MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa changamoto ya wananchi wa Kalenga ni ukamilishwaji wa barabara hiyo. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha wanatafuta mpango wa muda ili barabara hiyo iweze kupitika na wananchi wa Kalenga waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa vizuri zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Changamoto inayowakuta Kalenga inalikuta pia Jimbo la Temeke katika eneo la Buza, barabara ya kutoka kwa Mama Kibonge, Mashine ya Maji mpaka Azimio. Barabara hiyo imekuwa ni changamoto, kwani unafika mahali magari hayapiti, wananchi wanashindwa kwenda hata kwenye kituo cha afya.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha wanatengeneza utaratibu wa muda ili barabara hiyo ipitike, wananchi waendelee na shughuli za kiuchumi wakati tukimsubiri mkandarasi aingie na kutengeneza barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, ukamilishwaji wa kipande cha barabara kilichobaki cha kilometa 0.9 unakwenda kufanyika kwenye mwaka huu wa fedha 2025/2026, na Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga fedha, shilingi milioni 829 kwa ajili ya kazi hiyo na ujenzi utakwenda kuanza mara moja, kwa sababu fedha hiyo ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza ambalo limegusa Wilaya ya Temeke, ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na kwenye wilaya zote tano za Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza Mradi wa DMDP2. Imetenga milioni 438 Dola za Kimarekani kwa ajili ya kuendeleza miundombinu yote ya msingi ikiwemo barabara aliyoitaja ndani ya Wilaya hiyo ya Temeke, na hivi sasa tuko kwenye hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo barabara ambazo tumeshawapa wakandarasi waendelee na kazi na zipo barabara ambazo tunaendelea na usanifu kwa ajili ya kutangaza zabuni na kuanza kazi mara moja.