Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jonas William Mbunda (2 total)

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay, lakini pia kuna usafirishaji mkubwa wa makaa ya mawe kutoka Nyasa na Mbinga kwenda Mtwara; lakini pia tunategemea Mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma. Katika majibu ya msingi ya Naibu Waziri amesema kwamba upembuzi yakinifu wa kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa SGR kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay umeanza kutekelezwa. Je, itachukua muda gani kukamilisha upembuzi yakinifu na mradi huo ukaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu swali hili linagusa takriban Wabunge wote wa Kusini; na pengine wangesimama kutaka kuuliza reli ya kusini itaanza kutekelezwa lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitoe maelezo kwa ufupi sana. Serikali inatambua umuhimu wa reli ya kusini, kwanza kama kiunganishi cha Bandari ya Mbamba Bay na Bandari ya Mtwara, kwa sababu hizi mbili zikiungana unarahisisha usafirishaji; na nini kimekifanyika?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua za awali Serikali imekwishaanza kujenga Bandari ya Kisiwa Mgao pale Mtwara bandari ya pili ambayo itakuwa maalum kwa ajili ya kusafirisha dirty cargo; yaani cement, makaa ya mawe na kadhalika; zaidi ya bilioni 435 zimeelekezwa pale. Pia ujenzi wa bandari ya Mbamba Bay ambao utagharimu zaidi ya bilioni 70, ni hatua muhimu kuelekea kwenye jambo hilo. Tatu, fidia imelipwa kule Ludewa kwa wananchi waliopo kwenye maeneo ya Liganga na Mchuchuma, hiyo ni hatua pia. Nne sasa, tumekwishafanya usanifu. Kama nilivyosema, tunatafuta wawekezaji binafsi ambao tutashirikiana nao ili tuanze kujenga. Ninatoa rai tena kwa watu wote wa ndani na nje ya nchi ambao wapo tayari kushirikiana na Serikali, twendeni tukajenge reli hii ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri. Pili ninaishukuru Serikali kwa kuanza kujenga mnara wa simu katika Kata ya Kikolo, na pia kufikiria kuanza kufanya tathmini ya kujenga mnara wa simu katika Kata ya Kagugu. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, mradi unaoanza kutekelezwa kujengwa mnara katika Kata ya Kikolo unakwenda kwa kusuasua. Nataka nijue, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mnara huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kijiji cha Ruangai eneo la Kipungu Kata ya Mpepai kuna changamoto kubwa ya mawasiliano ya simu. Ni lini Serikali itaweka mkakati wa kuhakikisha kwamba inajenga mnara wa simu katika eneo hili ili wananchi waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa mnara tulioutaja katika Kijiji cha Kikolo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii itakamilika tarehe 30 Juni, 2026, kwa sababu tayari mkandarasi ameshapatikana na anaendelea na mobilization. Atakapokamilisha mobilization, ujenzi utaanza mara moja. Ifikapo tarehe 30 mwezi wa Sita, ujenzi huu utakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto ya mawasiliano katika Kijiji cha Luhangali, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mkakati wetu wa Serikali wa miaka mitano kuanzia mwaka 2025 kwenda mwaka 2030, tutafanya tathmini katika maeneo yote yenye changamoto na tutayafikia. Tutaanza na maeneo ya changamoto kubwa, changamoto za kati na changamoto zenye unafuu. Kwa hiyo, tutapitia zote na kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030 kila Mwananchi wa Tanzania atakuwa na uso wenye furaha katika sekta hii ya mawasiliano.