MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga mnara wa mawasiliano katika Vijiji vya Kazamoyo, Imani na Kilimani katika Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Fadhili Sandali Chilombe, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka minne jumla ya minara 1,041 imejengwa na inatoa huduma za mawasiliano kwa wananchi. Kati ya minara hiyo, minara 758 imejengwa kupitia Mradi wa Tanzania Kidigitali ambao ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais, tarehe 13 Mei, 2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inaendelea na jitihada za kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote yaliyosalia ambapo tarehe 5 Desemba, 2025 mikataba ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata 201 ilisainiwa na utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2027.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, Serikali kupitia UCSAF imepanga kufikisha huduma hizo katika maeneo mengine 280, yakiwemo maeneo ya kimkakati kama vile reli ya kisasa, hifadhi za Taifa, barabara kuu na maeneo ya mipakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na taasisi zake na makampuni ya simu, inaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Miaka Mitano (2025 – 2030) wa ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu wenye lengo la kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Lukumbule ina minara minne ya mawasiliano iliyojengwa na Makampuni ya Simu ya VIETTEL (mnara mmoja) na TTCL (minara miwili) pamoja na mnara wa Helios Towers Tanzania ambao Vodacom, Airtel na Honora wanautumia kwa pamoja kwa kuweka vifaa vyao vya mawasiliano. Aidha, kutokana na changamoto ya mawasiliano katika Kata hiyo, Vijiji vya Kazamoyo na Imani vimejumuishwa katika mradi wa mawasiliano vijijini, awamu ya tisa unaotekelezwa na Wizara. Usanifu wa minara katika vijiji hivyo umekamilika na ujenzi unatarajiwa kuanza mapema Februari, 2026 na kukamilika mwishoni mwa Mei, 2026, ambapo wananchi wataanza kunufaika na huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Kilimani kitapata mawasiliano kupitia mnara wa Kazamoyo mara utakapokamilika. (Makofi)
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara za kuunganisha vijiji vilivyoanzishwa toka mwaka 1974 katika Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Fadhili Sandali Chilombe, Mbunge wa Tunduru Kusini, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha vijiji vyote 65 vilivyopo katika Wilaya ya Tunduru ili kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kufikisha huduma za kijamii. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeendelea kuhudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 1,203.61 katika Wilaya ya Tunduru ambapo maeneo ya Jimbo la Tunduru Kusini pia yamepewa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuunganisha vijiji ambavyo havijafikiwa tangu mwaka 1974, Serikali kwa kutumia fedha za maendeleo ya jimbo na nyongeza ya tozo ya mafuta imeendelea kufungua barabara za kuunganisha vijiji. Mpaka sasa imeshafungua barabara mpya zenye urefu wa kilometa 117.7 ambapo shilingi bilioni 1.25 zimetumika kufungua Barabara za Semen – Tupendane – Mchesi, Nalasi – Nasomba – Lukala, pia Barabara ya Chikomo – Mkandu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtandao wa barabara wa TARURA ni kilometa 144,149.18 ambapo Serikali inaendelea kupanua mtandao huu, ili kuwezesha kufikia maeneo mbalimbali, ikiwemo ya vijijini. Kadri Serikali inavyojenga uwezo wa kibajeti wa wakala itawezesha maeneo mengi nchini kufikiwa, vikiwepo vijiji vilivyoanzishwa toka mwaka 1974 katika Jimbo la Tunduru Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)