Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipatia nafasi hii kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara kwa kazi nzuri ya kuandaa bajeti hii yenye dira ya kuendeleza miundombinu ya barabara nchini. Bajeti ya shilingi trilioni 2.47 ya maendeleo inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuweka miundombinu kuwa engine ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa jitihada kubwa inazoendelea kuchukua kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara maeneo mbalimbali nchini, aidha, pongezi kwa kuendelea kukarabati barabara zilizopo na za vijijini, kuhakikisha miundombinu hii inakuwa imara muda wote. Serikali kupitia Wizara wameendelea kujenga madaraja maeneo yote korofi, kukarabatiwa ama kujengwa upya ili kutatua changamoto. Miundombinu ya barabara ni sehemu ya ukuaji wa uchumi wetu, hivyo ni wajibu kuhakikisha inapitika muda wote katika hali nzuri. Mwelekeo mkuu wa bajeti ya Ujenzi ya mwaka 2026/2027 una mikakati mbalimbali mizuri yenye tija kwa Taifa letu hasa kwenye kukuza uchumi.

Mheshimiwa Spika, barabara za kimkakati; kipaumbele kwa barabara za lami zinazounganisha mikoa na bandari, ikiwemo upanuzi wa Dar es Salaam - Morogoro Highway ni muhimu hasa ujenzi wa barabara njia 4/4 toka Kibaha Maili Moja hadi Chalinze.

Mheshimiwa Spika, kuhusu matengenezo ya barabara za vijijini; TARURA iongeze fedha zaidi kwa matengenezo na ujenzi wa barabara za wilaya, vijijini na mitaani. Kwa upande wa madaraja na mifereji: fedha zilizotengwa kwa madaraja katika maeneo yanayokatika wakati wa mvua zitumike ipasavyo kuhakikisha wataalam wetu wanayatambua maeneo hayo kabla ya dharura kutokea na kusababisha madhara makubwa ya njia kufungwa.
Mheshimiwa Spika, tuhakikishe matumizi ya teknolojia kwa kuanzisha matumizi ya teknolojia ya “cold mix” na “low-cost sealing” kupunguza gharama za matengenezo ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa Serikali kuipunguzia gharama.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla napenda kuzungumzia maeneo kadhaa ambayo Wizara inawajibu ya kuyazingatia kimkakati kwani maeneo hayo yana umuhimu kiuchumi kwa wananchi wangu, aidha, ni maeneo ambayo yana muda mrefu yamekuwa yakisahahulika ingawa nimeyasemea hapa Bungeni na Wizarani, maeneo hayo napenda kuyaelezea kama ifuatavyo; kwanza, naomba Wizara ielekeze fedha nyingi kwenye miradi mikubwa ya kimkakati. Expressway ya Kibaha – Mlandizi – Chalinze – Morogoro, upanuzi wa Kimara – Kibaha na Barabara ya Kisarawe – Mlandizi ni miradi ya kimkakati kwetu sisi Wana- Kibaha Vijijini.

Mheshimiwa Spika, miradi hii ikikamilika itapunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa zetu sokoni. Pili, iendeleze utaratibu wa PPP. Kumpata mwekezaji wa sehemu ya Kibaha – Chalinze ni hatua sahihi ya kupunguza mzigo kwa Serikali na kuharakisha utekelezaji. Ninaomba Wizara ihakikishe mchakato huu unakamilika ndani ya mwaka huu wa fedha ili wananchi waone matokeo na kufaidika na mradi huu.

Mheshimiwa Spika, tatu, Serikali iendelee kutenga fedha kwa matengenezo kupitia Mfuko wa Barabara. Shilingi bilioni 1,047 kwa matengenezo ni muhimu kwa sababu barabara nzuri zinazoharibika haraka hazisaidii wananchi na kupelekea kudumaza uchumi.

