Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono bajeti hii ya Ujenzi. Pili, nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali na kipekee Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kutoa kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji nchini ikiwemo barabara, vivuko, meli, viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Njombe ni mkoa wenye mvua nyingi sana kwa mwaka, hivyo changamoto ya usafiri hasa barabara ni kubwa sana. Tunaiomba Serikali kutoa kipaumbele kwa kutenga na kuongeza ukubwa wa bajeti ya kutosha kwa ajili ya barabara za Mkoa wa Njombe ili wananchi wetu waweze kusafiri kwa wakati na kusafirisha mazao ya chakula na biashara kwa uhakika.
Mheshimiwa Spika, aidha wananchi wa Jimbo la Lupembe wanaimba kujua ni lini Barabara ya Kibena - Lupembe hadi Madeke kilometa 126, itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hii ilitangazwa tender ya ujenzi tarehe 12 Februari, 2025 kwa kuanza na kilometa 42 (Kibena hadi Kidegembye), hata hivyo hadi leo mkataba huo haujasainiwa.
Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali iharakishe kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara hii ili kuwanusuru wananchi hawa na adha ya usafiri katika barabara hii kwani barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Mikoa ya Njombe na Morogoro hadi Tanga kupitia Kilosa. Aidha, barabara hii itafungua uchumi na uwekezaji mkubwa kwa Mkoa wa Njombe na Morogoro na kuchangia Pato la Taifa kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.