Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Spika, naomba niwasilishe mchango wangu kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha miundombinu ya barabara. Niishukuru Serikali kwa kutujengea barabara ya lami kutoka Lamadi, Bariadi, Itilima, Maswa hadi Mwigumbi ambayo inaunganisha Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu na Makao Makuu ya Mikoa ya Mara na Shinyanga.
Mheshimiwa Spika, pamoja na shukrani hizi niombe Wizara ione namna ya kuiimarisha barabara hii kwani ina mashimo mengi kwa sasa na huharibika mara kwa mara. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Mkoa wa Simiyu na mikoa ya jirani ya Kanda ya Ziwa hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa wa Simiyu ndio mzalishaji mkubwa wa zao la pamba (51%+ ya pamba inazalishwa simiyu).
Mheshimiwa Spika, sera ya Serikali ni kuunganisha makao makuu ya kila mkoa Tanzania Bara na makao makuu ya kila mkoa jirani kwa barabara ya lami. Wakati Simiyu ikiwa sehemu ya Mkoa wa Shinyanga, Mkoa wa Shinyanga ulikuwa uunganishwe na mikoa ya Mara kupitia Mwigumbi, Maswa, Bariadi na Lamadi na tayari kipande hiki kimekamilika, japo kinahitaji ukarabati wa hali ya juu. Barabara hii ni muhimu sana hasa kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara wanaohitaji kupeleka bidhaa zao makao makuu ya nchi yetu (Dodoma) na Mkoa wa Dar es salaam, kwani hawatahitaji kuzungukia Mwanza – Shinyanga. Njia hii ni fupi kwao kwani wakitoka Musoma wanapita Lamadi - Bariadi - Maswa Shinyanga - Singida – Dodoma – Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, hapo awali kuunganisha Mkoa wa Shinyanga na arusha kiunganishi ilikuwa ni kupitia Kolandoto – Mhunze – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti- Matola – Mangola - Oldean Kisha – Mto wa Mbu – Makuyuni - Arusha. Ahadi ya kujenga barabara ya Kolandoto - Oldean imekuwa kwenye bajeti ya Serikali tangu Awamu ya Pili lakini mpaka tunavyozungumza bado haijajengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali yangu sikivu ikamilishe ujenzi wa barabara hii muhimu ili kujenga imani kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza kwanza na ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti ambalo lilikamilika wakati wa Awamu ya Tano tayari Simiyu ikiwa ni mkoa unaojitegemea, ili kurahisisha mawasiliano. Baada ya Simiyu kuwa mkoa, kiunganishi na Mkoa wa Singida ni kutoka Bariadi - Lagangabilili - Mwanhuzi – Sibiti – Iguguno - Singida.
Mheshimiwa Spika, niombe sana Serikali yangu sikivu ione umuhimu wa kujenga barabara hii muhimu sana kwa uchumi wa hii mikoa miwili na hasa ukuzingatia kuwa ndio shortcut ya kufika Dodoma makao makuu ya nchi ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Arusha kiunganishi ni Bariadi - Mwanhuzi – Matola - Mangola – Oldean – Arusha. Hivyo basi kwa Simiyu na Shinyanga bado barabara ya Kolandoto -Mwanhuzi- Sibiti – Mangola – Matola – Oldean – Arusha ni muhimu sana kwa uchumi wa mikoa hii mitatu. Hapa katikati kulikuwa na hoja ya wafadhili kutoafiki Mkoa wa Mara kuunganishwa na Mkoa wa Arusha kupitia Mbuga ya Wanyama ya Serengeti. Wafadhili walikuja na hoja kuwa Mkoa wa Mara kiunganishi kiwe barabara kutoka Oldean – Mangola – Matola – Sibiti – Mwanhuzi – Lalago – Maswa – Bariadi - Lamadi kwa maana ya Serengeti Southern Bypass.
Mheshimiwa Spika, ninaomba niunge mkono hoja hii kwa manufaa ya kulinda utajiri wa mbuga yetu ya Serengeti ambayo ina vivutio vya utalii kama vile migration ya wanyama kuelekea Kenya, Masai Mara. Kivutio adimu duniani kinachochochea utalii, na ni moja ya World Heritage Sites. Barabara hii ya Serengeti Southern Bypass ni muhimu kwa uchumi wa mikoa hii hvyo niiombe Serikali yangu sikivu iendelee kutenga pesa za ujenzi wa barabara hii kadri bajeti itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Spika, ninatambua na kuheshimu mawazo ya wenzetu wa Mkoa wa Manyara unaotaka barabara ya kuunganisha Mara na Arusha isianzie Oldean bali ishuke kidogo kuelekea Karatu – Mbulu – Dongobeshi - Hydomu -Matola – Sibiti – Lalago – Maswa (badala ya Oldean – Mangola – Matola) na hapa niipongeze Wizara kwani kwenye bajeti hii nimeona kuna ujenzi wa kiwango cha lami barabara kutoka Karatu – Mbulu – Hydom – Sibiti – Lalago – Maswa (kilometa 389).
Mheshimiwa Spika, pia kuna maandalizi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kolandoto – Kishapu – Lalago. (kilometa 64), lakini pia barabara ya Lalago – Ngoboko – Mwanhuzi (kilometa 74), na Iguguno Shamba – Mnolo (kilomita10). Hapa naomba kipande hiki kije kiunganishwe sasa na Mwandoya (Kisesa) – Lagangabilili – Bariadi.
Mheshimiwa Spika, ninaomba pia nipongeze ujenzi wa Daraja la Simiyu ambalo limekamilika kwa 73% na hivyo basi kurahisisha ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Spika, barabara nyingine muhimu na ambayo ni shortcut ya kuunganisha Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Mwanza ni barabara kutoka Bariadi - Ngulyati, Salama - Magu.
Mheshimiwa Spika, barabara hii ni muhimu sana, sio kiuchumi tu, bali pia katika kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi wanaokimbizwa Hospitali ya Bugando katika jitihada za kuokoa maisha ya wagonjwa hawa. Hivyo kadri bajeti itakavyoruhusu niiombe Serikali ione umuhimu wa kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, barabara nyingine muhimu pia ni ya kutoka eneo la Dutwa - Ngasamo – Nyashimo; eneo la Dutwa lina madini ya nickel na dhahabu pia. Barabara hii itafungua uchumi wa wananchi wa maeneo haya na kukuza pato binafsi, lakini pia pato la Taifa litakalotokana na tozo za madini haya.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unapita katika eneo la Malampaka, Jimbo la Maswa Magharibi, na kwa kuwa eneo hilo panatarajiwa kujengwa bandari kavu, niiombe sana Serikali ijenge kwa kiwango cha lami barabara kutoka Njia Panda kwenda Malampaka ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na barabara hii iambatane na taa za barabarani.
Mheshimiwa Spika, niombe sana na niungane na Wabunge wenzangu kuomba makusanyo ya road fund yaelekezwe kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara. Nimeona maoni ya Kamati ya Miundombinu kuwa Serikali ione namna ya kuongeza shilingi 100 kwenye miamala ya simu.
Mheshimiwa Spika, gharama za simu bado ni kubwa kwa mwananchi wa kawaida, hivyo kuweka ongezeko hili ni kumbebesha mwananchi mzigo, labda shilingi hii mia iwe kwenye data na sio kwenye muda wa maongezi. Ushauri wangu ongezeko hili liweke kwenye vinywaji ikiwemo bia, vinywaji vikali na kwenye sigara, kwani hivi sio necessity ni luxury.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na ninaomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja.