Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Esther Nicholas Matiko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tarime Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna Serikali ya Awamu ya Sita inajitahidi kuwekeza kwenye miundombinu ya barabara na sekta ya usafirishaji kwa ujumla, tumeona kuwa katika Awamu ya Sita imeweza kujenga kilometa 1,495.45 ambapo inafanya jumla ya mtandao wa barabara za lami kuwa jumla ya kilometa 12,225.6 na kubakiza kilometa 25,508.8. Hii ni hatua kubwa sana ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja makubwa na ya kimkakati katika kujenga uchumi imara.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa Barabara ya Tarime - Mugumu kwa viwango vya kimkakati; baada ya pongezi naomba kuzungumzia Barabara ya Tarime – Mugumu kama kichocheo cha uchumi na utalii. Barabara ya Tarime – Mugumu isiangaliwe kama Mradi wa Mkoa wa Mara pekee, bali kama strategic economic corridor inayounganisha biashara, madini, utalii na usafirishaji katika ukanda wa Kaskazini. Hivyo lazima Serikali ione umuhimu wake kwa utalii wa Serengeti, usafirishaji wa madini, biashara ya mipakani na mazao ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, miundombinu yenye tija ni ile inayozalisha uchumi, siyo inayounganisha maeneo pekee. Kwenye hotuba ibara ya 50 imeonesha hii barabara yenye kilometa 87.14 ni kipande cha Mogabiri hadi Nyamongo chenye kilometa 25 ndio pekee kimejengwa kna utekelezaji upo asilimia 61 tu. Lakini kipande cha Tarime Mjini hadi Mogabiri chenye kilometa 9.3 ni kimeharibika sana na mkandarasi ameshatoa certificate ya shilingi bilioni 7.99 lakini Serikali hadi leo haijapeleka fedha na iliahidi kupeleka fedha kabla ya mwaka huu wa fedha wa 2025/2026 kuisha.

Mheshimiwa Spika, hii barabara imepoteza maisha ya Watanzania wengi ikiwemo Diwani Philip, mfanyakazi wa halmashari na wengine wengi. Vilevile imesababisha ulemavu kwa wananchi wengi na kupunguza nguvu kazi ya Taifa letu, lakini pia kuna kipande cha Nyamongo hadi Mugumu chenye kilometa 48.15 na ile barabara ya mzunguko pale Mugumu yenye kilometa 3.6. Kwa masikitiko makubwa ibara ya 251 inaonesha hii barabara imetengewa shilingi bilioni saba tu kwa mwaka 2026/2027. Hii sio sawa, labda kama kuna fedha zinatoka kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha.

Mheshimiwa Spika, Serikali itambue kuwa barabara hii siyo tu ya wananchi wa Mara, bali ni mhimili wa biashara, utalii na usafirishaji kuelekea ukanda wa Serengeti. Kukamilika kwake kutapunguza gharama za usafiri, kuongeza mapato ya utalii na kurahisisha usafirishaji wa mazao na madini na mapato yatakayopatikana yatatumika kujenga barabara na miundombinu mingine kwenye maeneo ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, kuhusu madeni ya wakandarasi na athari kwa mfumo wa fedha wa ndani; kuchelewa kulipa wakandarasi wa ndani ni sawa na kuondoa ukwasi kwenye mzunguko wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, madhara ya kutolipa kwa wakati hupelekea wakandarasi hushindwa kulipa benki, riba huongezeka, ajira hupotea, gharama huongezeka kupitia penalt na riba na miradi kuchelewa kukamilika.

Mheshimiwa Spika, nashauri kuepuka haya kuwepo na Escrow/Payment Guarantee System, Predictable Payment Mechanism au mfuko maalum wa kulipa madai ya miradi iliyokamilika.

Mheshimiwa Spika, kupunguza mikopo yenye riba kubwa katika miradi ya ujenzi; Taifa linaweza kujenga barabara kwa gharama nafuu, lakini likaingia hasara kupitia gharama kubwa za fedha za mikopo. Baadhi ya mikopo ya miradi ya miundombinu ina gharama kubwa za riba ambazo zinaongeza deni la Taifa bila sababu. Hivyo napenda kuishauri Serikali kuongeza matumizi ya PPPs, infrastructure bonds, concesional financing na mifuko ya ndani ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kuna wakati Taifa haliumizwi na gharama ya ujenzi, bali gharama ya fedha iliyokopwa kujenga. Hivyo ni vyema tuweze tumia concesional financing, infrastructure bonds, PPP na matumizi ya local pension funds.

