MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa miongoni mwa vigezo ni kuandaa pamoja na maeneo ya kiutawala na vijiji hivi vya Songea, Mkamani, Kwaruma, Masimba na Sekioga vyote vina shule za msingi zaidi ya mbili na zahanati zaidi ya mbili. Kwa hiyo, kwa maana kwamba maeneo ya huduma yamekamilika. Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kutoa upendeleo maalum kwa maeneo hayo ili yaweze kupata huduma za kiutawala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Katika Wilaya ya Lushoto Kata ya Manolo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ina idadi ya watu 25,000 na ndiyo iliyoongoza katika Wilaya nzima, lakini ina sekondari tatu, vijiji sita na shule za msingi tisa. Serikali haioni kwamba ni wakati mwafaka kugawa kata hii ili tuweze kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa urahisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali inatambua kwamba kuna uhitaji wa kugawa baadhi ya vijiji ili kurahisisha huduma za kiutawala na huduma za kijamii lakini kwa vijiji hivi vya Songea, Mkamani, Kwaruma, Masimba na Sekioga katika Halmashauri ya Korogwe Vijijini, bado havijakidhi vigezo vya idadi ya watu kwa maana ya kwamba lazima kijiji ambacho kinazaliwa kiwe na idadi ya watu wasiopungua 5,000 na kile kijiji mama kiwe na watu wasiopungua 10,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sensa ya watu na makazi ya 2022 bado vijiji mama havijakidhi idadi ya watu 15,000 ili kuwezesha vijiji vingine hivi kuweza kugawika. Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijini kwamba Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu idadi ya watu na vigezo vingine ili ikiwezekana muda ukifika viweze kupata hadhi ya vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kuhusiana na Kata ya Manolo katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, tunafahamu kwamba ni kata kubwa ina watu wapatao 25,000 kwa taarifa za sensa na makazi 2022; na vijiji sita na shule za sekondari tatu, lakini bado haijafikisha idadi ya watu angalau 30,000 ili tukigawa kata ile, kata mama ipate angalau watu 20,000 na kata mpya ipate watu angalau 10,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kwamba tunatambua umuhimu wa kugawa kata hiyo, lakini namwomba tuendelee kufuatilia vigezo hivyo vya idadi ya watu na baadaye Serikali itaona utaratibu mzuri wa kugawa kata hiyo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikupongeze kwa jitihada hizi kubwa za kuifikisha Bajeti ya Barabara za Vijijini kufikia hizo shilingi bilioni 37 kwa Mkoa wa Tanga, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. Hii programu ya kupeleka lami hasa katika Miji Midogo imekuwa ikienda hasa kwa kusuasua na kujenga kilomita moja ama mbili. Je, Serikali ipo tayari kuongeza fedha ili angalau katika ile Miji Midogo lami iweze kujengwa angalau kwa kiwango cha kilometa tano mpaka 10?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Barabara nyingi ambazo zimefunguliwa vijijini, bado zinahitaji uboreshaji hasa kwa maeneo ya kalavati na pia kujengea sehemu ambazo ni za mifereji hasa katika Wilaya ya Lushoto ambayo maeneo mengi ni ya milima. Je, Serikali ipo tayari sasa kuongeza bajeti katika barabara hizo mpya zilizofunguliwa ili ziweze kupitika kwa mwaka mzima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Rashid Shangazi ambaye amekuwa akifuatilia na kuweka msukumo wa maendeleo katika Jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza ninaomba kumpata taarifa Mheshimiwa Rashid Shangazi kwamba, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali Awamu ya Sita, utaona dhamira ya dhati ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara zetu hizi za zinazohudumiwa na TARURA za ngazi ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya shilingi bilioni 100 zimetumika katika Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara hizi. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hata katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa maana ya mwaka wa bajeti unaofuata tayari fedha inatarajiwa kutumika bajeti imetengwa shilingi bilioni 37.1 kwa ajili ya kwenda kuimarisha miundombinu ya barabara hizi katika Mkoa wa Tanga, ikiwemo katika maeneo ya Miji Midogo ili lami ziweze kujengwa na barabara hizi ziweze kuwanufaisha wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na barabara hizi ambazo zimefunguliwa za vijijini ambazo zinauhitaji wa kalavati, mifereji ikiwemo katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge la Lushoto, ninaomba nimtaarifu kwamba katika bajeti hiyo ya shilingi bilioni 37.3 ya mwaka wa fedha ujao, tayari kuna mipango ambayo ipo ya kujenga kalavati 33, mifereji ya maji kilometa 1,020.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ataona dhamira ya dhati kabisa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha miundombinu hii muhimu kabisa ya barabara katika Mkoa wa Tanga na Jimbo lako hili la Lushoto, ndiyo maana utaona Mkoa wa Tanga ulikuwa una bajeti kila mwaka shilingi bilioni 12.4, lakini sasa tunazungumzia mwaka wa fedha 2025/2027, bajeti itakuwa ni shilingi bilioni 37.1. (Makofi)