Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jacqueline Ngonyani Msongozi (2 total)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninaomba nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kuanza kujenga daraja lile ambalo lilikuwa linaleta athari kubwa kwa wananchi wa maeneo yale.

(a) Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba daraja hili linakamilika kwa wakati?

(b) Je, Naibu Waziri yupo tayari kuongozana nami kwenda katika eneo la ujenzi wa daraja hilo pale Mitomoni ili aweze kupokea zawadi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais kwa sababu wananchi wamefurahi sana kuanzishwa kwa ujenzi wa Daraja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan nipokee pongezi za Mheshimiwa Mbunge, ninaamini hizi ni pongezi pia za Wanaruvuma wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuhusu swali lake la (a), kwamba mikataba tuliyosaini na tulivyokubaliana na wenzetu wa World Bank, miradi yote hii inatakiwa ikamilishwe ndani ya mwaka mmoja na hatutegemei kuwa na changamoto yoyote ya mtiririko wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulishakubaliana na wakandarasi, tunawasimamia tutahakikisha kwamba wanakamilisha hizo kazi kama tulivyokubaliana kwenye mkataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kupokea zawadi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakubaliana tarehe sahihi na tutakuwa tayari kwenda kupokea zawadi ya Wanaruvuma kwa ajili ya Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kujenga hili daraja muhimu sana, ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana katika kuchagiza uchumi katika Manispaa ya Songea. Wanawake wamekuwa wakipata adha kubwa kupeleka bidhaa zao masokoni.

(a) Je, Serikali ni lini itaanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami?

(b) Serikali imeeleza hapo kwamba inatakiwa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kilometa tano. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha na vifaa vya ujenzi, graders, caterpillars ili ujenzi huu uanze mara moja kwa ajili ya kuchagiza uchumi katika Manispaa ya Songea? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa barabara zetu hizi za Wilaya, barabara zinazosimamiwa na TARURA hasa kwa maana barabara hizi zinachangia sana katika shughuli za uchumi na kuwawezesha wananchi kufika katika huduma za msingi kabisa za kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona katika Wilaya ya Songea, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, zaidi ya shilingi bilioni 20 zimetumika katika kuimarisha miundombinu ya barabara hizi za Wilaya. Katika mwaka wa fedha 2025/2026, shilingi bilioni 7.65 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kumjibu Mheshimiwa Jacqueline Msongozi kwamba lini ujenzi wa barabara hii utaanza, kama nilivyotangulia kusema, tayari usanifu umefanyika katika barabara hii ya Mshangano – Legele, na imebainika kwamba shilingi bilioni 2.5 zinahitajika kwa ajili ya kuijenga barabara hii kwa kilometa tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa, fedha itakapopatikana, ujenzi utaanza, ataona wakandarasi wako site, ataona hiyo mitambo anayotaka kuiona, ataiona ipo site, kwa ajili ya kuanza kujenga barabara hii, kwa sababu kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, barabara hii ina umuhimu mkubwa sana kiuchumi, lakini inawasidia wananchi kufikia huduma za msingi za kijamii.