Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaanza kwanza kwa kutoa shukrani zangu nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii ya Unaibu Waziri wa Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninatoa pia pongezi na shukurani nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana, ambayo ameifanya katika Nchi ya Tanzania, hasa sekta ya miundombinu. Tukumbuke tu kwamba, ametambuliwa kuwa, ni kati ya Marais bora katika Afrika ambao wamefanya kazi kubwa sana kwenye sekta ya miundombinu, hususan barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru sana wananchi wa Ileje kwa kuendelea kuniamini. Ninaishukuru familia yangu, ambayo inanipa ushirikiano mkubwa sana kuweza kutimiza majukumu yangu hapa, kama Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru wewe, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya, kuliongoza Bunge hili kwa kweli, kwa umahiri mkubwa, lenye viwango vya Kimataifa. Hongera sana Mheshimiwa Spika.
Mheshimiwa Spika, ninaishukuru Kamati yangu ya Miundombinu chini ya Mheshimiwa Selemani Kakoso kwa miongozo mbalimbali, ambayo anaitoa. Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge, ambao hakika lazima tukiri wametoa michango bora, yenye tija na ninasema tumeichukua yote na tutaifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, ninamwachia Mheshimiwa Waziri wangu aweze kuongea, lakini ninasema neno moja tu; mwaka huu tuna Mashindano ya AFCON. Moja ya eneo ambalo tunategemea kulifanyia kazi kubwa sana ni katika Mji wa Arusha.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kuanza kujenga miundombinu na hasa barabara, pale Mjini Arusha. Tunavyoongea mkandarasi ameanza kazi za mobilization kujenga; kwa watu wanaojua pale Arusha, kuanzia Mbauda, pale kwa Mrombo hadi Losiyani ambapo tayari, ataunganisha na ile Barabara ya Afrika Mashariki, njia nne.
Mheshimiwa Spika, pale Tea Packers, pale Moshono, kwenda Losiyani kuunganisha ile Barabara ya Afrika Mashariki. Pia, tunavyoongea tayari wametoa fedha, kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Barabara ya kutoka Airport, pale Kisongo kwenda Soko la Kilombero na kutoka Barabara ya Airport hadi Technical College, pale TCA, kwa njia nne. Hizo ndiyo barabara ambazo tunazijenga sisi TANROADS, zitakuwa zinaingiza watu katika uwanja ule wa Arusha. Pia, maelekezo yametolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu Barabara ya Tengeru kwenda Mererani ikiwa ni sehemu ya bypass, ambayo sisi kazi tunayoifanyia hiyo barabara ni namna ya kuijenga kwa uharaka.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais, ametoa fedha nyingi sana na tulichojifunza ni kwamba, unaweza ukawa na fedha, ukajenga barabara moja ndefu sana ya lami, lakini pengine isiwe na tija kuliko ukaainisha maeneo ambayo ndiyo vikwazo vya barabara, kama alichofanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ametoa zaidi ya shilingi 800,000,000,000 kuainisha madaraja ambayo yalikuwa yanakwamisha na leo watu wanapita, kwa hiyo, tumepata somo kubwa sana. Ninawahakikishia Waheshimiwa Wabunge tayari iko mipango, ataelezea Mheshimiwa Waziri, kuunganisha mikoa yote ambayo hawa Wabunge wameisema.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, ninaomba nimwachie Mheshimiwa Waziri wangu, aweze kufafanua na kujibu hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge, wamezitoa. Ninaomba kuunga mkono kwa asilimia mia moja hotuba hii ya bajeti, lakini pia na hii Bajeti yetu ya Ujenzi. Ahsante. (Makofi)