MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jibu la Serikali limeonesha matumaini ya kukamilika upembuzi yakinifu wa mradi huu wa kuyatoa maji Mto Rufiji; na kwa kuwa ni maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan; na kwa kuwa Serikali hii imejaliwa ubunifu wa kutafuta vyanzo mbadala wa kutekeleza miradi.
Je, Serikali ipo tayari kuanza kutafuta chanzo mbadala kwa mfano ilivyoruhusu Mamlaka ya Maji Tanga kuwa na hati fungani ya kijani, lakini pia ilivyoruhusu Mfuko wa Barabara (TARURA) kuwa na Samia Bond; je, Serikali ipo tayari nayo kutekeleza mradi huu kwa kutumia hati fungani?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali ilinunua magari ya kuchimba visima; na kwa Mkoa wa Pwani imefanyakazi nzuri kati ya visima 900 tumepata visima 35 na vimetoa maji vikiwepo visima 10 vya Wilaya ya Bagamoyo, lakini bado baadhi ya Kata zina changamoto kubwa ikiwemo Kata ya Makurunge; je, Serikali ipo tayari kuanza awamu ya pili ya visima vingine kugusa maeneo yenye changamoto ya maji ikiwemo Kata ya Makurunge, Bagamoyo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nikupongeze sana Mheshimiwa Subira Mgalu kwa ufuatiliaji wa karibu sana masuala ya maji kumtua mama ndoo kichwani, lakini vilevile katika mradi huu kuona kwamba tunaweza tukatumia hati fungani ndiyo mpango wa Wizara kuhakikisha hati fungani itatumika pale inapowezakana.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na magari ya uchimbaji wa visima nipende tu kukupongeza pia kwa ufuatiliaji, haya magari yataendelea kuchimba visima nchi nzima na katika hili eneo la Makurunge na maeneo yote ambayo bado hayajapata visima naamini katika mwaka ujao wa fedha Mheshimiwa Mbunge maeneo hayo pia yatapatiwa visima.