Answers to supplementary Questions by Hon. Rahma Riyadh Kisuo (4 total)
MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
kwanza kabisa nishukuru kwa majibu mazuri ya Wizara, na
niipongeze Serikali kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa sana
umefanyika katika sekta ya elimu. Kuna mikakati mingi imefanyika
na Serikali ya Awamu ya Sita, lakini nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na miradi
hii ya kimkakati kutoa ajira kwa vijana, je, Serikali ina mpango wa
kuweka Sera au miongozo itakayolazimisha miradi yote ya uwekezaji kutenga asilimia maalumu ya ajira za kitaalamu kwa
wahitimu hawa wa vyuo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA
MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO): Mheshimiwa Mwenyekiti,
ninakubaliana na mwuliza swali 100% kuwa miradi ya kimkakati
imeonesha uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira. Hata hivyo, Sera za
Ajira zinaelekeza ajira zitolewe kwa ushindani bila kutoa
upendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri
Mkuu, Wizara ya Kazi, Ajira, na Mahusiano inaendelea kusimamia
utekelezaji wa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni (Na.1) ya
Mwaka 2015, ambapo pamoja na mambo mengine inaelekeza
wafanyakazi wa kigeni yaani wataalamu kurithisha ujuzi kwa
wazawa katika ajira za kitaalamu ili pale kibali cha kazi cha
wageni kitakapokwisha, mzawa aweze kuchukua nafasi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali itaendelea kutoa
kipaumbele kwa wafanyakazi wazawa katika miradi ya kimkakati
kwa nafasi za kazi ambazo utaalamu wake siyo adimu katika soko
la ndani ya ajira. (Makofi)
MHE. ASHA J. FERUZ: Mheshimiwa Mwenyekiti, jina langu ni
Asha Juma Feruz, Mwakilishi ninayewakilisha kundi la Vyuo Vikuu.
Ninaomba kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani
maalumu katika kutumia fursa za ajira katika kundi la vyuo na
vyuo vikuu kupitia mahusiano ya kikanda na kidiplomasia
tuliyonayo hasa zile kozi tunazoziita rare professionals? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA
MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO): Mheshimiwa Mwenyekiti,
Serikali kwa kushirikiana na vyuo na vyuo vikuu, imeanzisha
mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo
katika ngazi mbalimbali za elimu za vyuo na vyuo vikuu na vyuo
vya kati ikiwa ni sehemu ya mtaala ili kuwawezesha kuhitimu elimu
katika ngazi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali inatoa Mafunzo ya
Internship yanayojumuisha wahitimu wa ujuzi wa ngazi mbalimbali
za elimu hususan elimu ya juu na kati ambapo wanapatiwa fursa
ya kujifunza kwa vitendo mahali pa kazi. Lengo la mafunzo hayo
ni kuwapatia wahitimu ujuzi, maadili ya kazi, uzoefu na kufanya
kazi za taaluma zao na kuwawezesha kuajirika. (Makofi)
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya ngongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, utaungana na mimi kwamba, katika majibu yake ya msingi kuna programu mbalimbali ambazo wamezianzisha kupitia Wizara hii. Nataka kufahamu programu hizo zilizoanzishwa, kama Wizara, imechukua hatua gani ya kuwasaidia vijana, hasa wa vijijini kuzijua fursa hizo na kuweza kuzipata kwa urahisi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kuna vijana wana vipaji mbalimbali, lakini vijana hao Serikali bado haijawatambua na kuwawezesha kiujumlajumla. Nataka kujua ni upi mpango wa Serikali wa kuwasaidia vijana hao moja kwa moja, ili zinapotoka fursa hizo waweze kuzipata kwa haraka, hususan katika mikopo mbalimbali? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO) K. n. y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Latifa Juwakali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kuwezesha programu hizi kuwafikia vijana wa vijijini imeanzisha utaratibu wa kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii, vyombo vya habari, redio na magazeti. Aidha, elimu imekuwa ikitolewa kupitia makongamano na maadhimisho mbalimbali. Vilevile, baadhi ya fursa hizi zimekuwa zikibandikwa katika mbao mbalimbali za matangazo za watendaji kata na vijiji.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Muhsin Ussi, swali la nyongeza. Mawili, endelea.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutambua vijana wenye vipaji na kuwaunganisha katika fursa mbalimbali Serikali, kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika Mfuko wa Uwezeshaji wa shilingi bilioni 200 za Mama kwa Vijana, Wizara hii imepewa jumla ya shilingi bilioni 30 za kuwawezesha vijana katika sekta ya ubunifu nchini, ikiwemo wasanii, wanamuziki, watengeneza maudhui maarufu kama content creators, influencers, waandishi wa habari na wabunifu mbalimbali wa kazi za sanaa kwa kuwapatia mikopo. Hatua inayolenga kukuza uchumi na ubunifu kwa kutoa fursa zaidi za kiuchumi kwa vijana.
MHE. MUHSIN HAJI USSI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha wale vijana ambao wapo vijijini hawana smartphone na hawana uwezo wa ku-access mitandao ya kijamii, wanaweza kufikiwa kwa haraka kuweza kupata taarifa husika juu ya uwepo wa fursa hizi kwa vijana Tanzania? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO) K. n. y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Naibu Spika, hili nimelijibu pia, kwenye swali la kwanza la nyongeza la Mheshimiwa Juwakali. Kwa wale ambao hawataweza kupata access ya social media, tunaweza kutoa elimu kupitia makongamano na maadhimisho mbalimbali. Vilevile baadhi ya fursa zimekuwa zikibandikwa katika mbao mbalimbali za matangazo za watendaji kata na vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.