Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii. Ninaomba niitumie fursa hii pia, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kufika katika hatua hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza ninashukuru sana kwa michango mingi sana iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Kwa hakika tumepokea michango ya mazungumzo 95 na vilevile michango ya maandishi rasmi takribani mitano, iliyokwenda kwenye mfumo na bado kuna michango ya maandishi zaidi ya 10 kwa hivyo, unaweza ukaona namna ambavyo hoja yetu imepata wachangiaji wengi zaidi. Ninawashukuru sana kwa unyenyekevu mkubwa Waheshimiwa Wabunge na hilo ni deni la utumishi kwangu mimi na timu yangu. Ahsanteni sana.

Mheshimiwa Spika, katika jambo ambalo Wabunge wote wamelichangia humu kwa hakika ni juu ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ni rekodi ya namna ya kipekee, ambayo ndani ya uongozi wake wa miaka mitano amekamilisha Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, malengo na dira iliyowekwa na Serikali; Rais Samia amei-champion na ameonesha ya kuwa, yeye yupo tayari katika kuhakikisha anaipeleka nchi yetu mahali pazuri na pakubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuonesha ushahidi wa jambo hili katika miaka hii minne, mitano, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na yote aliyoyafanya kwenye madaraja, pamoja na kilometa zaidi ya 1,400 za lami zilizojengwa nchi nzima, lakini utaona kwamba, tayari amesaini mikataba takribani 80 yenye thamani ya takribani shilingi 6,000,000,000,000, ambayo ipo kwenye pipeline. Hii ni commitment ya hali ya juu kabisa, ambayo ameonesha ni nini anakusudia na ni wapi anataka kulifikisha Taifa letu. Ndiyo maana nimekubaliana na hoja ya Kamati na ninakubaliana na hoja za Wabunge wote ya kwamba, tujikite katika kuhakikisha viporo vyote na miradi yote iliyosainiwa ni muhimu na ni lazima tuendelee nayo kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wachangiaji wengi wamezungumzia juu ya barabara kuu na ubovu wa barabara hizi. Ninawashukuru wote kwa ujumla, wapo waliosisitiza sana, hususan barabara kama vile ya Kusini. Ninawatoa hofu Waheshimiwa Wabunge na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wa kule Kusini, wakiongozwa na mtoa hoja namba mbili, kaka yangu, Mheshimiwa Nape, wala yeye asishike shilingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, ukweli ni kwamba, katika bajeti yetu ukisoma kitabu cha randama imeeleza wazi ukurasa namba 200, ukurasa namba 213, ukurasa namba 214, tumeeleza tutakavyokwenda kujenga vile vipande kutoka Mkuranga mpaka Kongowe, kutoka Ikwiriri mpaka Nyamwage mpaka Somanga, kutoka Somanga mpaka Nangurukuru na kutoka Nangurukuru mpaka Mbwemkuru, imeelezwa wazi katika bajeti ile. Vilevile, nimeshukuru kwamba, Waheshimiwa Wabunge wa eneo hili wameeleza kwa kina sana juu ya madaraja makubwa na mazuri yaliyojengwa katika maeneo yale.
Mheshimiwa Spika, ikaelezwa juu ya ile Barabara ya Mzunguko kutoka Mnazi Mmoja – Mingoyo mpaka Masasi. Masasi – Newala – Tandahimba mpaka Mtwara Vijijini na kurudi tena hapa Masasi. Pale Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka jumla ya fedha zaidi ya shilingi 600,000,000,000 zipo eneo lile peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, habari iliyo njema zaidi ni vijiji 30 vya kutoka pale Mnazi Mmoja kwenda Masasi, ambavyo takribani kilometa 70 zinapita katika Jimbo la Mtama peke yake, vyote vitawekewa taa. Eneo lile lina taa zaidi ya 3,000 kwa hivyo, ninaomba kwa heshima kubwa na taadhima hakutakuwa na sababu. Ninaomba kabisa ya kwamba, hii shilingi isishikwe kwa sababu, ikishikwa inaweza kusababisha pia, vilevile mradi ule usiendelee kule kwa hivyo, kwa heshima kubwa na tahadhima isishikwe hii shilingi, ili tuendelee kujenga nchi yetu katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba pia, nieleze juu ya shukrani nyingi zimesemwa hapa kwa Mheshimiwa Rais. Mama yangu Mheshimiwa Salma Kikwete, Mheshimiwa Chikota, Mheshimiwa Zainab Kawawa, Mheshimiwa Nawanda, Mheshimiwa Katani na Mheshimiwa Mapalilo; wote wa barabara hiyo, wote wamezungumza vizuri na kumsifu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya.