Mheshimiwa Spika, sustainability ya deni la Taifa haitegemei ukubwa wa mkopo pekee, bali gharama ya fedha yenyewe.
Mheshimiwa Spika, kuhusu maintenance economy - kulinda miundombinu Iliyojengwa; tumejikita sana kwenye kujenga, lakini bado hatujawekeza vya kutosha kwenye uchumi wa matengenezo ya miundombinu.

Mheshimiwa Spika, ninashauri Serikali ione umuhimu wa preventive maintenance, matumizi ya teknolojia, drainage systems na asset management systems. Lazima tujue barabara nyingi haziharibiki kwa uzito wa magari pekee, bali kwa kukosekana kwa mfumo endelevu wa matengenezo.

Mheshimiwa Spika, hatua ya maendeleo ya Taifa lolote huonekana kwanza kwenye ubora wa miundombinu yake. Hata hivyo, miundombinu bora siyo ile inayojengwa kwa kasi pekee, bali ile inayojengwa kwa tija, inalindwa kwa weledi na inachochea ushindani wa uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, miundombinu ya barabara inahitaji maintenance, lakini kuna changamoto ya kutolipwa Mfuko wa Barabara. Hasara ya kutotoa fedha hizi ni kubwa na zipo kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, ushauri zingatieni sheria, hakikisheni fedha hizi za mfuko zinatumika kadri zinavyokusanywa.

Mheshimiwa Spika, tunajisifu mafanikio ya bandari, lakini siri kubwa ya mafanikio haya ni Mfuko wa Huduma ya Bandari ambapo TPA anaruhusiwa kukusanya pesa na kumuwezesha kutekeleza miradi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wakandarasi wazawa kupewa kipaumbele kwenye miradi mikubwa ya ujenzi; wakandarasi wazawa wanakopa kwenye mabenki yetu kwa riba kubwa sana ukilinganisha na gharama ya fedha wanayoipata wakandarasi wa nje kutoka taasisi za kifedha za kimataifa. Jambo la kujiuliza ni hili, Serikali inapochelewa kuwalipa wakandarasi wa nje, madai yao yanaendelea kuongezeka kupitia interest charges na contractual penalties, wakati kwa wakandarasi wazawa wanapocheleweshewa malipo huishia kulipwa contractual penalties bila interest charges. Hii sio sawa na hudhoofisha wakandarasi wazawa na hata kupelekea kufilisika.

Mheshimiwa Spika, hivyo Taifa hupata double financial exposure; kwanza kupitia gharama kubwa za fedha kwa wakandarasi wazawa na pili kupitia escalation ya madai ya wakandarasi wa nje kutokana na kucheleweshwa kwa malipo na ikizingatiwa kuwa wakandarasi wa nje miradi yao ina gharama kubwa zinazotokana na mikataba yao hususani pale miradi inapofadhiliwa kwa mikopo yenye riba kubwa na masharti ya kibiashara.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa mapendekezo yafuatayo:-

(i) Serikali iweke mfumo wa prompt payment kwa wakandarasi ili kuzuia escalation ya claims na riba.

(ii) Benki za maendeleo na taasisi za fedha ziweke special infrastructure financing window kwa wazawa yenye riba nafuu.

(iii) Miradi mikubwa iwe na kiwango cha lazima cha ushiriki wa wakandarasi wazawa.

(iv) Serikali ifanye contract risk assessment kabla ya kuingia mikataba yenye penalty clauses kubwa.

(v) Contractors Assitance Fund (CAF) iongezewe kiwango toka dhilingi bilioni nne hadi walau shilingi bilioni 500.

Mheshimiwa Spika, ulinzi wa wakandarasi wazawa si suala la upendeleo bali ni mkakati wa kulinda mtaji wa ndani, ajira za Watanzania na uthabiti wa kifedha wa taifa.

Mheshimiwa Spika, mwisho, lazima ujenzi wa barabara uendane na kasi ya maboresho ya bandari na ujenzi wa reli tunaona vituo vya SGR vimekamilika, SGR inafanya kazi, lakini hakuna barabara au zipo finyu. Hivyo kasi ya reli na barabara zisipishane na kuna maeneo TANROADS ifanye kazi mgongoni mwa TRC kutokana na changamoto ya kifedha, kama kuna sehemu tunahitaji kuendeleza reli hatuna budi kuchagua wapi zitakutana na sio lazima zi-run in parallel.

Mheshimiwa Spika, katika hili tunawapongeza sana Uchukuzi kwa kuunganisha matumizi ya SGR bandarini mpaka Bahi na MGR toka Bahi mpaka Isaka. Sasa kutoka Isaka ni barabara, kwa mfumo huu itawezekana kuokoa barabara za Dar es Salaam - Morogoro - Dodoma.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.