Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ritta Enespher Kabati (2 total)

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Serikali iliahidi kujenga vituo vya afya vya kimkakati, ili wananchi wasiendelee kufuata huduma katika umbali mrefu sana. Katika Wilaya yetu ya Kilolo kuna Kata za Kimara, Idete, Ukwega, Kwiugumu na Image, wananchi wanapata mateso sana kufuata huduma za afya na barabara hazipitiki. Mpaka sasa hivi madaraja hayapo…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, je ni lini sasa hivi vituo vya kimkakati vitajengwa, ili wananchi wasiendelee kupata mateso makubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilimetenga bajeti ya zaidi ya vituo 120 katika majimbo 120 vya kimkakati, zaidi ya shilingi bilioni 30. Tayari tumeomba fedha zingine, kwa ajili ya majimbo 94 pamoja na yale majimbo ambayo ni mapya, yote yataingia katika mpango huo na tutakwenda kujenga hivi vituo vya afya vya kimkakati. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, lini Serikali itapeleka pesa katika Kata ya Ibumu iliopo katika Wilaya ya Kilolo kwa sababu wanatembea umbali mrefu sana kufuata matibabu zaidi ya kilometa 40 na hata Kata ya Mlafu jirani yao pia hawana kituo cha afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali iliweka utaratibu wa kujenga vituo vya afya katika kata za kimkakati ambazo zinakidhi idadi ya watu wasiopungua 10,000 lakini zenye umbali mkubwa wa kutoka kwenye kituo cha jirani zaidi cha huduma za afya. kwa hiyo, ikiwa kituo hicho cha kata hiyo inayotajwa na Mheshimiwa Mbunge inakidhi vigezo hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutafanya mawasiliano na halmashauri ili tuanze kutenga fedha kwa awamu kwa ajili za ujenzi wa kituo hicho cha afya.