kubwa ikiwemo Kata ya Makurunge; je, Serikali ipo tayari kuanza awamu ya pili ya visima vingine kugusa maeneo yenye changamoto ya maji ikiwemo Kata ya Makurunge, Bagamoyo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nikupongeze sana Mheshimiwa Subira Mgalu kwa ufuatiliaji wa karibu sana masuala ya maji kumtua mama ndoo kichwani, lakini vilevile katika mradi huu kuona kwamba tunaweza tukatumia hati fungani ndiyo mpango wa Wizara kuhakikisha hati fungani itatumika pale inapowezakana.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na magari ya uchimbaji wa visima nipende tu kukupongeza pia kwa ufuatiliaji, haya magari yataendelea kuchimba visima nchi nzima na katika hili eneo la Makurunge na maeneo yote ambayo bado hayajapata visima naamini katika mwaka ujao wa fedha Mheshimiwa Mbunge maeneo hayo pia yatapatiwa visima.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa miradi mingi ya maji kwenye Wilaya ya Kyerwa inachukua muda mrefu kukamilika kama ule Mradi wa Runyinya – Kimuli na wa vijiji 46; ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba inakamilisha miradi hii ili wananchi wa Kata ya Nyakantuntu na Kamuli waweze kunufaika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Halmashauri ya Mji wa Tarime tunapata Mradi kutoka Ziwa Victoria, lakini tuliahidiwa kwamba tungeweza kupelekewa visima ambavyo vingeweza kusaidia kwenye maeneo kama ya Shule ya Sekondari Nyandoto, Nyakisese na Mkongole vilevile Vituo vya Afya vya Kibumayi na Magena; ni lini sasa Serikali itapeleka uchimbaji wa visima hivi wakati tukisubiria mradi mkubwa wa Ziwa Victoria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, lini tutakamilisha miradi hii ya vijiji 46 na huu mradi unaoenda kwenye hii Kata uliyoitaja Mheshimiwa Mbunge. Nikuhakikishie Serikali kadiri inapopata fedha tutahakikisha miradi hii inakamilika kwa sababu lengo la Serikali ni kuona wananchi wanapata maji safi na salama na kumpunguzia mwendo mwanamke ambaye anafuata maji umbali zaidi ya mita 400.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tarime hivi visima navyo vipo katika mpango, Mheshimiwa Waziri naye anaendelea kuona namna ya njema ya kuhakikisha visima hivi tunakuja kuvichimba mapema sana na dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mama ndoo kichwani inaweza kukamilika.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Kata ya Kikukuru mkandarasi ameondoka site zaidi ya miezi miwili kwa sababu ya madai; ni lini atalipwa ili arudi site kukamilisha mradi huu ambao ni muhimu kwa wananchi wa Kikukuru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza; lini mkandarasi atalipwa ili mradi ukamilike?

Mheshimiwa Spika, tayari Wizara imeanza malipo kwa wakandarasi wapo kwenye foleni wanapunguzwa taratibu na kadiri fedha inapopatikana tutahakikisha wakandarasi wote wanalipwa ili waweze kufanyakazi kadiri ya mikataba waliyosaini. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona, mradi wa maji unaogusa Kata za Maji ya Chai – Kikatiti hadi Samaria Kata ya Maroroni inatekelezwa kwa kusuasua sana na katika ufuatiliaji wangu nimegundua kwamba mkandarasi pia mwenye matatizo kwa hiyo kuna haja ya kuchukua hatua stahiki mapema inavyowezekana.

Je, Waziri utakuwa tayari kuambatana na mimi twende jimboni tukafanye site meeting na stakeholders wote ikiwepo DC, Mkurugenzi na RUWASA? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwanza mkandarasi yeyote ambaye hatekelezi majukumu yake anafahamu namna sheria ambavyo zinambana. Kwa hiyo, nikutoe hofu Mheshimiwa Mbunge naamini Wizara ya Maji wataenda kumshughulikia na kuona kwamba anafika site na kufanyakazi iliyotarajiwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuambatana na yeye naomba nipokee na nitamfikishia Mheshimiwa Kundo naamini hatakuwa na kipingamizi katika hilo. (Makofi)