Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nikushukuru kwa kuniona ili niweze kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia kila rehema za kuwepo hapa. Mwenyezi Mungu ambaye hata ambayo bado hayakuwa anajua ikiwa yatakuwa, yatakuwaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu kipenzi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi makubwa ya kuwa Rais wa maono kugusa nyoyo za watu, lakini kuwa na mipango ambayo siku zote inaleta tija katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu, ambaye naye ni kiongozi wa maono akitembea kama alivyo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hili tumelidhihirisha pale ambapo alikuwa katika ziara za kimikoa, alipopita katika Mkoa wa Tanga, lakini Wilaya ya Lushoto halafu akafika Jimbo la Bumbuli ambalo mimi ndiyo mwakilishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru pia Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii iliweza kufika Bumbuli Jimbo ninaloliwakilisha katika Kiwanda cha Mponde na walitoa tabasamu kubwa kwa wananchi wa Mponde kwa kuongelea, kupokea na kushauri kuhusu matatizo ya kiwanda hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi mzuri utamwona. Katika mashairi ya Ndugu Shaaban Robert alieleza sifa ya viongozi wazuri na viongozi wabaya, lakini viongozi wabaya alitumia mnyama kuku kwa sababu kuku ni mnyama yupo karibu sana na binadamu. Kwa kutumia lugha za vinaya na lugha za majazi akasema:
“Kuku akipata nyama, hukimbia ale peke,
japo wenzake watamuandama waishike,
katu hatokubali, iondoke mdomoni,
atatafuta mahali, ajilie kwa makini,
kuku akipata nyama, hukimbia ale peke.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama Samia hayuko hivyo. Mama Samia yuko kama yule kiongozi aliyesifiwa na mwanafalsafa mmoja akiitwa Christopher Robin akamwambia: “You are braver than you believe, you are stronger than you seem and you are smarter than you think.” Christopher Robin walikuwa wakibishana sana na huyu jamaa yake, lakini kwa sababu ni mzalendo hakuacha kumsifia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye yale maeneo machache ambayo ninataka niyagusie. Kwanza kabisa ni eneo la afya. Ninashukuru sana Katika Jimbo la Bumbuli Mama Samia wakati ameingia tayari ametupatia zahanati 17. Mambo ya ajabu sana, mapinduzi makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vituo vinne vya afya ambavyo viwili wakati wake vilianza na vingine ameviboresha hapo nyuma. Niombe sasa kidogo, maana imeandikwa katika Waraka wa Kwanza wa Wathesalonike 5:17-18 kwamba, “Ombeni pasipo na kikomo na shukuruni katika kila jambo.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiki Kituo kimoja cha Milingano, kimejengwa lakini hakijaweza kukamilika. Sasa ili tabasamu liwafikie wana Bumbuli niombe katika Wizara hii ya TAMISEMI sasa wakikumbuke kituo hiki ambacho kitaleta tabasamu kwa Watanzania walioko Bumbuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nihame niende kwenye eneo la elimu. Eneo la elimu Katika Jimbo la Bumbuli kuna mageuzi makubwa na Mama Samia avishwe taji lake. Hata hivyo, zipo shule chache kwa sababu ya umbali, basi hapa tutahitaji kupata mabweni kutoka eneo moja linaitwa Kwebamba kuja Kata ya Milingano, Sekondari ya Mibukwe. Kumbukeni Waheshimiwa Wabunge, umri tuliosoma sisi miaka ile ni tofauti na sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabinti wanachukuliwa kule kilometa 30, wanaenda sekondari inabidi wapangishiwe maeneo ya kuishi bila uangalizi. Kwa hiyo, eneo hili linahitaji mabweni ambayo yatasaidia watoto wa kike kupata haki yao ya elimu katika hali ya utulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee kwenye eneo la vijana, wenzangu wamegusa maeneo mengi muhimu. Ninaomba nikumbushie tu suala la NIDA ni tatizo na niombe tamko maalum litoke ili wale wanaopaswa kutekeleza hilo wafanye mara moja, kwa maana vijana wanakosa fursa hii ya mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee tena katika eneo muhimu, eneo nyeti la barabara. Kwanza nianze kuomba kabla sijashauri niombe Barabara ya Mbelei – Ibaga – Mgwashi – Mkongowi – Milingano kilometa 42 ni barabara ya kimkakati. Ilijengwa kidogo na TARURA, lakini labda ni kwa sababu ya bajeti ghafla wakaondoka. Niombe hii ikumbukwe ili kuzidi kuleta tabasamu kwa Watanzania walioko pembeni mwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo ni kipaumbele pia kwa Wanabumbuli ni kilometa 22 kutoka Soni hadi Bumbuli – Dindila, lakini awamu ya kwanza kilometa 22 upande wa Bumbuli na kilometa 9.3 kwa upande wa Korogwe Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi muda ni mchache, lakini niombe kuna barabara ya kimkakati inayounga majimbo matatu: Jimbo la Mlalo, Jimbo la Lushoto, Jimbo la Bumbuli na hatimaye Korogwe Vijijini kilometa 87.3 ambayo ni Barabara ya Magamba – Mlola – Makanya – Milingano – Mashewa, hii nayo ni barabara ya kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mfupi niende kushauri kwa wenzangu wa TARURA, mimi ni Mhandisi niliyesajiliwa na Bodi ya Uhandisi nilitaka niwashauri kidogo katika mambo ya kitaalam. Muda usipotosha basi nitafikisha kwenye meza ya ndugu yangu Mheshimiwa Shemdoe ili aweze kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kwa sababu ya mvua nyingi na mabadiliko ya tabia ya nchi ndiyo yanasababisha hilo. Basi ni vizuri sanifu zetu ziwe ni Climate Resilience Design, kwa maana miundombinu iweze kustahimili mvua nyingi katika maeneo ya milima na maeneo mengine ya tambarare, lakini mifereji ya pembeni (side drains) ziwe za kutosha, lakini na mitaro ya kupunguza kasi ya maji ambayo kitaalam wanaita catch water drains. Kwa sehemu za tambarare kuna vitu vingine tunaita mitre drains zikiwekwa za kutosha zitaweza kuondoa maji haraka barabarani, lakini kutumia makaravati mengi na madaraja kwa maeneo ya milima huwa barabara zetu hazina tofauti na mfano wa nyoka kwa sababu ya kwenda na contour za milima..
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukakuta mto mmoja umeukatiza mara tano. Kwa hiyo, maeneo ya milima yapewe kipaumbele cha makalavati ili maji ndiyo adui wa kwanza. Wakati ninasoma Chuo Kikuu profesa wangu alinishangaza sana aliniambia adui wa kwanza wa barabara ni maji, adui wa tatu ni maji, wa pili na wa tatu kwenye barabara ni maji. Kwa hiyo, hii alikuwa akionesha msisitizo kwamba maji yasipotafutiwa njia yana kawaida ya kutafuta njia yake na hapo ndipo uharibifu utakapokuwa unatokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe tunadhibiti maporomoko katika maeneo ya milima. Tujitahidi kuweka buffer zones ambazo mtu haruhusiwi kufanya shughuli zozote za kibinadamu ikiwepo kilimo na kupanda nyasi pamoja na miti rafiki ambayo itazuia mmomonyoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo lingine, mambo ni mengi, lakini nitayaandika ila niende eneo la ushirikishwaji wa jamii katika kutunza barabara. Hili jambo hapo nyuma lilikuwepo na wenzetu wa TANROADS kabla ya TARURA zilikuwepo hata kambi za ujenzi, ilikuwepo pale Mkuranga, ilikuwepo kambi ya ujenzi pale Manga ukielekea Tanga na maeneo mengine. Hizi zilifanya vizuri kwa sababu emergence zikitokea (dharura zikitokea) walikuwa wakizikabili mara moja. Sasa kwa sababu sina wasiwasi na TARURA, sina wasiwasi na wataalam wa Tanzania ninadhani walikalie hilo waliangalie upya, lakini jamii ishirikishwe kwa matengenezo madogo madogo na mikataba midogo midogo ambayo ni community-based contracts.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoa elimu ni muhimu kwa jamii hii athari gani itapatikana ikiwa mifereji itakuwa haijadhibitiwa, ikiwa mifereji itakuwa imezibwa na watu wanaofanya shughuli za kilimo. Pia, kuunda vikundi vya ulinzi wa barabara kwa maeneo husika, leo barabara imekuwa ndiyo moyo wa Watanzania, barabara leo kama haipitiki, shughuli za biashara hazitafanyika, watoto hawataenda shule kwa sababu zitabomoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende pia katika eneo la kuweka vipaumbele katika barabara: barabara zetu ni lazima tuziwekee vipaumbele, tutenge barabara kwa makundi, ziwepo barabara za kiuchumi kwa maana ya barabara ambapo tutapitisha mazao na kwenda kwenye minada na masoko. Ziwepo barabara za huduma muhimu kwa mfano huduma za hospitali, lakini na kwenda shule, hizi barabara zipewe kipaumbele. Ukiangalia katika mtandao, Wilaya ya Lushoto ni zaidi kilometa 1,200 na kwa Bumbuli tuna kilometa 544. Kwa kuwa haya mambo ni ya kitaalam zaidi niombe niyafikishe kwenye meza ya Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Shemdoe, nami sina wasiwasi naye, atayafanyia kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache nikushukuru sana na niwashukuru viongozi wetu kwa kujitahidi kuonyesha tabasamu kwa Watanzania. Ninashukuru sana kwa kupata nafasi hii. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante kwa mchango wako.
MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)