Primary Questions from Hon. Jacqueline Ngonyani Msongozi (4 total)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Daraja la Mtomoni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa daraja la Mitomoni unatekelezwa kupitia fedha za dharura zilizotolewa na Benki ya Dunia kupitia dirisha la Contingent Emergency Response Component (CERC) kwa gharama ya shilingi bilioni 9.29. Mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 1 Novemba, 2024. Hadi sasa utekelezaji wa mradi huu umefikia 21% na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2025.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mshangano – Legele hadi Mletele?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa barabara ya Mshangano - Legele hadi Mletele, na tayari imefanya usanifu wa ujenzi kwa kiwango cha lami ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2.513 kinahitajika ili kujenga kilometa tano, na kwa sasa inaendelea kutafuta fedha za kutekeleza mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imekuwa ikiendelea kuifanyia matengenezo barabara hii, ambapo katika mwaka 2022/2023 yalifanyika matengenezo ya kuifungua barabara, kung’oa miti, ujenzi wa mitaro, ujenzi wa makalavati na uwekwaji wa changarawe kwa gharama ya shilingi milioni 42.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2023/2024 na 2024/2025 Serikali ilifanya matengenezo ya kawaida katika barabara hiyo ikiwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha tuta la barabara kwa kuichonga na kuchimba mitaro ya kutolea maji ya mvua kwa gharama ya shilingi milioni 84.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2025/2026 Serikali imeweka katika mipango yake matengenezo ya kawaida kwa shilingi milioni 47.5. Serikali itaendelea kuihudumia miundombinu ya barabara na madaraja ya Mji wa Songea kwa kuijenga, kuikarabati na kuifanyia matengenezo kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JACQUELINE K. NGONYANI aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Mshangano - Legele hadi Mletele yenye kilometa 9.2?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Profesa Shemdoe, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa Barabara ya Mshangano - Legele hadi Mletele, kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami ambapo, shilingi bilioni 2.51 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa awali wa kilometa 5.0 za barabara hiyo. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuweza kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Spika, aidha, wakati tunasubiri upatikanaji wa fedha katika mwaka wa fedha 2025/2026, barabara hiyo imetengewa shilingi milioni 20, kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo ya kawaida. Vilevile, kwenye mwaka wa fedha ujao wa 2026/2027, Serikali imepanga kutenga shilingi milioni 250, kwa ajili matengenezo ya barabara hiyo ili kuhakikisha inapitika muda wote.
MHE. HAPPINESS D. NGWANDO K.n.y. MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -
Je, lini ujenzi wa Soko la Mfaranyaki katika Manispaa ya Songea utaanza kwa kuwa hali iliyopo ni hatarishi kwa usalama wa watumiaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani, Mbunge wa Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Soko la Mfaranyaki ni soko la muda lililotengwa pamoja na maeneo ya Mji Mwema na Bombambili, kwa ajili ya kuhifadhi wafanyabiashara waliopisha ujenzi wa Masoko ya Manzese A na B katika Manispaa ya Songea.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa masoko ya kudumu ya Manzese A na B unaendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 23.5 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba, 2026. Masoko hayo yakikamilika yatatumika kwa wafanyabiashara walioondolewa kupisha ujenzi na wafanyabiashara wengine.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mfaranyaki ni eneo la muda na halina miundombinu stahiki, wafanyabiashara wanakabiliwa na changamoto za kutokuwepo kwa jengo la wafanyabiashara, hivyo kusababisha kutiririka kwa maji, usalama mdogo, na kushindwa kudumisha ubora wa bidhaa zinazouzwa katika soko hilo.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Songea imetenga shilingi milioni 80 katika bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa ajili ya ujenzi wa paa katika soko la Mfaranyaki wakati tukisubiri kukamilika kwa ujenzi wa masoko ya kudumu ya Manzese A na B.