Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi ambazo ameendelea kuzifanya, Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamesema. Kila mtu anaona nini kinaendelea ndani ya hii nchi. Kwa hiyo, ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wengine kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anazoendelea kuzifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kujielekeza kwenye changamoto ya barabara. Tatizo la barabara ni kubwa na limesemwa, kila Mheshimiwa Mbunge anayesimama hapa ataongelea the same. Hata hivyo, ninaipongeza Serikali kwenye angle hiyo kwamba kabla sijaingia Bungeni nilikuwa ninasikia watu wanasema bwana Bajeti ya TARURA ni ndogo iongezwe na mwaka huu Serikali imefanya uamuzi wa kizalendo, imeongeza bajeti. Hii ni safari nzuri yenye mwelekeo mwema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja pongezi hizo, ninaomba kushauri mambo yafuatayo:- Kuna shida kubwa sana Serikalini, sijaingia Bungeni na hapa kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyasema hayo mambo. Moja kati ya shida kubwa ni kwamba Serikali inapanga bajeti, ikishapanga ile bajeti, fedha inayofika sasa kwenye utekelezaji wa hiyo bajeti ni ndogo. Sasa ukiangalia tatizo la TARURA lilivyo halafu ukaipelekea hela ndogo, shida kwa kweli zinaendelea kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaishauri Serikali, ninajua ina vipaumbele vingi, inatakiwa ifanye kazi nyingi kila kitu kinafanywa na Serikali, lakini moja kati ya vipaumbele vikubwa ambavyo Serikali inatakiwa kuvifanyia kazi, ni kupeleka fedha kwenye barabara za TARURA. Kwa kufanya hivyo ninaamini changamoto zitapungua kwa kiwango chake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, Serikali iongeze usimamizi wa kazi za TARURA. Ziko baadhi ya sehemu katika nchi hii, kazi zinazofanywa na TARURA siyo nzuri, haziko kwenye viwango. Kuna maeneo ukienda leo unakuta daraja limejengwa halina nondo kabisa. Matokeo yake ni nini? Yapo maeneo daraja moja limejengwa, in a span of less than 10 years limejengwa mara mbili. Sasa unaweza ukajiuliza kwamba fedha inayopelekwa ni ndogo, halafu tunajikuta tunaenda kujenga palepale kwa sababu kwenye eneo hilo hiyo barabara ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawajengi kwa kiwango, madhara yanayotokea ni nini? Ukiangalia maeneo mengi ya nchi, utakuta kwamba ziko barabara kila mwaka zenyewe ndiyo huwa zinapitiwa. Barabara zingine haziguswi, kwa sababu gani, kiwango cha fedha ni kidogo na pale wanapojenga hawajengi katika kiwango kinachotakiwa. Kwa hiyo ninaishauri Serikali iongeze usimamizi kwenye barabara za TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine, alisema juzi hapa Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali, Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, alisema hivi, “Mtandao wa barabara za TARURA nchi hii upo kilometa 144,429.77”. Ukienda kuangalia taarifa, hiyo maana yake ni kwamba ukubwa huo wa barabara ni sawasawa, hao watu wa TANROADS wana kilometa 37,435.04, hii ni 25% tu ya barabara ambazo TARURA wanazihudumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huu mtandao wa kilometa 144,000, ni kilometa 3,053 tu ndiyo zenye lami, hizo za TARURA, kilometa 3,053 pekee ndiyo zenye lami. Ukiangalia, kiwango hicho cha barabara ni zile ambazo ziko mijini, maana yake ni kwamba maeneo mengi ya vijiji hayana lami kabisa. Kwenye jimbo langu hakuna lami hata sentimita moja. Sasa hiyo naamini siyo Tunduru Kusini peke yake, maeneo mengi yapo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa, kumbe kuna Mifuko ilishaanzishwa kwa ajili ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kwenda kujenga hizo barabara. Ninaomba Serikali sasa ianzishe mkakati kwamba pamoja na hiki kilichofanyika sasa, kizuri, chema cha kuongeza bajeti, ninaomba hii iwe routine kila mwaka tuwe tunaongeza bajeti angalau kidogokidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu leo hii tunavyoongea kuna hizo kilometa nilizozitaja hapo, lakini mwakani tukifika hapa, barabara za TARURA zinazidi