Supplementary Questions from Hon. Ibrahim Mohamed Shayo (3 total)
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, Moshi ni Mji ambao ulikuwa na viwanda vingi sana, lakini viwanda vile sasa hivi vimekufa na vimechukuliwa na wawekezaji na wale wawekezaji hawawekezi wamevichukua tu kama magofu. Ni lini Serikali itaweza kuwanyang’anya viwanda vile na kuvifanyia kazi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilivitoa viwanda hivi kwa wawekezaji kwa nia ya uzalishaji. Mkataba wa makabidhiano wa viwanda hivi kwa hao wawekezaji unawataka wauheshimu kwa maana ya kuendelea na shughuli za uzalishaji. Ndiyo maana kwa Moshi kuna Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools ambacho mimi mwenyewe nilikuwa pale wiki mbili zilizopita kazi za uzalishaji inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maeneo mengine ambayo wawekezaji wamepewa viwanda hivi na havizalishi, rai yetu ni moja tu kuwaambia kwamba, aidha warudi kwenye uzalishaji ama Serikali itachukua hatua ya kuwapatia viwanda hivyo wawekezaji ambao wana nia ya dhati ya kushiriki katika ujenzi wa Dira ya 2050 kwenye Uchumi wa Viwanda na Uzalishaji kwa ajili ya shughuli ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yetu.
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ninaomba niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Barabara ya Maili Sita – Kiboriloni ujenzi wa njia nne utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kuianza hiyo barabara, kwa sababu ni barabara ambayo inaanzia Tengeru inakwenda Kikafu – Maili Moja – Kiboriloni kwa njia nne. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko kwenye hatua za mwisho kabisa ili barabara hiyo ianze kujengwa. (Makofi)
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri nikushukuru sana, ulipokuja Moshi uliwaahidi wananchi wenzangu wa Moshi kwamba Serikali itakwenda kujenga mortuary ya kisasa. Je, ni lini mortuary ile inakwenda kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ibrahim, Mbunge wa Moshi kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwapigania wananchi wa Moshi. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekwishakupeleka shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa mortuary pale Moshi na mkandarasi ameripoti site wiki iliyopita na tumesema kwa kazi nzuri aliyofanya Mheshimiwa Mbunge pindi ujenzi utakapoanza atakwenda yeye mwenyewe kuweka jiwe la msingi katika mortuary ile ya Hospitali ya Mawenzi.