Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nami nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetupa afya na uhai wa kuwemo ndani ya Bunge hili siku ya leo na hasa, Bunge la Kumi na Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninaishukuru sana Serikali. Wahenga walisema “Usione vyaelea, vimeundwa.” Sisi Wabunge wengi kwenye majimbo na mikoa ambako tunatoka, zipo kazi nyingi zimefanywa na Serikali. Hata Jimbo la Lupembe, kwa mfano, ukienda leo, hali ilivyokuwa miaka mitano iliyopita, Jimbo la Lupembe, leo jimbo zima linawaka umeme vijiji vyote 45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumepata vitongoji vingine 28, tunaendelea kukamilisha vitongoji vyote kwa ajili ya umeme Jimbo la Lupembe. Hii ni kazi kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita. Ukienda kwenye elimu, madarasa yamejengwa, ukienda kwenye zahanati vituo vya afya hadi kule Ikondo vimejengwa, ambako havijawahi kujengwa tangu kuumbwa kwa dunia hii. Hii ni kazi nzuri ya Chama cha Mapinduzi. Ninaishukuru sana Serikali kwa kazi ambayo inaifanya, kwa ajili ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najielekeza kwenye mchango wangu wa siku ya leo, kwenye eneo la Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Sehemu ya kwanza ambayo imesemwa na Wabunge wengi ni kuhusu hali ya barabara nchini. Tumeambiwa kwenye hotuba, Wabunge wengi wamesema na mimi naomba kupaza sauti kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lupembe. Hali ya barabara za nchi yetu hivi sasa siyo nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe leo hii kwa mfano, Barabara ya Njombe – Lupembe – Madeke mpaka Mlimba kule Morogoro, nimekuwa naisemea ndani ya Bunge hili kila wakati. Sasa hivi yako maeneo yanaleta shida, magari yanakwama, wananchi hawasafiri vizuri na imeahidiwa takribani miaka 20 sasa. Barabara hii ni muhimu kwa sababu, inaunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wananchi wa Mkoa wa Morogoro wanategemea Mkoa wa Njombe kwa ajili ya mbao. Bidhaa za majani ya chai, parachichi na mazao mengine mbalimbali. Tukijenga hii barabara itaweka msukumo wa uwekezaji Lupembe na kufanya wananchi wengi wapate ajira na viwanda vingi sana kujengwa Lupembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali, umefika wakati sasa tujifunge mkanda tuandae mkakati maalum wa kujenga barabara za nchi hii ili kusudi wananchi wetu waweze kuwa na uhakika wa kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu Barabara za TARURA. Hapa nina ushauri maalum kidogo na ninaomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Profesa Shemdoe na Manaibu wako mnisikilize vizuri sana kwenye sehemu hii ya TARURA. Mheshimiwa Rais alimengea wakati fulani, ukisoma kwenye hotuba ya leo hapa TARURA imeongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 940 mpaka shilingi trilioni 1.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni habari njema, lakini lipo tatizo kwenye Barabara za TARURA, na hapa ndipo naomba Serikali mnisikilize vizuri. Hizi barabara maeneo mengi tunajenga kila mwaka, barabara hizo hizo. Tunaweka shilingi bilioni moja mwaka huu, shilingi milioni 500 mwakani, mvua ikija inasomba barabara zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa nchi yetu alitoa maelekezo kwamba, ni muhimu TARURA mkatafuta teknolojia ya kujenga hizi barabara zikae kwa muda mrefu, ili kusudi tukijenga mwaka huu barabara mwakani tusirudie tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa, Profesa ninakuomba sana ukae na wataalamu wako mjifunze teknolojia mpya ya kujenga hizi barabara, ili fedha ya walipakodi isipotee kila mwaka kwa sababu, bila kufanya hivyo ni kama kila mwaka fedha ya wananchi inapotea kwa kusombwa na maji kwenye barabara za TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda Jimbo la Lupembe, Barabara pale Mtwango – Welela kwenda Kichiwa, Barabara pale Itunduma – Ibumila – Ikando kwenda Nyombo haipitiki vizuri kwa sababu, barabara hii mwaka 2025 imejengwa, lakini mwaka huu tena imeharibika. Ukienda kule Njinga kwenda Ikondo, mwaka 2025 imejengwa, mwaka huu tena haipitiki, kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu, tunajenga barabara za tope bila kuwa na teknolojia