Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Said Ibrahim Mzimba (2 total)

MHE. IBRAHIM S. MZIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa vituo hivi vinahudumiwa na ndugu zetu wa polisi ambao wanafanya kazi kubwa sana ya kulinda nchi yetu. Je, Mheshimiwa Waziri, yupo tayari kuambatana nami kwenda Jimbo la Mtambile kujionea hali halisi ya makazi ya polisi wetu hawa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Said Ibrahim; na ombi lake la kwenda Mtambile nimelipokea na nipo tayari kuambatana naye kwenda Mtambile.
MHE. SAID IBRAHIM MZIMBA: Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa makazi duni yanazorotesha utendaji kazi wa ndugu zetu Polisi, je, katika Kituo cha Polisi cha Kengeja, ni lini yatapatikana makazi ya Polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Said Ibrahim Mzimba kwa kazi kubwa anayoifanya. Mwaka wa fedha uliopita wa 2025/2026 alituuliza kuhusu kituo ambacho tumekikarabati sasa cha Mtambile na kimeshafanyiwa kazi pamoja na makazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka huu ninaona amekuja na hii ya Kengeja. Serikali inaendelea na utekelezaji wa mpango wa miaka mitano wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya makazi pamoja na vituo vya Polisi nchi nzima. Aidha, Serikali imepanga katika kila mkoa walau kuwa na majengo makubwa mawili ya ghorofa ikiwa ni sehemu ya kuimarisha makazi ya Askari.

Mheshimiwa Spika, hivyo, ninataka Mheshimiwa Mbunge na Askari wa eneo lake wote na Watanzania kwa ujumla wajue, Serikali inafanya kila liwezekanalo kuimarisha makazi na maeneo yao ya kazi ili kusudi waweze kufanya kazi kama wanavyofanya wengine katika ofisi zao katika mazingira mazuri zaidi. Ninaomba kuwasilisha.