Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Fagason Aron Nkingwa (2 total)

MHE. FAGASON A. NKINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa sababu, Jimbo langu la Mbogwe lina kata 17, lakini ipo Kata ya Masumbwe yenye wakazi zaidi ya 100,000 na ni kata yenye wafanyabiashara wengi, je, ni lini sasa Serikali itakuja kujenga soko la kisasa kwenye Kata ya Masumbwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za masoko ni muhimu, hasa kwenye miji yenye wafanyabiashara wengi, ili kuwawezesha kufanya biashara vizuri na pia kuboresha huduma na mapato ya ndani ya Halmashauri. Kwa hiyo, ninatumia nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Fagason.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii pia, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbogwe, kupitia wataalamu wake na Baraza la Madiwani kukaa na kutathmini, kutafuta eneo na kuona uwezekano wa kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani kwa awamu, lakini pia kuleta taarifa rasmi na andiko la mapendekezo hayo Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ili kwa pamoja Serikali ione namna ya kuendelea kuboresha ujenzi wa masoko katika maeneo hayo.
MHE. FAGASON A. NKINGWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo. Jimbo langu la Mbogwe linazo kata 17, vijiji 87, vitongoji 335, lakini wananchi hawa hawana majisafi na salama. Je, ni lini Serikali italeta maji kwenye Jimbo langu la Mbogwe kutoka Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, labda niweke takwimu sahihi kwamba, siyo kwamba Jimbo la Mbogwe hakuna majisafi na salama. Tunafahamu kwamba mpaka sasa tuna zaidi ya 69% ya wananchi wa Mbogwe wanaopata huduma ya maji safi na salama. Nimtoe hofu, tunayo miradi inayoendelea ndani ya Jimbo la Mbogwe. Tutahakikisha kwamba tunaisimamia na tunapeleka fedha wakandarasi waweze kukamilisha miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, pia hatutamsahau katika maji kutoka Ziwa Victoria kwa sababu yeye yuko katika njia ambayo inaenda katika maeno ya Bukombe pamoja na Kahama. Hivyo, tunamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa wananchi wake wa Mbogwe watapata maji kutoka Ziwa Victoria bila ya kuwa na shida yoyote.