Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Said Ibrahim Mzimba (2 total)

MHE. SAID I. MZIMBA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatenga Bajeti kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya Polisi Mtambile na Kengeja kwa kuwa vimechakaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Said Ibrahim Mzimba, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishafanya tathmini ili kubaini gharama halisi za ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi cha Kengeja baada ya kituo kinachotumika sasa kuwa kichakavu na kwamba hakiwezi kufanyiwa ukarabati. Kiasi cha fedha shilingi milioni 165 zinahitajika. Tathmini kwa ajili ya kubaini gharama halisi ya ukarabati wa Kituo cha Polisi Mtambile zimefanyika na kiasi cha fedha cha shilingi milioni 90 zinahitajika. Fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Polisi vya Kengeja na Mtambile zinatarajiwa kutengwa toka kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027.
MHE. SAID IBRAHIM MZIMBA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Makazi ya Askari Polisi katika Jimbo la Mtambile Wilaya ya Mkoani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Said Ibrahim Mzimba, Mbunge wa Mtambile kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa makazi bora ya Askari Polisi, ikiwa ni chachu ya kuboresha utendaji kazi wa kila siku wa ulinzi wa raia na mali zao. Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ulifanyika ukarabati mkubwa wa kituo cha Polisi na makazi ya Askari ambayo yapo ghorofa ya juu ya kituo cha Polisi katika Jimbo la Mtambile lililoko Wilaya ya Mkoani.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kutokuwepo kwa eneo la ujenzi wa jengo jipya la makazi katika eneo hilo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeingiza kwenye mpango wa ukarabati jengo la ghorofa ya makazi lililopo kituoni hapo kwa mwaka wa fedha 2027/2028. Ninaomba kuwasilisha.