Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Janeth Peter Pinda (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. JANETH P. PINDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia kwa siku hii ya leo, lakini kabla sijaendelea ninaomba sana nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenipa afya njema mpaka siku hii ya leo nami kuweza kuchangia katika Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii pia kumshukuru sana Mama yangu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo amekuwa akisimamia shughuli za maendeleo na kutufanya sisi wananchi tuishi katika amani, lakini tukikua kiuchumi siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo anamsaidia Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutekeleza shughuli za Serikali. Nimemfahamu vizuri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba alivyokuja kwenye ziara kule Katavi. Amekuwa akifanya kazi nzuri sana na kutatua changamoto za wananchi mbalimbali (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue nafasi hii pia, kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa kuniamini, lakini pia Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunipa ridhaa ya kuwa Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Katavi na kuweza kuwawakilisha wananchi wa Mkoa wa Katavi katika Bunge hili. Ninawaahidi kwamba nitashirikiana na Wabunge wenzangu kuhakikisha changamoto zote tunazifikisha kwa Serikali ili waweze kuzitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza sana mama yangu Mwanamvua Mrindoko, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, kwa namna ambavyo akisimamia shughuli za maendeleo na uchumi za Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja sasa katika kuchangia hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkoa wetu wa Katavi ni mkoa wa kimkakati, ni mkoa unaokua kiuchumi siku hadi siku, lakini Mkoa ule wa Katavi hauna barabara za kuunganisha mikoa, zaidi ya barabara ile ya Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa namna ambavyo imetoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa kiasi cha kilometa. Niwaombe sana wale wanaozisimamia, mamlaka hizo waweze kuharakisha mipango hii ya ujenzi wa barabara ili iweze kukamilika kwa wakati ili wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kunufaika kwa barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali pia, kwa zile barabara za ndani, ninaendelea kusisitiza kwamba Mkoa wa Katavi bado hatuna barabara, niiombe Serikali ituongezee pesa kwa ajili ya zile barabara za TARURA ili wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kunufaika na kuweza kujiendeleza zaidi kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye suala zima la afya. Tunaishukuru sana Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikiboresha hasa miundombinu ya afya. Tumepata Hospitali kubwa sana ya Mkoa ambayo inahudumia wananchi wa Mkoa wa Katavi, lakini haina uzio, pia na hospitali zetu za wilaya. Ninapenda kuitetea Hospitali ya Wilaya ya Mlele, tumepata hospitali nzuri, lakini haina uzio, ninaomba mamlaka zinazohusika ziweze kutusaidia ili hospitali ile iweze kupata uzio. Kituo cha Afya cha Usevya nacho hakina uzio, ninaiomba Serikali kuweza kukipatia uzio kituo hicho cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda moja kwa moja katika Kituo cha Afya Chamalendi, tunaishukuru Serikali imeweza kutoa pesa za ujenzi, lakini ujenzi wake unaenda taratibu sana kiasi ambacho wananchi wa Chamalendi wanapata changamoto kubwa katika suala zima la matibabu, hasa pale wanapohitaji masuala ya upasuaji, na kadhalika. Ninaomba wale ambao wanaendelea kusimamia eneo hilo la ujenzi waweze kuharakisha ujenzi huo, ili wananchi wa Chamalendi waweze kupata huduma hizo za afya kwa uharaka na zenye uhakika. Ninaomba pia, katika Kituo cha Afya cha Kibaoni, tunashukuru tumepata Kituo cha Afya kule Kibaoni, Mpimbwi, lakini hakina huduma za mionzi, kama x-ray na ultrasound.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoka kuzungumzia suala la shida za barabara. Wananchi tunaozunguka maeneo yale kikiwemo Kituo hicho cha Chamalendi tunapata shida kuitafuta au kuifikia hospitali ya Wilaya, kwa ajili ya kupata huduma za mionzi. Ninaomba zile mamlaka zinazohusika basi ziweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda moja kwa moja katika suala la uwekezaji, kama nilivyozungumza kwamba, Mkoa wa Katavi ni wa kimkakati, unakua kiuchumi siku hadi siku. Mkoa wetu wa Katavi una madini na wananchi wengi kutoka sehemu mbalimbali, wageni kutoka nchi mbalimbali wanafika Mkoa wa Katavi; basi ninaiomba Serikali kuweka vizuri Sheria ya Utoaji wa Leseni za Uchimbaji. Zitolewe baada ya kujiridhisha kuwa, hao waliopo katika ardhi hiyo ndiyo hasa wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itapunguza migogoro pamoja na malalamiko, hasa migogoro ya ardhi, katika eneo hilohilo la uchimbaji wa madini. Ninaomba sana wale wachimbaji wadogowadogo basi waweze kutambulika, lakini pia, ikiwezekana na wenyewe waweze kupewa elimu zinazohusiana na shughuli nzima za uchimbaji wa madini, hii itasaidia kuondoa migogoro na malalamiko. Ninachukua nafasi hii sasa kuiomba Serikali kusimamia eneo hilo la uchimbaji wa madini, wale waliopewa leseni za uchimbaji wa madini kuangalia wasiende kuchimba karibu na vyanzo vya maji au mito. Hii itasaidia kuepusha uharibifu wa miundombinu, lakini hasa madhara ya viumbe hai wakiwepo binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mambo mengi, ninaomba tu niyawasilishe hayo kwa leo. Hivyo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)