Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Lucy Simirya Kombani (2 total)

MHE. LUCY D. S. KOMBANI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa hii migogoro imekuwa ya muda mrefu sana na inaleta madhara makubwa sana kwenye hizi jamii zetu na kwa upande mwingine tukiangalia tuna wataalam ambao wamesomea utatuzi wa migogoro; je, Serikali haioni haja sasa ya kuwatumia wataalam hawa katika kumaliza haya matatizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025 hakujaripotiwa migogoro yenye kuleta mapigano katika maeneo mengi nchini. Serikali inamuahidi Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kuwatumia wataalam hawa ili kuweka hali hii ya usalama wa wakulima na wafugaji. Tunaendelea kuhamasisha zile kampeni (kwa mfano, Kampeni ya Tutunzane) ili kuona kabisa wakulima na wafugaji wanavyohitajiana na waweze kuishi katika maeneo kwa usalama na uzalishaji mali uendelee.
MHE. LUCY S. KOMBANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Swali langu la kwanza la nyongeza, je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya skimu za Lupiro, Euga na Minepa ambapo Skimu hii ya Lupiro tu ikikamilika ina uwezo wa kuhudumia ekari 40,000, na hii ya Euga ikikamilika ina uwezo wa kuhudumia ekari 32,000 ambayo ni sawasawa na wakulima 82,000 watanufaika kwenye skimu hizi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Wilaya ya Mvomero hususan kwenye Tarafa ya Mgeta ni wakulima na wasambazaji wazuri sana wa mbogamboga pamoja na matunda, lakini wakulima hawa wamekuwa wakitumia njia za kienyeji kama kutumia mianzi ili kupitisha maji kwenye mabomba yao. Je, Serikali haioni haja ya kuwaboreshea miundombinu hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninampongeza Mheshimiwa Lucy Kombani, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro kwa maswali yake mawili ya nyongeza ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja ni kwamba kuhusu Skimu ya Lupiro na Luhuga kwamba lini tutapeleka fedha, nimwambie tu kwamba skimu hizi ziko katika mpango wa fedha wa mwaka unaokuja kuhakikisha kwamba zinaendelea kutekelezwa. Kwa hiyo, tuko katika hatua za mwisho za kuhakikisha kwamba fedha inashuka katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Tarafa ya Mgeta katika Jimbo la Mvomero, amesema wananchi wanatumia mianzi kama sehemu ya mabomba kupeleka maji na ameiomba Serikali kuhakikisha tunaboresha mradi huo. Nimthibitishie tu kwamba mradi huo tayari tumeshatuma wataalamu wanaofanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kwenda kuboresha ule mradi ili wananchi wale sasa wapatiwe miundombinu bora na ya kisasa.