Mheshimiwa Spika, sasa niruhusu nizungumzie Kibaha Vijijini. Kibaha Vijijini ni kitovu cha kilimo na biashara kati ya Dar es Salaam na Pwani, lakini kwa miaka mingi tumekuwa tukipata changamoto ya barabara zinazoharibika haraka na Daraja la Mto Ruvu linalokatika kila msimu wa mvua. Natoa shukrani kwa Wizara kwa kutambua umuhimu wa eneo hili kwenye hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, miradi ifuatayo ni habari njema kwa wananchi wangu; Expressway ya Kibaha – Mlandizi – Chalinze – Morogoro; shilingi bilioni 1.320 zimetengwa. Hii ni hatua kubwa ya kubadilisha uso wa Kibaha Vijijini. Ninaomba utaratibu wa ununuzi wa mwekezaji wa Kibaha – Chalinze ukamilike mapema ili ujenzi uanze ndani ya mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, pili, Barabara ya Kisarawe – Mlandizi kilometa 119; fedha zilizotengwa kwa maandalizi. Barabara hii itaunganisha wakulima wa Mlandizi, Kwala na Dutumi na soko la Pwani na Dar es Salaam. Niombe Wizara iharakishe usanifu ili ujenzi uanze mwaka huu wa fedha na kukamilika kwa wakati ili wananchi wangu waanze kufaidika na kukuza uchumi wao.

Mheshimiwa Spika, tatu; Kibaha – Kiluvya – Kisarawe kilometa 22; fedha zilizotengwa naomba ziende kwenye mradi kwa wakati. Hii itafungua kata za jirani kutokea Kibaha Vijijini na Kisarawe, kupunguza muda wa kusafiri.

Mheshimiwa Spika, nne, fedha zilizotengwa kwa mradi wa Makofia – Mlandizi kilometa 36.7: Hii itasaidia wananchi wa sehemu ya Kaskazini ya Wilaya kufika Mlandizi kwa urahisi na kusaidia wakulima kufikisha mazao yao kwa wakati. Naomba fedha hizi zilizotengwa kwenye miradi hii zifike kwa wakati na miradi hii ianze mwaka huu wa fedha ili wananchi wa Kibaha Vijijini washuhudie miradi hii ikianza kutekelezwa kwani ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Aidha, miradi ya Barabara ya Makofia, Mlandizi Mzenga takribani kilometa 102 na kwa umuhimu wake barabara hii itakwenda kuunganisha bandari itakayojengwa Bagamoyo na Bandari Kavu ya Kwala.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Serikali ihakikishe miradi hii inakamilika kwa wakati kwenye mwaka huu wa fedha ili shughuli za kiuchumi kwa wananchi zianze mara moja na kuchangia pato kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, ingawa miradi hii ni mizuri, naomba nilete maombi matatu kwa niaba ya wananchi wa Kibaha Vijijini; moja, naomba Wizara iangalie upya Daraja la Mto Ruvu, Kijiji cha Mlandizi, wananchi wangu wamechoka kukatika kila msimu wa mvua. Ikiwezekana mradi huu uingizwe kwenye bajeti ya dharura au PPP ili utekelezwe haraka.

Mheshimiwa Spika, mbili, naomba Wizara ihakikishe fedha za TARURA zinafika Kibaha Vijijini kwa wakati. Mwaka jana tulichelewa kupata awamu ya pili na miradi mingi haikukamilika. Wananchi wanataka kuona Barabara za Dutumi – Gwata, Mtongani – Soga na Kwala – Kijijini zinakamilika kwa wakati na kwa ubora.

Mheshimiwa Spika, tatu, ninaomba Wizara ianzishe utaratibu wa kudhibiti malori mazito yanayopakia mkaa na mchanga kwenye barabara za vijijini. Barabara zetu zinaharibika ndani ya miezi sita kwa sababu ya uzito kupita kiasi. Bila udhibiti huu, hata tukijenga leo, kesho tutarudi Bungeni kuomba fedha tena.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, naiunga mkono bajeti hii kwa 100%. Ni bajeti ya matumaini kwa Kibaha Vijijini na Tanzania kwa ujumla. Nawaomba Waziri na timu yake wakae karibu na Halmashauri ya Kibaha Vijijini ili kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa ubora, kwa wakati na kwa gharama stahiki.

Mheshimiwa Spika, ahsanteni sana na Mungu ibariki Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja.