Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Yannick Ikayo Ndoinyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha mchango wangu kuhusu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, awali nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake na ujenzi mkubwa sana wa miundombinu za barabara, madaraja, usafiri wa anga na ardhini kwa kupitia SGR. Hata bajeti ya leo inadhihirisha dhamira njema ya Mheshimiwa Rais ya kujenga barabara na madaraja nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, aidha nikupongeze Mheshimiwa Abdallah Ulega na timu nzima ya Wizara kwa utendaji bora na usio na mashaka ya kuwahudumia Watanzania. Pamoja na pongezi hizi, ninawaalika kutembelea Wilaya yangu hasa kujionea miundombinu na hali zake.

Mheshimiwa Spika, kupitia Wizara hii, naomba Serikali itenge fedha na kuanza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kigongoni/Mto wa Mbu hadi Wasso, Loliondo. Barabara hii ina umuhimu wa kipekee kwa wananchi wa Jimbo la Ngorongoro na Mkoa wa Arusha kwa ujumla, kwa kuwa ndiyo kiungo muhimu kinachoweza kufungua wilaya yetu kiuchumi, kijamii na kiutawala.

Mheshimiwa Spika, Ngorongoro (Loliondo) imebaki kuwa miongoni mwa maeneo machache na kwa mazingira ya Mkoa wa Arusha ni wilaya yenye uhitaji mkubwa ambayo bado haijaunganishwa kikamilifu na barabara ya lami kuelekea makao makuu ya mkoa. Hali hii imekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji, wakulima na wafugaji wanaotegemea barabara hii kwa usafiri, biashara na huduma mbalimbali za kijamii.

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kigongoni/Mto wa Mbu hadi Wasso, Loliondo, ni barabara ya kimkakati. Ujenzi wake utafungua fursa kubwa za uwekezaji katika sekta za utalii, mifugo, kilimo, biashara na huduma. Kwa sasa wawekezaji wengi wamekuwa wakilalamikia changamoto ya ubovu wa miundombinu na ugumu wa kufika Loliondo, jambo linalopunguza kasi ya uwekezaji na maendeleo katika eneo hili lenye fursa nyingi za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, barabara hii pia ina umuhimu mkubwa kijamii na kikanda. Itawezesha wananchi wa Loliondo, Sale, Ngorongoro, maeneo ya Kanda ya Ziwa, pamoja na wananchi kutoka nchi jirani ya Kenya, kufika Arusha na Dodoma kwa urahisi zaidi. Aidha, itasaidia wakulima na wafugaji kusafirisha mazao, mifugo na bidhaa nyingine kwenda masokoni kwa gharama nafuu, kwa haraka na kwa usalama zaidi.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kusisitiza kuwa barabara hii siyo ombi jipya, tayari Serikali ilishafanya tathmini na kuanza utekelezaji kwa kujenga kipande cha Wasso hadi Sale chenye urefu wa kilometa 49. Hivyo, ombi letu kwa Serikali ni kuendeleza hatua iliyokwishakuanza kwa kukamilisha ujenzi wa barabara hii muhimu hadi Kigongoni/Mto wa Mbu.

Mheshimiwa Spika, tarehe 3 Oktoba, nilipata nafasi ya kumweleza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu umuhimu wa barabara hii kwa wananchi wa Ngorongoro. Kwa heshima kubwa, naiomba Serikali sasa ichukue hatua mahsusi ya kuiweka barabara hii katika vipaumbele vya utekelezaji ili wananchi wa Ngorongoro waweze kufurahia matunda ya ukuaji wa kasi wa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara hii utakuwa siyo tu utekelezaji wa ahadi ya maendeleo, bali pia ni hatua muhimu ya kuunganisha wananchi, kupunguza gharama za maisha, kukuza uchumi wa ndani, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha usalama wa kijamii na kiuchumi katika ukanda huu wa kimkakati.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, ninaomba kuwasilisha mchango wangu na ninaunga mkono hoja.