Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rebeca Sanga Nsemwa (1 total)

MHE. REBECA S. NSEMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuiwezesha timu ya Taifa ya Mpira wa Pete, kwani timu hii imekuwa ikifanya vibaya sana katika mashindano ya Kimataifa, lakini pia imekuwa ikienda kushiriki katika mashindano haya ikiwa haijakaa kambi, wala haina jezi zenye nembo ya bendera yetu ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rebeca kwa swali zuri. Serikali imekuwa ikiigharamia mara kwa mara Timu ya Mpira wa Pete, na kama anavyosema, hatujawahi kuwa na matokeo mazuri sana katika miaka ya karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunaendelea na juhudi mbalimbali za kuiwezesha timu hii, na kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha tunahakikisha ya kwamba timu hii inakaa kambi na kuwa na vifaa vya kutosha na inaweza kusafiri na kuweza kuhudhuria mashindano mbalimbali kwa ajili ya kuiwakilisha nchi yetu. Bado tunafanya juhudi nyingi kuhakikisha uwezo na ubora wa timu hiyo unaimarika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tutaendelea kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Pete ili kuhakikisha tunaimarisha timu hii.