Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Edwin Enosy Swalle (2 total)

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kata ya Kidegembye, hasa pale kwenye Kijiji cha Image, ambako Mheshimiwa Naibu Waziri anapafahamu, wananchi wamejengewa shule nzuri sana ya amali, lakini ipo mbali na makazi ya wananchi, kwa hivyo, hakuna nyumba za waalimu wala karakana kwa ajili ya wale wanafunzi, na hakuna bweni. Ni lini Serikali itapeleka fedha, kwa ajili ya bweni, karakana na nyumba za waalimu pale Image?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa shule hizi tulianza na awamu ya kwanza ya shilingi milioni 584 na tulijenga miundombinu ya madarasa na shule zile zimeanza kutoa huduma, kwa maana ya shule za kutwa. Awamu ya pili, tunakwenda kutenga shilingi bilioni 1,600, kwa ajili ya kujenga miundombinu inayosalia, yakiwemo mabweni, karakana na kununua vifaa vya kihandisi, ili wanafunzi wanaojifunza masuala ya kiuhandisi waweze kuwa na mazingira bora ya kujifunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Swalle, Mbunge wa Jimbo la Lupembe, unayefanya kazi kubwa sana kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Lupembe, kwamba, Serikali hii sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua hilo, na tupo kwenye taratibu za kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha shule hizo zote 103, ili ziweze kutimiza lengo lililokusudiwa, ahsante.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mikopo ya 10% imetoa fursa kwa watu wenye ulemavu kukopa mtu mmoja mmoja; pia imetoa fursa kwa watu kuunda vikundi vya watu watano na kuendelea, lakini wapo vijana wengi wamehitimu vyuo vikuu na vyuo vya kati wana ujuzi maalum ambao pengine kuwapata kuwa kikundi, watu wengi ni ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni haja sasa kuongeza kundi la nne ambalo ni la watu ambao wana ujuzi maalum waruhusiwe kukopa mtu mmoja, mmoja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe kwa wazo zuri. Serikali ipo tayari kupokea mawazo ya Waheshimiwa Wabunge. Kupitia wataalam wetu watakaa na kufanya tathmini, na tutapata majibu na kuona namna ya kuzingatia ushauri huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokea ushauri huo wa Mheshimiwa Mbunge na tutafanya tathmini kupitia taratibu za Serikali na kuona namna ya kuboresha hatua kwa hatua, kwa sababu mikopo hii itaendelea kuboreshwa siku hadi siku kulingana na mahitaji ya jamii yetu. Ahsante sana.