Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Lucy Simirya Kombani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. LUCY D. S. KOMBANI: Mheshimiwa Spika, ninapenda kushukuru kwa nafasi hii ya kuweza kuwasilisha mchango wangu katika bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuona umuhimu wa ku-support miundombinu katika mkoa wetu, hili kwetu ni kubwa sana kwani limekuwa linaturahisishia kwenye masuala mbalimbali hasa ya kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nishukuru kwa juhudi nzima ya kujumuisha mradi wa Barabara ya Nachingwea-Liwale-Ilonga-Mwaya-Mahenge (kilometa 345) kwenye mpango wa bajeti wa mwaka 2026/2027, mradi ambao utakapokamilika utaunganisha Mkoa wa Lindi na Morogoro, jambo ambalo Wana-Morogoro tunategemea kunufaika kwenye mahusiano ya kilimo hasa kwenye mazao ya korosho na ufuta na pia muunganiko wa kimasoko katika mazao hayo.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kushukuru pia kwa kutambua umuhimu wa Barabara ya Kidatu-Ifakara-Lupiro-Malinyi-Londo-Lumecha/Songea (kilometa 499) (ukurasa wa 29). Barabara hii inaenda kusaidia siyo tu wananchi wa Malinyi, bali inaenda kurahisisha mahusiano ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Songea, kwa kurahisisha usafiri wa wananchi pamoja na mazao.

Mheshimiwa Spika, pia kwa sasa hospitali kubwa ya rufani ambayo inafanya matibabu hadi ya kansa inapatikana Ifakara, hii itawarahisishia wananchi wa mikoa ya jirani kusafiri kwa urahisi na kupata matibabu kwa amani hasa pale wanapotakiwa kurudi mara kwa mara kwenye kliniki za Chemotherapy.

Mheshimiwa Spika, maombi yangu; Barabara ya Lupiro kuelekea Mahenge ambayo ni kilometa 40 tu ambayo ina milima na kona nyingi sana. Barabara hii imekuwa haipitiki kipindi cha masika jambo ambalo limekuwa likikwamisha sana shughuli mbalimbali za kijamii na za kiuchumi. Wilaya ya Ulanga imekuwa ikitegemea Ifakara kwenye mahitaji ya bidhaa mbalimbali ikiwa bidhaa za chakula, dawa, hata matibabu ya rufani na operation wananchi wa Ulanga wamekuwa wakitegemea kupata Ifakara.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi haya mahitaji yamekuwa ni magumu kupatikana kwani barabara zinakuwa hazipitiki hasa pale magari yanapokwama njiani hata siku tatu. Wilaya ya Ulanga imekuwa na utajiri mkubwa wa madini na pia wawekezaji wamekuwa wakishindwa kufika huko kwa kipindi chote cha masika. Wizara tunaomba muangalie hili jambo kwa ukaribu kwani tunaamini kama barabara itajengwa kwa kiwango cha lami na wawekezaji wataongezeka huko.

Mheshimiwa Spika, ombi la pili; hotuba imeainisha barabara ya Ifakara – Kihansi – Mlimba – Madeke – Kibena (kilometa 346.43); Ifakara – Mlimba (kilometa 62.5) na Mbingu - Chita JKT (kilometa 37.5) kwamba maandalizi ya kuanza kazi yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, tunaomba majibu ya lini hii kazi itaanza kwani kwa mhandisi kujiandaa tu, tutashindwa kufuatilia hili jambo kwani hakuna time frame ambayo Wizara imeji-commit kwenye hili jambo.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia napenda kuunga mkono hoja.