Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava (4 total)

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa watumishi wetu, vijana wetu wanajitolea katika sekta ya afya pamoja na elimu wanapotuma maombi huwa wanaambatanisha ile barua ya taasisi ambayo walikuwa wanajitolea, kwa nini hawapewi kipaumbele?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwisha kueleza kwenye swali letu la msingi, kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma kwamba ajira zote kwa sasa zinatolewa kwa njia ya ushindani ili kutenda haki kwa watu wote, ili kupata usawa, hivyo basi, msisitizo unaendelea kuwekwa kwamba vijana wanapopata nafasi ya kujitolea, wajitolee ili kujijengea uzoefu na wapate ujuzi na maarifa ili yale waliyoyapata darasani waende kuyatumia katika vitendo na mwisho linapotokea suala la ajira basi washiriki katika ushindani ili waweze kuajiriwa Serikalini.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, TARURA imekuwa ikijenga barabara kwa kiwango cha lami kwa baadhi ya centre, lakini katika Halmashauri ya Shinyanga, Jimbo la Solwa hakuna Kata ambayo ina barabara ya kiwango cha lami, ni lini Serikali itatujengea angalau kwenye Makao Makuu ya Halmashauri barabara kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mpango wetu wa barabara za vijijini na mijini tunazo barabara za udongo, barabara za changarawe na barabara za lami, na tumeweka kipaumbele kuendelea kuongeza barabara za lami, hususan maeneo ya miji ili kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie kwamba tunapoendelea na bajeti zetu, tutatoa kipaumbele kwenye eneo la Jimbo hilo la Solwa na hizo barabara za Kata zile ambazo zinawezekana kujengwa kwa awamu, tutaanza ujenzi kwa awamu.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, Kata ya Didia ambayo iko Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ni ya kimkakati, ina idadi kubwa ya watu na ni kata ambayo inazalisha sana zao la mpunga. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya katika kata hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninampongeza sana dada yangu, Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, amekuwa mfuatiliaji wa karibu
kuhusiana na ujenzi wa kituo cha afya kwenye kata hiyo ya kimkakati katika Wilaya ya Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inaendelea kufanya tathmini na kuainisha kata zenye idadi kubwa ya wananchi, ambazo ziko umbali mrefu kutoka vituo vya karibu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya.
Tutahakikisha tumetoa kipaumbele katika kata hiyo, ili kwa awamu tuendelee kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kila kata.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya migogoro ya ardhi imekuwa ni nyingi sana na wananchi wanaongezeka na mipaka iko vile vile, je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kupunguza maeneo ya hifadhi kuwagawia wakulima na wafugaji ili kupunguza migogoro hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa swali zuri na nia njema ya kutaka kupunguza migogoro hii, na kimsingi kuzuia.

Mheshimiwa Spika, huku tukifahamu, idadi ya watu inazidi kuongezeka na ardhi yetu bado ipo vilevile, haiongezeki, Mheshimiwa Waziri Mkuu, ametueleza, ni sisi kuwa na mipango mizuri ya matumizi ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Bunge hili limepitisha fedha kwa ajili ya kupanga matumizi bora ya ardhi. Tunachotakiwa sisi wafugaji na wakulima, tuwe na mipango mizuri ya kujua na kufuga kisasa na kulima kisasa. Hakutakuwa na migogoro.

Mheshimiwa Spika, pia hakutakuwa na ardhi ya kutosha kwa sababu ardhi imebaki vilevile na idadi ya watu inaongezeka. Hivi niwasihi wafugaji, tufuge kisasa kwa kuwa na malisho ya kimkakati ya kulima wenyewe na tusiende kuvuruga mipango ya matumizi mengine ya hifadhi ya ardhi yetu. Ninaomba kuwasilisha.