Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Fadhili Sandali Chilombe (5 total)

MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwenye Jimbo la Tunduru Kusini, ninakotokea, kuna barabara kuu mbili ambazo ni muhimu sana kwa uchumi wa eneo lile. Barabara ya kwanza inaanzia Misechela – Namasakata – Tuwemacho mpaka Mjini; na ya pili inaanzia Mtina – Nasya – Tuwemacho mpaka Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye barabara hizi kila moja ina eneo korofi. Kwa mfano, hii inayoanzia Mtina – Nasya kuna eneo linaitwa Lamitado, pana kipande cha kilomita kama moja hivi ambayo mvua ikinyesha korosho hazipiti pale, magari yanalala pale hata siku tatu, siku nne. The same kwa upande wa Namasakata, kwenye Daraja linaloanzia Namasakata kwenda Chemchem, kuna kipande kina changamoto ambapo korosho ndiyo zinatoka nyingi, lakini huwa tunapata tabu kuzipitisha pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kupata Kauli ya Serikali, ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba, maeneo yale yanapata suluhisho la kudumu?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru Kusini, jana wakati anatoa hoja hapa alitoa elimu kubwa sana ya umeme kwa Mheshimiwa Ado Shaibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara hizi za Tunduru Kusini, maeneo yote korofi sisi tunayafahamu na tunakwenda kuyafanyia kazi. Tumefanya hivyo kwenye maeneo mengi ya nchi yetu kwa kutumia miradi mbalimbali, ukiwemo Mradi wa Agri Connect, pamoja na Mradi wa Rise. Vivyo hivyo, tutaangaza macho kwa ajili ya wananchi wa Tunduru Kusini. (Makofi)
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika siku za hivi karibuni pamekuwa na ongezeko kubwa sana la watumiaji wako wa simu kwenye baadhi ya maeneo ndani ya Jimbo la Tunduru Kusini, hali hiyo imesababisha baadhi ya minara kuzidiwa na ubora wa mawasiliano kutoka kwenye minara hiyo kupungua.

(a) Je, Serikali haioni haja ya kwenda kufanya review, kwa maana ya mapitio kwenye baadhi ya minara ili kuangalia uwezekano wa ama kuongeza masafa au kujenga minara mingine karibu na maeneo hayo?

(b) Je, kama inakubaliana na mimi, kazi hiyo itaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mhandisi Fadhili, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kufanya tathmini upya ni kweli baadhi ya minara kutokana na kuongezeka kwa watumiaji inakuwa inazidiwa. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kumwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA kutuma wataalam katika maeneo ya Jimbo la Tunduru Kusini ili wafanye tathmini na kubaini changamoto hiyo haraka iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tunduru, hususan Jimbo la Tunduru Kusini ina vijiji vingi ambavyo bado pamoja na jitihada za Serikali za kufungua, lakini hivyo vijiji havijawahi kupata hizo barabara. Mimi nafananisha barabara kama uwepo wa mishipa ya damu kwenye mwili wa binadamu kwamba ili tu-speed up maendeleo tunatakiwa pale sehemu ambapo tunaweza tukatengeneza ukaribu wa vijiji kuwasiliana ikafanywa hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa mfano, kipo Kijiji cha Semen na Kijiji cha Chiwana au kuna Kijiji kinaitwa Nalasi na Kijiji cha Mnemasi. Ukitoka Semen kwenda Chiwana ipo shortcut ya kilometa tano tu, lakini hivi tunavyoongea leo, ili kukifikia kijiji hicho unahitaji kutembea kilometa 17. Sasa swali je, Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha kwamba vile vijiji ambavyo vinakaribiana kwa mtindo huo vinafanyiwa sasa? Hilo swali langu la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ipo barabara inatokea Chiungo inapita Mkambara inaenda mpaka Mkasale. Barabara hii ilifunguliwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, kinachoombwa sasa ni ile barabara kusajiliwa ili iweze kupata huduma ya TARURA na ukitoka hapa Mkambara kwenda Mkasale ni kilometa zisizozidi nne katikati pale pana mto ambao huwa unajaa, sasa wananchi wa Mkambara wanategemea Hospitali ya Mkasale.

Je, Serikali itakamilisha lini jambo la kuisajili ile barabara kwa sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Fadhili, engineer huyu. Kwa bahati nzuri nilifika katika Jimbo lake na tulifanya mkutano mkubwa sana pale jimboni na wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini pamoja na Tunduru Kaskazini ni waungwana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, maswali yake mawili ya nyongeza. Hili la kilometa tano nawaelekeza TARURA kuanzia sasa wafike eneo hili kufanya tathmini katika shortcut hii na kuweza kuitengea bajeti ya kuanza utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kusajiliwa; tuna utaratibu wa kusajili barabara hizi katika Wakala wetu wa TARURA na pia nawaelekeza Meneja wa TARURA wa Mkoa pamoja na yule wa Wilaya waweze kuisajili barabara hii iweze kutoa huduma kwa watu katika Jimbo la Tunduru Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kituo cha Afya Mtina kinachohudumia kata mbili, hakina jengo la mama na mtoto, hali inayosababisha staha ya wakina mama kuondoka hasa wakati wanapojifungua. Tulishaanzisha ujenzi pale na jengo halijakamilika, nini mpango wa Serikali kukamilisha jengo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Eng. Fadhili, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini kwa kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa vituo hivi vya afya ambavyo tayari tulishaanza kujenga na tunatoa huduma zile za OPD, lakini tunajua miundombinu ambayo bado inatakiwa kukamilishwa, tunaendelea kutenga bajeti kukamilisha miundombinu hiyo.
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alivyofika Tunduru alitoa ahadi ya kujengwa Barabara ya Misechela - Tunduru. Barabara hii ni kati ya barabara ambazo zinatoa uzalishaji mkubwa sana wa korosho. Je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini amekuwa akifuatilia sana suala la ujenzi wa barabara hiyo na sisi tunafahamu kwamba hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi ahadi za viongozi wetu wa kitaifa ni kipaumbele nambari moja.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kutenga fedha kuhakikisha barabara hiyo inajengwa na dhamira ya Serikali na Mheshimiwa Rais kuwatumikia na kuwahudumia wananchi wa Tunduru inafikiwa.