kuongezeka. Jimboni kwangu, juzi hapa niliuliza swali, ninahitaji kupasua barabara 20. Maana yake ukubwa huu ambao sasa hivi TARURA wana umiliki, mwakani siyo hivi na maeneo mengine yako hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wenyewe mashahidi, katika kila eneo la mtu anapotoka hapa, kuna vile vitu vinaitwa vitongoji, vimekuwa vinatakiwa vipandishwe hadhi viwe vijiji, barabara zitapasuliwa maana yake TARURA inazidi kuongezewa eneo lake. Kwa hiyo ninashauri kwamba Serikali itengeneze mkakati wa kuhakikisha kwamba huu uongezaji wa hela, kila mwaka ziongezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye hilo, zile barabara zinaongezeka, 60% ya watu nchi hii wanakaa vijijini na uzalishaji wote tunaoutegemea kwenye uendeshaji wa nchi kwa maana ya chakula na mambo mengine, unatokea vijijini. Ninaishauri Serikali pia ianze kutengeneza mkakati wa kuhakikisha kwamba kila mwaka, kila jimbo linapata angalau kilometa tano za lami. Tukianza safari hiyo tutafika, vinginevyo watajikuta wanatengeneza mijini tu, vijijini huku hakuguswi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili, ninatoka Tunduru, kwa ulinganifu Wilaya ya Tunduru ina square kilometer za mraba zile ziko 18,776, nikilinganisha na Mkoa wa Mtwara, una kilometa za mraba 16,707. Wilaya ya Tunduru ina halmashauri hii moja wakati tunawazidi Mkoa wa Mtwara kwa zaidi ya square kilometer 2,000. Mtwara wana halmashauri tisa, nimeweka hiyo kama ulinganifu. Vilevile, Mkoa wa Ruvuma ninaotokea mimi una halmashauri nane, kuna watu 1,981,884 katika mkoa huo, kati ya hao wananchi 400,000 wa Mkoa wa Ruvuma wanatokea Tunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? watu 1,500,000 plus wanatokea kwenye zile halmashauri saba ambazo ukigawa unapata wastani wa watu 224,000. Ninalenga kusema nini? Ninaiomba Serikali, tumeshaleta hili ombi mara nyingi ile halmashauri igawanywe ni kubwa mno. Hapa panakuwa hapana ulinganifu, kwenye mkoa tu wenyewe, sisi tupo watu 400,000, halmashauri nyingine zina watu 200,000 plus, eneo ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja ku-wind up, wananchi kule wanataka kusikia nini kauli ya Serikali kwenye kipande hiki? Ninaomba sana Serikali kwenye angle hiyo watusaidie, Tunduru, hili Bunge lisiishe lazima tuwe na halmashauri nyingine kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wakati ninaelekea kumaliza mchango wangu, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Watu wamempongeza na mimi ninasema tu, wakati ule anateuliwa hapa, Hayati Lukuvi alipewa nafasi ya kusema, alisema kumhusu Mheshimiwa Waziri Mkuu. Yaliongelewa maneno, nikawa nahisi kwamba mbona kama kuna chumvi inaongezwa, lakini baada ya kuwa ameanza kazi, ninaona zile sifa zilikuwa chache, anastahili zaidi. Anafanya kazi na kwa kweli anatupeleka kwenye dira iliyo njema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwake, aende na atengeneze mechanism ya kufuatilia kwa sababu sasa anapotoka huku nyuma mambo yanakuwa business as usual.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu nyingine, ninaomba kumpongeza Mkuu wangu wa Mkoa, Mheshimiwa Brigedia Mohamed Abbas pamoja na Katibu Tawala wake anaitwa Mama Mary Makondo. Mkoa wa Ruvuma ni mkubwa, lakini mkoa ule umetulia sana, ametoka kusema mtu mmoja hapa “Ukiona vinaelea, vimeundwa”. Ukimya ule siyo wa hivi hivi, yako mambo yanatokea kule, lakini wale watu wanayamaliza, lazima tuwape sifa zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Mkuu wa Wilaya ya Tunduru. Wilaya ni kubwa nimetoka kusema hapa, lakini imetulia ni kwa sababu wao wanafanya kazi. Kipekee, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, anapambana mno. Kuna watu wana halmashauri ndogo, lakini kwenye utendaji Halmashauri ya Tunduru ni kati ya zile ambazo zinafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupongeza wewe, ninampongeza Mheshimiwa Spika kwa sababu moja tu, hapa ndani sisi ni wageni lakini mnatupa nafasi tunaongea. Ninawashukuru na ninawapongeza kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. Ahsanteni kwa kunisikiliza.