Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Paschal Inyasi Chinyele (2 total)

MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Mitaa hii mitano na siyo Kata, Mitaa hii mitano ilipimwa kama vijiji mwaka 1973. Je, ni hatua gani Serikali inachukua kuwanusuru wakazi wa Kata hii ya Mbalawala wapatao takriban 12,000 ambao wanategemea ardhi hii kwa maisha yao ya kila siku? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakati Serikali inajiandaa kutwaa Bonde la Mzakwe iliwafidia wakazi wa vilivyokuwa vijiji vya Mzakwe na Mchemwa, baadhi kuwahamishia katika Kata ya Chahwa ambayo sasa hivi iko kwenye Jimbo la Mtumba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia wakazi wa mitaa hii ya Kata ya Mbalawala ili wapishe Bonde la Mto Ruvu kama ilivyowafidia waliokuwa wakazi wa Vijiji vya Mzakwe na Chahwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Inyasi, Mbunge wa Dodoma Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali la pili, kwa maana kwamba sisi TAMISEMI ndiyo wamiliki wa ardhi, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuona namna gani ya kuendelea kuwafidia wale ambao hawajapata kwa sababu Serikali imeendelea kutoa fidia katika maeneo mengi sana nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja na Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Ardhi kuona namna gani tunaweza tukafikisha maendeleo haya kwa wananchi wetu kwa maana ya kwamba vijiji vimeshapimwa toka mwaka 1973, tuone namna gani sahihi ya kuendeleza eneo hili. (Makofi)
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini Serikali itatekeleza mpango wa ujenzi wa viwanda katika kongani za viwanda katika kata za Nala pamoja na Mpunguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini, kwa kuwatetea wananchi wa Dodoma, hususan wananchi wa Nala na wananchi wa Mpunguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wetu wa miaka minne, tume-commit kuanzisha miradi saba ya kielelezo (National Flagship Programs). Katika ile miradi saba ya kielelezo, tunakuja kuanzisha kongani ya viwanda eneo la Nala ambayo kimsingi tunaweka pale viwanda vya kuchenjua dhahabu kwenye madini ambayo ni rare na critical, kwa mfano lithium, cobalt, nickel na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa eneo la Mpunguzi tumelitenga kama eneo la mkakati kwa sababu Mpunguzi wanazalisha sana zabibu. Kwa hiyo, ninamwondoa mashaka Mheshimiwa Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini, kwamba hili lipo kwenye mpango wetu wa miaka mitano. Pia, tumeliingiza na kwenye mpango wa mwaka mmoja, tumelitengea bajeti. Ninashukuru. (Makofi)