Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Janeth Peter Pinda (2 total)

MHE. JANETH P. PINDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa katika barabara hii ina vipande na Wakandarasi wa kutoka Vikonge – Luhafwe, lakini kutoka Luhafwe – Mishamo, wakandarasi hawapo site. Je, ni lini Serikali itatoa pesa kwa ajili ya ukamilishaji wa kipande hiki cha barabara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Barabara hii kutoka Katavi – Uvinza na Serikali imeweka utaratibu au mpango wa kuunganisha barabara. Je, ni lini Serikali itakamilisha barabara hii ili kuondokana na adha ya usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi pamoja na Kigoma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kipande hiki cha Luhafwe – Mishamo ambacho kinajengwa na CHICO kulikuwa na changamoto kidogo, lakini tumeshaitatua na Mkandarasi anarudi site kuendelea na kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la barabara ya kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma pamoja na Mkoa wa Rukwa. Kutoka Kibaoni – Stalike, Mkandarasi alikuwa anasuasua tayari ameshalipwa malipo yake na yuko site anaendelea ili kuunga Kibaoni – Mlele – Stalike. Nimpe Mheshimiwa Mbunge habari njema kabisa kwamba, tunaenda kuunga Katavi na Kigoma kuanzia Mishamo – Uvinza, kandarasi itatangazwa muda siyo mrefu kukamilisha hizo kilomita zote 95. Muda siyo mrefu tunakwenda kutangaza hiyo tenda kila kitu kipo tayari. Kwa hiyo tutakuwa tumeunganisha kutoka Kibaoni – Uvinza – Mishamo – Mpanda hiyo ndiyo kazi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuiunganisha mikoa. Ahsante.
MHE. JANETH P. PINDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya nyongeza. Wanawake wengi wamekuwa wakiomba mikopo, lakini hawana elimu ya kutosha. Je, ni lini Serikali itatoa elimu kwa akinamama hawa ili waweze kupata elimu hiyo ya mikopo? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vipaumbele vya utoaji wa mikopo ya 10% kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ni kutoa elimu na hamasa kwa makundi husika. Serikali imeweka kamati katika ngazi za kata, wilaya na mkoa, lakini wapo Maafisa Maendeleo ya Jamii katika halmashauri zetu na kwa baadhi ya halmashauri mpaka kwenye ngazi ya kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, bado kuna changamoto ya elimu na hamasa ya kutosha kwa makundi haya ambayo yanalengwa kwa ajili ya kupata mikopo ya 10%. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kuwasimamia watendaji wote katika ngazi za Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuendelea kutoa elimu kwa akinamama, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kupata mikopo hii kwa kadiri inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, trend ya mikopo hii inatia matumaini makubwa kwa sababu, tangu tuliporejesha utaratibu wa Julai, 2024, Serikali imekusanya jumla ya shilingi bilioni 253 kwa ajili ya kukopesha. Mpaka Disemba, 2025 tayari makundi haya yameshakopa shilingi bilioni 230.66 sawa na 91% ya malengo ya kukopesha kwa muda huo, lakini marejesho pia yameendelea kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki marejesho yaliyofanyika ndani ya muda ni shilingi bilioni 100.27 sawa na 82% ya malengo. Kwa hiyo, pamoja na changamoto za mikopo ya 10%, kuna matumaini na mtiririko au trend inayoonesha improvement kubwa. Serikali itaendelea kusimamia kuhakikisha mikopo hii inawafikia walengwa, lakini pia, urejeshaji unakuwa na ufanisi mkubwa zaidi.