MHE. NASSOR SAID NASSOR MAROO aliuliza:-
Je, Serikali kupitia Wizara ya Muungano na Mazingira inachukua hatua gani za kimkakati za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Nassor Said Nassor, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Hatua hizo ni pamoja na kuendelea kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao kwa kuzingatia kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uwezo wa nchi kustahimili ukame, mafuriko na mvua zisizokuwa na uhakika.
Mheshimiwa Spika, aidha, tunaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo jua, upepo, joto ardhi, gesi asilia na umeme ili kupunguza utegemezi wa matumizi ya kuni, mkaa na mafuta machafu.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Sera na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo Dira 2050 hususan nguzo ya tatu inayohusu mazingira na uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na mkakati wake wa utekelezaji unaoanzia 2021 – 2030, Mpango Kabambe wa Mazingira 2022 - 2032 na Mpango wa Taifa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi 2025 - 2035.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.