Mheshimiwa Spika, hiyo pia, inaenda sambamba na zile barabara kuu nyingine. Kwa mfano Barabara ya kutoka Singida – Babati, dada yangu Mheshimiwa Asia Halamga ameizungumza vizuri na Mbunge wa Babati Mjini. Ninataka niseme, hii ni katika zile tulizoziweka kwenye mkakati wetu kwamba, tunakwenda kushughulika nazo, tena ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, haturudi nyuma tunakwenda mbele. Hatuzungumzi juu ya single carriage, barabara moja ambayo magari yanapishana namna hii, barabara ni mbili, ilani imeelekeza, ni dual carriage na tunakwenda kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge pale waliposisitiza juu ya fedha za Mfuko wa Barabara. Mimi ninawasisitiza na kuwaomba sana kwamba, sisi katika Serikali tumejipanga vyema kutumia fedha hizo na tutakuwa na ile Hati Fungani, ambayo ninawahakikishia Wabunge wasiwasi wao na maoni yao, Serikali kwa upande wa Wizara ya Ujenzi na mwenzangu wa Wizara ya Fedha, tumeyachukua. Hatutafanya mchezo na fedha hizi hata kidogo na kwamba, labda hizi fedha zitatumika vibaya pindi mambo yatakapokuwa yameiva, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawapa commitment, ikiwa jambo hili limefanikiwa, litakwenda kufanya vizuri. Tunataka tufike mahali barabara hizi, ambazo ni za kiuchumi na zimechangiwa na Wabunge wengi humu, zitufikishe mahali zijengwe katika utaratibu ulio mzuri, ulio bora na tutoke kwenye kuzizungumza tena baada ya miaka michache ijayo. Tunataka miaka michache ijayo tuwe na mazungumzo haya ya akina baba Levo, ya kuwaombea watu wa Kigoma flyovers.

Mheshimiwa Spika, ninataka tufike mahali tusizungumze tena kukarabati. Tufike mahali kwamba, Mheshimiwa Musukuma akija humu Bungeni asizungumze mambo ya Barabara ya Nkome – Nzala, aje kuwaombea watu wa Geita flyovers, ndiyo tunataka tufike huko. Kwa hivyo, ninawaomba kwa heshima kubwa na taadhima watuamini na watuunge mkono. Ninawaomba kwa heshima kubwa na taadhima wasishike shilingi, tumejipanga, tunakwenda kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kwa sababu, hoja ni nyingi sana, watu 100 kusema mmoja baada ya mwingine, ni lazima nikubali, na kwa ufinyu wa muda Wabunge waridhike kwamba, Serikali imejipanga vyema. Nimefurahi kwamba, katika mazungumzo makubwa na mazuri yaliyotokea hapa nimekaribishwa sehemu nyingi mara baada ya kusema kuwa, tutakapofunga Bunge na kwa kuwa, hela zimekwenda, Wabunge wamenikaribisha tupite majimboni.

Mheshimiwa Spika, mmoja katika Wabunge, aliyetia fora, amenialika niende jimboni, ni mtani wangu yule Mbunge wa Kahama, Mheshimiwa Benjamin Lukubha. Yeye kanipa na ofa, anasema uje Kahama, sisi tunataka uje kuiona Barabara ya Kakola na barabara nyingine, lakini tutakupa na jiko uongeze. Sasa ukipewa jiko na Wasukuma unakataa vipi?

Mheshimiwa Spika, hilo nimeliunga mkono, ninakuja huko na tutakwenda katika maeneo mengine pia. Tutahakikisha kwamba, tunakwenda kufanya kazi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa na taahadhima ninaomba Waheshimiwa Wabunge watuamini, watutume kazi. Tumejipanga, tunakwenda kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema haya, ninaomba kutoa hoja na ninaomba watuunge mkono kwa heshima kubwa na taadhima. Ahsante sana. (Makofi)