Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Tamima Haji Abass (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo ili kuwa sehemu ya wachangiaji. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia na kunijaalia uhai, uzima na afya njema katika kufanikisha majukumu yangu ya kila siku; ninamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana vilevile, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na uongozi wa chama changu wote, pamoja na uongozi wa Jumuiya ya UWT, kwa kuniamini, wakasema na ninaweza kulisukuma gurudumu hili na kuwa Mbunge kupitia kipindi hiki cha Bunge la Kumi na Tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na wao kwa kuniamini na kunichagua nikaweza kuwakilisha ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anazozifanya kila siku na hatimaye maendeleo kila kona yanaonekana. Vilevile, ametuheshimisha wanawake ndani ya Tanzania na ndani ya dunia kwa jumla. Dunia imetambua kama mwanamke na yeye ni nguzo imara na uongozi anauweza na anaweza kusimamia chochote akiamua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa jitihada zake kubwa za kuing’arisha Zanzibar. Zanzibar imeonekana, kila kona maendeleo yameonekana, tunampongeza sana kwa kazi kubwa anazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani kwa uongozi mzima wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Waziri Mkuu tunampongeza, kwanza kwa kuteuliwa kwa nafasi hii. Anaitendea haki nafasi hii na Mheshimiwa Rais hakukosea kumteua Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kusimamia Wizara hii au kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu pia na shukrani kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi ambacho amekaa tunampongeza sana. Tumeona mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yamefanyika ndani ya Bunge hili kama maboresho ya mitambo, tunampongeza sana. Pia, tunampongeza kwa uendeshaji wake wa kutufundisha, wa kutuendeleza mpaka tukaweza kuwa Wabunge wazuri na tunaweza kutoa michango yetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, niende kwenye mchango wangu sasa kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo ameiwasilisha hapa. Nianze kwenye suala la kuwaendeleza vijana. Vijana ndani ya nchi hii tunasema ndiyo nguvukazi na ni nguvukazi kweli. Sasa, katika kuwaendeleza vijana ni lazima tuwe na mipango imara, mipango thabiti ya kuwasimamia vijana hawa ili wawe vijana bora baadaye wawe wazazi bora. Tutafanya hivyo kwa kuanzisha jitihada za kuwasomesha watoto wetu, kwa sababu watoto ndiyo wanaoanza, baadaye wanakuja vijana. Hawa watoto tuwajengee misingi imara wanapoanza shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kujitahidi kuandikisha wanafunzi wengi sana katika kipindi hiki. Tunaambiwa hadi Februari, 2026, wanafunzi wapya wa shule za awali zaidi ya 70% wameandikishwa na zaidi ya 80% wameandikishwa darasa la kwanza. Hiyo inaonesha wazi kuwa wananchi wamehamasika kuwapeleka watoto shule. Pia wazazi wametimiza wajibu wao wa kuwapeleka watoto wale shule kwa ajili ya kupata elimu bora ili waje wapatikane vijana bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika takwimu ile ya 70% na 86% walioandikishwa tunaona kuwa baada ya muda lile kundi lote lililoandikishwa linafikia mahali wengine wanaishia njiani kutokana na sababu mbalimbali ambazo wao wenyewe wanazijua. Sasa, ni vyema Serikali iwe na mkakati madhubuti wa kuwafuatilia wale watoto wanaoandikishwa kwa kipindi kile. Kama tumeandikisha 70% au 80%, basi tuwafuatilie mpaka ifikie wakati wamemaliza shule na wamehitimu. Kama hatukuwafuatilia tutakuwa tunasema ufaulu umeongezeka, lakini kumbe kuna kundi la watoto wamedondoka njiani, hawajafika hata darasa la saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, niiombe Serikali katika hatua hii tutilie mkazo wale vijana au watoto ambao wanaacha shule mapema kabla ya kumaliza. Kama hatutatilia mkazo, kutokana na wale watoto ambao wataachia njiani tutapata kundi ambalo halisomeki popote. Kama halisomeki popote wakati mwingine unakuta wanajiingiza katika mambo wasiyoyafahamu kwa kufuata mkumbo, kumbe hawakupata misingi bora. Ndipo pale tutakapowatafuta wale vijana bora, hatutaweza kuwapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa hapa kuwa Serikali ina mpango madhubuti wa kuwaendeleza vijana. Sasa, vijana hawa ni lazima watokane na kule wapate ule msingi bora waweze kuja kujiendeleza huku. Hata ile mikopo tunayowapelekea vijana ya 10% hawataweza kuitumia vizuri kama hawatakuwa na elimu au hawana misingi mizuri ya matumizi ya zile fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazazi wengi au wazazi wote wanategemea kuwa watoto wao watakuwa na msingi mzuri na hawatokuwa tegemezi. Kwa sababu, wakiwa tegemezi ile faida ya kuwasimamisha vijana itakuwa haipatikani. Kwa hiyo, ninaiomba sana Wizara ya TAMISEMI ijitahidi basi kusimamia ili watoto wote wapate elimu bora bila ya kujali umri, bila ya kujali wapi anatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika lile kundi linaloacha njiani kuna changamoto ambazo zinajitokeza. Pengine wengine wanakatisha tu masomo kutokana na labda kuna upungufu wa vyoo. Basi ni lazima Serikali hili iliangalie. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, muda wako umekwisha, malizia.

MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)