Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Adonis Alfred Bitegeko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ADONIS A. BITEGEKO: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Serikali kwa ujumla kwa kazi kubwa na ya kihistoria iliyofanyika mpaka sasa ya ujenzi wa miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Spika, ninashauri yafuatayo; kwanza kukamilisha mapitio ya Sera za Ujenzi na Usalama Barabarani. Serikali ikamilishe mapitio ya sera hizo na kuandaa mipango mikakati ya kuzitekeleza ili ziweze kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea kutokea nchini na duniani ikiwa ni pamoja na kukidhi malengo ya Dira 2050.

Mheshimiwa Spika, pili, kuwalipa wakandarasi na wahandisi washauri; Serikali kupitia Wizara ya Fedha itafute fedha na kulipa madai ya wakandarasi na wahandisi washauri ili kuwezesha miradi ya barabara na vivuko kutekelezwa kwa wakati na kupunguza riba.

Mheshimiwa Spika, tatu, fedha za Mfuko wa Barabara ziingizwe moja kwa moja katika akaunti ya Mfuko wa Barabara (RBF) zilizopo Benki Kuu na zitumike tu katika ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Spika, Wizara kuleta fedha katika Mkoa wa Kagera zilizotengwa katika mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Nashauri Serikali ipeleke fedha katika bajeti za mwaka 2025/2026 katika Mkoa wa Kagera ili ujenzi wa barabara ufanyike. Barabara nyingi zimeathirika na mvua zilizonyesha.

Mheshimiwa Spika, uchache wa fedha zilizopo katika makadirio ya mpango na bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa Mkoa wa Kagera. Fedha zilizotengwa takribani shilingi bilioni 14 ni chache kwa Mkoa wa Kagera kutokana uhitaji wa ukarabati wa barabara na madaraja na ujenzi wa barabara na madaraja. Serikali iangalie uwezekano kuongeza bajeti ya Mkoa wa Kagera ili iendane na mahitaji ya mtandao wa barabara wa Mkoa wa Kagera takribani kilometa 2156.

Mheshimiwa Spika, halmashauri zinunue na kutumie mitambo ya ujenzi wa barabara ili kupunguza gharama; na Serikali itoe kipaumbele katika kukamilisha miradi ya ujenzi na ukarabati barabara na madaraja badala ya kuanza miradi mipya.

Mheshimiwa Spika, kutokana na Wabunge wengi kutoa ushauri unaohusiana na kutokuwepo kwa fedha za kutosha za ujenzi au ukarabati na barabara na madaraja ni vyema Serikali ikatoa kipaumbele na kufanya tathmini ya mfumo mzima wa upatikanaji wa fedha na ujenzi wa miundombinu hiyo ili tupate suluhisho la kudumu/muda mrefu ya changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika, kufanya pia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kata ya Nshamba mpaka Kata ya Mushabago katika Jimbo la Muleba Kaskazini na Kamachumu mpaka Hospitali ya Ndolage, Jimbo la Muleba Kaskazini, Wilaya ya Muleba.

Mheshimiwa Spika, vilevile, kufanya mapitio ya usanifu wa barabara ya lami ya Muhutwe-Kamachumu-Muleba kipande cha mteremko na kona ya Kyamalebe (kilichopo Kata ya Ibuga), Wilaya ya Muleba. Kipande hicho cha barabara kimekuwa na ajali ya nyingi za vyombo vya moto na watu kupoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Waziri wa Ujenzi atume timu ya wataalamu kufanya tathmini ya eneo na kufanya maamuzi ya kitaalamu.

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja.