Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa ninaomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na mimi binafsi ninashukuru kwa mara ya kwanza kusimama katika Bunge hili kutoa hoja. Pia, ninamshukuru Mwenyezi Mungu, watu wa Dodoma tumepata mvua nzuri tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu. Ninamshukuru vile vile Mheshimiwa Rais kwa kunikubali mimi kugombea katika Jimbo la Dodoma Mjini, ninashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia wakazi wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa kuniamini na kunichagua kwa kura nyingi mimi pamoja na Mheshimiwa Rais na Madiwani. Wamekiheshimisha sana Chama Cha Mapinduzi na mimi binafsi ninaahidi kutumia nguvu zangu zote kuhakikisha kwamba matarajio yao yanafikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kufanya mambo mengi katika Jimbo la Dodoma Mjini, lakini kwa haraka haraka tu niseme, tumejengewa SGR, sasa hivi watu wa Dodoma tunapata usafiri kwa urahisi zaidi kwenda Morogoro na Dar es Salaam, hospitali pamoja na vituo vya afya kadhaa vimejengwa, miradi ya maji na umeme, barabara hii ya mzunguko pia tumejengewa kiwanda kikubwa cha mbolea katika eneo la Nala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni baadhi, yapo mengi kwa sababu ya muda nitajikita katika maeneo matatu na niseme tu ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri iliyosheheni matumaini makubwa wa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo na mimi ningependa nijadili ni suala la uchukuzi ambalo katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ameliweka suala hili vizuri katika ukurasa wa 32 na ninaomba nisome kwa jinsi lilivyowekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameeleza kuhusiana na kufungamanisha sekta za uchukuzi, sekta hizi zinapofungamanishwa zinaleta tija kubwa sana kwa uchumi wa nchi. Ninaomba niseme tu, katika Jimbo la Dodoma Mjini tumepata bahati ya kupitiwa na barabara ya mzunguko (ring road), katika eneo la Zuzu barabara hii inakutana na SGR, reli ya mwendokasi. Hata hivyo, katika kituo hiki hakuna kituo cha SGR ni ombi la wakazi wa Dodoma Mjini kwamba eneo hili la Zuzu lipate stesheni ya SGR kwa kuwa tayari kuna access road ambayo ni ring road.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vituo kadhaa ambavyo SGR inapita kwenda Dar es Salaam, maeneo ya Soga na Gulwe, Serikali ya Dkt. Samia inajitahidi sana kujenga access roads lakini hapa Zuzu tayari ipo access road ambayo inakwenda katika maeneo mbalimbali, hii barabara inashika maeneo ya Nala, Mbalawala, Bihawana, Matumbulu mpaka Mpunguzi, kote huko inafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jirani kabisa na hiki kituo ambacho tunapenda kijengwe cha Zuzu kuna kongani ya viwanda inatarajiwa kujengwa katika eneo la Zuzu, ambapo ni maombi ya wananchi kwamba litoke tawi la reli ya SGR kutoka hapa Zuzu kuelekea Nala ili mizigo itakayokuwa inakwenda kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hivi ipite kwenye reli badala ya kupita kwenye barabara zetu ambazo zinajengwa kwa gharama sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande mwingine ambao ningependa nichangie ni sekta ya ujenzi ambayo katika ukurasa wa 28 imewekwa vizuri na ninaomba ninukuu. Mheshimiwa Rais amesema hivi; “eneo lingine tutakalolipa uzito mkubwa ni sekta ya ujenzi. Kipaumbele kitakuwa ni kukamilisha miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara ambazo tayari zimeanza na zinaendelea. Tutaendelea na kasi ya utekelezaji wa miradi ya barabara pia TANROADS ili kufikia lengo la kuunganisha barabara za Makao Makuu ya Wilaya na Mikoa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana ya kujenga barabara za nchi hii, ningependa nitoe wito kwa vijana wetu katika nchi hii na niseme tu kwamba nchi hii imetoka mbali sana katika sekta ya barabara. Miaka ya kabla ya 2000 wakazi wa Dar es Salaam na maeneo mengine kama Morogoro na Dodoma walikuwa wanakwenda katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kutumia treni peke yake. Hakukuwa na usafiri mwingine zaidi ya treni, ilikuwa inachukua hata siku tatu na hiyo ni katika hali ya kawaida, lakini ikitokea reli imekwama katika maeneo ya Kidete kwa mfano, ambapo kila mara huwa kuna shida wakati wa mvua, basi abiria walikuwa wanaweza kukaa njiani hata kwa wiki nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika mbali katika ujenzi wa barabara ambapo kwa sasa Mheshimiwa Rais amefanikiwa kujenga kilomita 11,900 hadi 12,197 za barabara nchi nzima. Tuko mbali katika barabara na suala hili Watanzania tunapaswa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake hizo. Nitatoa mfano mdogo wa hii Barabara ya Ring Road, barabara hii ni barabara ambayo ni ya mfano. Nilikuwa najaribu kupitia nchi mbalimbali kuona ni nchi zipi ambazo zina barabara zenye urefu kama huu, tunaambiwa kwamba barabara hii ya ring road ambayo ina kilomita 112 .3 ni barabara kubwa kuliko zote katika Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeenda mbali zaidi nikaangalia Morocco pamoja na South Africa, lakini nimekuta wote wana barabara za ring road ambazo zina urefu mdogo. South Africa wana kilomita 83, Morocco wana kilomita 41 ni Misri peke yake ina kilometa 400 ambayo ndiyo inatuzidi, sisi ni wa pili tunayo barabara ambayo kwa kweli ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta wote wana barabara za ring road ambazo zina urefu mdogo. South Africa wana kilometa 83, Morocco wana kilometa 41; lakini ni Misri peke yake ina kilometa 400, ndiyo inayotuzidi. Sisi ndiyo wa pili na tuna barabara ambayo kwa kweli ni kubwa. Barabara hii ya ring road inasaidia sana ufikaji katika Jiji la Dodoma. Ninasema tu, ndugu zangu wanaotoka Iringa na wanakwenda labda mji wa Serikali, hawana haja tena ya kwenda mjini, wanafika Matumbulu wanaingia moja kwa moja Mji wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu pia wanaotoka Mwanza, Shinyanga na kadhalika, wakifika maeneo ya Nala hawana haja tena ya kuja mjini, wanaingia kushoto, wanapita Veyula wanakwenda Mji wa Serikali wanakuwa wameshamaliza. Kwa hiyo barabara hii ni msaada mkubwa sana kwa sisi Watanzania hasa ndugu zangu tunapoingia katika Mkoa wa Dodoma, kwa hiyo barabara hii ni nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: …barabara katika mkoa wetu, tuna Barabara kutoka Mjini Dodoma kuelekea Mvumi. Barabara hii ni ya muhimu na wananchi wetu ambao wanapitiwa na hii barabara hawajalipwa fidia. Ninapendekeza walipwe fidia zao kwa sababu ni haki yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umeisha.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)