nzuri, ili hizo barabara ziweze kukaa kwa muda mrefu. Hili Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana mlifanyie kazi, ili kusudi hii fedha iwe na thamani, ili kila mwaka tujenge eneo lingine, kwa ajili ya ufanisi wa barabara zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo wananchi wa Lupembe wamenituma kusema kwa niaba yao, ni kuhusu mikopo ya 10%. Ukisoma kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imetoa mikopo mingi sana, zaidi ya shilingi bilioni 130 zimetolewa, kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliongea wakati fulani hapa ndani ya Bunge, moja ya changamoto kubwa kwenye mikopo hii ya 10% ni hairejeshwi. Ninamshukuru Mungu kwa wananchi wa Mkoa wa Njombe, nimefuatilia Taarifa ya TAMISEMI, Mkoa wa Njombe na Halmashauri ya Njombe DC ni kati ya mikoa ambayo wananchi wake wanaongoza kwa kurejesha mikopo ya 10%. Hongereni sana Mkoa wa Njombe. Watu wa Njombe ni waaminifu sana, lakini maeneo mengi mikopo ya 10% hairejeshwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ya mikopo kutokurejeshwa, na hapa ndipo naomba kushauri, ni huu utaratibu wa kupeana mikopo kwenye vikundi peke yake, hauwezi kuwa na tija. Inawezekanaje unamchukua mtu mmoja mwenye ujuzi wa biashara unasema aunde kikundi na watu watano au kumi, ambao hawajui mambo ya biashara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mikopo hiyo wanagawana fedha, wanaenda kutumia, lakini ukimpa mkopo mfanyabiashara mmoja mwenye biashara, anayejua biashara, anaweza kuajiri wenzake 50 mpaka 100 ikawa na tija kubwa. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali, sheria hii ya mikopo ya 10% ya mwaka 2024 iletwe Bungeni tuifanyie marekebisho, ili mwananchi mmoja mmoja mwenye wazo zuri la biashara, mtu mwenye biashara yake, apate mkopo urejeshwe kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo, tutaendana na Dira yetu ya 2050 ya kusaidia wananchi wetu kuweza kuwa na tija na ajira kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, naomba nichangie kuhusu dawa za kulevya. Tumesoma hapo kwenye Taarifa yetu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu kwamba, watu wa kudhibiti dawa za kulevya wamefanya kazi nzuri sana nchini. Leo hii nchini dawa za kulevya zimedhibitiwa kwa zaidi ya 80%. Ninatumia nafasi hii kuwapongeza sana DCEA na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa udhibiti wa jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwao ni pamoja na mafanikio kwenye dawa za kulevya. Limetokea tatizo lingine, kuna ongezeko kubwa la bidhaa fake mitaani. Zipo pombe nyingi fake mitaani ambazo watu wetu wanaendelea kunywa na zinaweza kuwa na madhara zaidi kuliko hata cocaine na dawa za kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Waziri wa Viwanda, ameanza vizuri, washirikiane na Taasisi ya Kudhibiti Dawa za Kulevya wadhibiti uholela wa pombe haramu, pombe fake na bidhaa fake ambazo zinaweza kuathiri afya za wananchi wetu kuliko hata dawa za kulevya. Hili ni jambo muhimu sana kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa siku ya leo, Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Madiwani, wanaiomba Serikali inapoendelea na mipango yake iangalie uwezekano wa kuona namna ya kuwapa posho watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Madiwani, Wabunge pia waliongea wakati fulani hapa, wanakaa vikao siku mbili, siku moja, Waziri Profesa Shemdoe, atoe maelekezo kwa Wakurugenzi kwamba Madiwani wetu wapate muda wa kutosha kukaa vikao kwenye Halmashauri, angalau kwa siku tano hadi siku saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatuwezi kuwaongezea mishahara, basi wakae vikao muda wa kutosha wajadili vizuri miradi ya maendeleo kwenye halmashauri ili kuwe na tija, lakini pia waweze kujikimu kama viongozi wetu wa halmashauri. Hali kadhalika kwa vijiji na vitongoji vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo Rais wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi aliwahi kutuasa kwamba maisha haya ni hadithi tu. Akasema: "Ewe ndugu yangu, andika hadithi yako vizuri." Ninataka niwaombe viongozi walioko Serikalini, Mawaziri, tuandike hadithi yetu vizuri kwa kupeleka maendeleo kwa wananchi wetu. Asanteni sana. (Makofi)