Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Faraji Buriani Nandala (2 total)

MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati. Nina maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya eananchi wa Jimbo la Ndanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka 2025/2026 ndiyo hii ambayo tunaitekeleza na tunaelekea kuikamilisha hivi karibuni. Hizi fedha shilingi bilioni tano zilishatengwa, ina maana zipo. Kwa hiyo, nataka majibu ya Serikali, ni lini hasa watawalipa hawa wananchi wakati tuko kwenye process za kupitisha bajeti mpya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ninataka kufapata ushauri wa Serikali, je, wale wananchi waendelee kuandaa mashamba yao au wasiendelee, kwa sababu hii gridi ya Taifa inapita kwenye mashamba ya wananchi? Kama wasiandae yale mashamba, je, Serikali itakuwa tayari kulipa penati itayotokana na kuchelewesha kulipwa kwa hii fidia yao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Faraji kwa kufuatilia maslahi ya wananchi wake wa Ndanda, amekuwa anatufuatilia mara kwa mara na kuja ofisini kwa ajili ya kujua hatima ya line hii ambayo itaingiza mikoa ya Lindi na Mtwara katika gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa, sisi Wizara ya Nishati pamoja na Wizara ya Fedha, tunajitahidi sana kuhakikisha kwamba fidia italipwa kwa wakati ili wananchi hawa wasiingie kwenye mgogoro mwingine kati yao na Serikali. Kwa hiyo, hilo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunajitahidi kutafuta fedha, na bado muda tunao, na hilo litatendeka ndani ya mwaka huu wa fedha, Mwenyezi Mungu akitujalia.
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.

Swali langu, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ndanda, nataka kufahamu ni lini Serikali itaona ipo haja ya kupunguza siku za maombi ya mikopo hii kutoka siku 90 zilizopo sasa hivi mpaka siku saba au 14, ili tuweze kuwafikia Watanzania wengi kwa muda mfupi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama alivyoliuliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi siku 90 zipo kwa utaratibu, kwa maana ya kwamba wapewe elimu ambayo Mheshimiwa Mbunge ametoka kuuliza ni kipindi cha kupewa elimu, lakini kufanya ufuatiliaji wa kuona kwamba vikundi ambavyo vimeomba ni kweli vina haki ya kupewa mikopo ile na vina uwezo wa kurejesha. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tunauchukua ushauri wake na tutaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)