Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, awali ya yote ninapenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ambaye ameendelea kutusimamia na kutuongoza vyema, tumeweza kutimiza majukumu yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyoonyesha juu yangu. Ninasema ahsante sana mama, hakika nami sitamwangusha. Nitaendelea kufanya kadiri ya maagizo ninayopewa, lakini vilevile kwa mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, naye pia amekuwa ni mlezi mzuri, Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa na Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko. (Makofi)
Pia ninapenda kumshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa maelekezo yake, miongozo, ya namna njema ya kuweza kuwahudumia wananchi kwa kupitia Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Waziri wangu Mheshimiwa Jerry Silaa, naye pia amekuwa ni kiongozi mzuri kwangu na ameweza kunipa nafasi ya kufanya kazi na kuweza kumsaidia pale ilipobidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisimsahau Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge, namna nzuri mliyoifanya kutuwezesha sisi kama Mawaziri kutekeleza majukumu yetu, lakini vilevile kuweza kufanya kazi kwa ukaribu na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote na ninawashukuru sana kwa namna ambavyo mmekuwa na msaada mkubwa katika kutimiza majukumu yangu. Mmeweza kuniuliza maswali mengi nimewajibu, tumeweza kufanya mawasiliano nje ya podium na tumeweza kuhakikisha tunatoa huduma njema kwa wananchi. Waheshimiwa Wabunge, hongereni na asanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kwa namna ambavyo michango iimeendelea katika kuwezesha bajeti yetu hii; ninawapongeza wote kwa namna njema mlivyochangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakwenda kuchangia kidogo sana na kuacha sehemu kubwa Mheshimiwa Waziri Jerry ataendelea nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninapenda kuwashukuru kwa namna ambavyo mmekuwa msaada katika kuona kwamba hasa hii minara 758 na minara 636 tunaweza kuitekeleza katika majimbo yenu. Wakati wote mliponihitaji mliniomba na mimi niliweza kufika, tulishirikiana na tumeweza kuweka imani kubwa kwa wananchi kuona kabisa namna ambavyo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kuipa nguvu Wizara yetu na kuhakikisha suala la mawasiliano linapewa kipaumbele. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, niwatoe hofu, yale maeneo machache ambayo bado hatujayafikia, tutakuja kuhakikisha minara inajengwa na mawasiliano yanaimarika. Maeneo ambayo tuna minara ile ya zamani tunakuja ku-upgrade kuona kwamba lile suala la matumizi ya 3G, 4G liwe kwa wote. Hayo ndiyo malengo ya Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninapenda kuongelea suala la ulaghai mitandaoni na hili limekuwa janga kubwa sana. Ninawapa pole sana wale Waheshimiwa Wabunge ambao pia yamewahi kuwakuta. Suala hili si laana, ni suala la kumshukuru Mungu, ni suala la kumshukuru Mheshimiwa Rais, ni ukuaji wa teknolojia. Tatizo la Watanzania ni matumizi yasiyo sahihi ya ukuaji wa hii teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tutaendelea kuhakikisha tunafanya kazi kwa ukaribu na Wizara ya Mambo ya Ndani, kuona kwamba hawa wote ambao wanakwenda kinyume na matumizi sahihi ya teknolojia ambayo imekua sana hapa nchini, lakini ni mapenzi mema ya Mheshimiwa Rais aliyeruhusu fedha nyingi iweze kutumika na kuona kwamba tunaweza kusimika mifumo ambayo inaenda kutusaidia kuboreka kimaisha, lakini vilevile kiuchumi, kielimu, kiafya. Inaendelea kutusogeza katika mabadiliko makubwa ambayo dunia inataka, lakini vilevile kuona kwamba wananchi pia wananufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu kwa wananchi wote, ninapenda tu kusema kwamba wananchi wote tuwe makini katika matumizi ya ukuaji huu wa teknolojia. Kila mmoja kwanza anapaswa kuwa makini, lakini vilevile kila mmoja anatakiwa atambue angalau vitu ambavyo anaweza kuvitumia wakati wa matumizi ya teknolojia, na kila mmoja aweze kulinda taarifa zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais ameweza kutupa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, lakini na sisi wenyewe lazima tulinde taarifa zetu. Usitoe neno lako la siri kwa mtu yeyote yule, lakini vilevile usitoe taarifa zako kwa mtu yeyote yule ambaye hapaswi kuzichukua, lakini kubwa, usijibu message ambayo hujui nani aliyekutumia, wala usifanye malipo yoyote kwa mtu ambaye humfahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kusisitiza hili kwa wananchi wote, lengo ni kuona kwamba hakuna ambaye ataendelea kutapelika na ndiyo maana tumeendelea kuleta semi mbalimbali ambazo zitatusaidia kila mmoja akumbuke. Kwa hiyo, kila mwananchi akiweka kwenye akili yake na moyo wake kwamba sitapeliki, maana yake hakuna ambaye atatapelika, hakuna ambaye atafanya vitu tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Waziri anakwenda kuongea kwa urefu, mimi niseme nimeona tu niongelee kwa ufupi masuala ya minara, lakini masuala yanayoendelea yasiyofaa kwenye mitandao yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninapenda kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Mbeya kwa kunipa nafasi hii adhimu. Heshima kubwa waliyonipa wanawake wa Mkoa wa Mbeya ninasema tu kwamba nimejitahidi kufanya kadiri ya uwezo wangu na Mungu amenifikisha hapa, lakini tarehe 28 Juni na mimi nitakwenda kuchukua fomu kwa dhamira ya kuendeleza maendeleo ya kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muumini wa siasa na uchumi na tumeshaanza kufanya mwanzoni hapa. Ninaamini sasa kwa phase inayofuata tutakwenda kufanya mambo makubwa sana na wanawake wote wa Mkoa wa Mbeya tutakwenda kuimarika kiuchumi zaidi, ambapo itatusaidia kiafya, lakini vilevile katika kuimarisha familia zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea hayo kwa ufupi, ninashukuru sana kwa hii nafasi, ninashukuru sana. (Makofi)