Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Ramadhani Hamza Singano (2 total)

MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika mipango mizuri ni kuweka mipango ya muda mfupi ya kati na ya muda mrefu. Sasa kwa kuwa wananchi wa Tanga wameshahamasika sana na zao hili la maziwa, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuhakikisha kwamba wananusuru mapato haya yanayopotea katika zao la maziwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana. Nami ninampongeza sana Mbunge mwingine wa Mkoa wa Tanga ambao kwa kweli kwa kiasi kikubwa wanafuatilia mgogoro huu kwa karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza katika swali la msingi, mgogoro huu ni kipaumbele chetu kwa sasa. Tunaendelea kutafuta solution za muda mrefu, lakini hata za muda mfupi ikiwa ni pamoja na kuona namna gani tunaweza kutenga fedha kadri zinavyopatikana kuongeza juhudi ya kuhakikisha tunazuia upotevu wa malighafi hii ya maziwa kwa wafugaji wetu wa Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunaendelea kulifanyia kazi kwa karibu sana.
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Soni ni miongoni mwa miji mikubwa kibiashara kwa Jimbo la Bumbuli. Ni lini Serikali itafikiria kuwa na soko la kimkakati, kwa ajili ya kuongeza uchumi na kipato kwa wananchi wa Bumbuli?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuhakikisha maeneo yote yenye sifa za kujengewa miundombinu ya stendi, masoko na miundombinu mingine inaendelea kujengwa kwa awamu. Wajibu wa halmashauri ni kuandaa maeneo, kuandaa michoro, kuandaa makadirio na kuanza kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya ujenzi na kuwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ili Serikali pia iendelee kuandaa bajeti, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Bumbuli, Engineer kwamba, tunatambua suala hilo. Serikali hii itakwenda kulitekeleza, lakini halmashauri pia waanze kutenga fedha kwa awamu, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.