Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Onesmo Merdson Mnkondya (2 total)

MHE. ONESMO M. MNKONDYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha mbolea inapatikana kwa haraka wakati wa msimu wa kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Onesmo Merdson Mnkondya, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mbolea inapatikana kwa wakati kwa wakulima. Mikakati hiyo ni pamoja na kuandaa mahitaji kwa wakati, kuhusisha vyama vya ushirika kusambaza mbolea na kuhamasisha kampuni za mbolea na mawakala binafsi kufungua vituo vya mauzo ya mbolea kwenye maeneo ya uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada hizo, Kampuni za mbolea za OCP, METL, ETG Inputs Limited, ITRACOM, MINJINGU, One Acre Fund, Premium Limited, na AFRISIAN zimefungua ghala nane za mbolea katika Wilaya ya Mbozi na kusajili mawakala 174 ili kusambaza mbolea kwenye jumla ya vituo vya mauzo 85 katika wilaya hiyo. Lengo ni kuhakikisha mbolea zinapatikana kwa wakati ili wakulima waweze kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo.
MHE. ONESMO M. MNKONDYA aliuliza: -

Je, lini Serikali italipa fidia kwa Wananchi waliopisha eneo la JKT Itaka?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, ni mara yangu ya kwanza kuzungumza mbele ya Bunge lako, ninaomba nitumie wasaa huu kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Mbunge, lakini pia, kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Onesmo Mnkondya, Mbunge wa Mbozi, kwanza kwa namna anavyofuatilia suala la malipo ya fidia ya wananchi waliopisha eneo letu la JKT Itaka lililopo Mbozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inakiri kufanya uthamini katika maeneo ya Kikosi cha 845 KJ kilichopo Itaka JKT, ili kulipa fidia kwa wananchi wanaotarajia kupisha maeneo hayo kwa ajili ya matumizi ya jeshi letu. Uthamini huo ulifanyika Mwaka 2022 na kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali (Chief Valuer) mwaka wa fedha 2023/2024 ukiuhusisha maeneo ya Vijiji vya Sasenga, Mbozi na Itewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla kuu ya gharama ya fidia kulingana na Mthamini Mkuu wa Serikali ni shilingi 5,715,942,200. Kati ya fedha hizo zimegawanywa katika makundi matatu ambapo, kundi la kwanza litalipwa shilingi 3,491,271,800. Hii ni kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wapatao 312 katika Kijiji cha Sasenga, shilingi 74,358,600 inawalipa wananchi wanne katika Kijiji cha Mbozi na mwisho ni shilingi bilioni 2.15 ambayo hii inawalipa wananchi 150 katika Kijiji cha Itewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majedwali ya uthamini au valuation ya kulipa fidia yamewasilishwa tayari Hazina (Wizara ya Fedha), ili taratibu za uhakiki na ulipaji ziendelee. Aidha, Wizara inaendelea kuwasiliana kwa karibu na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili kuhakikisha wananchi wetu wanalipwa fidia zao kulingana na uthamini uliofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba wananchi hawa waendelee kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho Serikali inashughulikia suala lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.