MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE aliuliza:-
Je, Serikali imechukua hatua gani kudhibiti mikopo hatarishi yenye riba kubwa inayotolewa na baadhi ya Taasisi zisizo rasmi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nami nichukue wasaa huu kuweza kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Fedha. Pia nimwahidi pia kwamba nitafanya kazi kwa uwezo wangu wote, nguvu zangu wote na akili zangu zote kulitumikia Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho basi niwashukuru pia Wananchi wa Jimbo langu la Kavuu kwa kura nyingi kwa Mama Samia na mimi mwenyewe. Baada ya hapo, basi ninarudi kwenye swali la Mheshimiwa Dkt. Neema Peter Majule, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha nitajibu swali hili. Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania na wadau wengine, imechukua hatua mbalimbali za udhibiti wa mikopo hatarishi yenye riba kubwa inayotolewa na baadhi ya taasisi zisizo rasmi. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na zifuatazo:-
(a) Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuwa utoaji wa mikopo unapaswa kufanywa na watu wanaotoa huduma wenye leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 2006, pamoja na Sheria ya Huduma Ndogo za fedha ya mwaka 2018;
(b) Kuwatambua na kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watoa mikopo wasioidhinishwa. Katika kutekeleza hatua, programu zaidi ya 69 za mikopo ya kidigiti zilizobainika kutoa mikopo bila leseni zilisitishwa na programu 126 zilifungiwa;
(c) Pamoja na mwongozo maalum wa utoaji huduma za mikopo ya kidigiti ili kuhakikisha uwazi, uendeshaji wa kimaadili, utoaji wa taarifa kamili kuhusu gharama za mikopo, pamoja na ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha; na
(d) Kuandaa rasimu ya kanuni za kusimamia mikopo ya kidigiti, ambazo zinatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2026/2027. Kanuni hizo zinalenga kuimarisha udhibiti wa wakopeshaji wa kidijiti nchini Tanzania.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, lini Kituo cha Forodha katika Jimbo la Momba kitaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichwale, Mbunge wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vituo vya forodha ikiwemo katika Jimbo la Momba hufanyika kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali, ukamilifu wa taratibu na kanuni za kiforodha, utayari wa nchi jirani tunazopakana nazo, masuala ya kiusalama, upatikanaji wa rasilimali fedha, pamoja na tathmini ya umuhimu wa eneo husika katika shughuli za biashara za mipakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kufanya tathmini ya mahitaji ya ujenzi wa Kituo cha Forodha katika Jimbo la Momba ikiwemo upembuzi yakinifu, upatikanaji na utambuzi wa eneo, na gharama za mradi na utayari wa nchi jirani. Aidha, eneo hilo linaangaliwa kwa kuzingatia ongezeko la shughuli za biashara na umuhimu wake katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa biashara mipakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kituo hicho utaanza mara baada ya kukamilika kwa maandalizi yote muhimu, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa fedha za utekelezaji wa mradi katika bajeti ya Serikali na kutangazwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na maandalizi na itatoa taarifa rasmi pindi ratiba ya utekelezaji wa ujenzi itakapokamilika.