MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nitoe pongezi zangu kwa Serikali kwa juhudi kubwa inayofanya kuhakikisha mawasiliano yanapatikana, na hasa ninampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeona juzi tu, tarehe 10 Aprili, 2026 alizindua minara 785 kwa ajili ya mawasiliano nchini. Pongezi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa mawasiliano yanaendelea kuimarika, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa urahisi hasa ukizingatia wafanyabiashara wengi wanatumia mitandao kwa ajili ya kufanya biashara zao wakiwemo wanawake?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninamshukuru kwa pongezi kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anayofanya kuhakikisha kwamba nchi hii yote inakuwa na mtandao wa kuaminika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwenye jibu lake kwamba Wizara yetu ina mpango mkakati mkubwa wa miaka mitano ya kuhakikisha kwamba nchi hii yote inakuwa na mtandao wa mawasiliano wa kuaminika na katika hilo, hii itatoa kipaumbele kikubwa kwa makundi maalum yakiwemo akina mama, vijana, wenye ulemavu na watu wengine wote walio katika makundi hayo kama wazee na watu wasiokuwa na uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kuhakikisha, ndani ya miaka hii mitano, kila mwananchi na kila kundi maalum litakuwa na uso wa furaha katika sekta hii ya mawasiliano.