Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungi anayetujalia uzima na kutujalia amani katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayotufanyia Watanzania. Hakika Rais wetu amefanya mambo mengi na makubwa sana katika Taifa letu. Leo karibu barabara zote kuu zimejengwa kwa kiwango cha lami. Hongera sana. Tuliona kama ni hadithi au ndoto ya mchana kuwa Watanzania tungeweza kusafiri kutoka Mtwara mpaka Kagera kwa kutumia gari ndogo (Toyota Mark II, IST, Corola, Carina na kadhalika). Waheshimiwa Wabunge, ndoto hii leo imekuwa kweli. Tunawashukuru sana viongozi wetu wakuu kwa kazi hii waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana vilevile Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya. Wameyapokea maelekezo na maono ya Mheshimiwa Rais na kuyaweka katika vitendo hakika wameitendea haki Wizara hii. Niwapongeze zaidi kwa kuwa wanyenyekevu na wasikivu kwa wananchi na husasani kwa Wabunge, hii imetupa moyo sana.
Mheshimiwa Spika, tunajua bado kuna kazi kubwa ya kufanya, lakini tunasema safari ni hatua kuna siku nchi yetu itakuwa na barabara nzuri kama matamanio ya Watanzania ambayo wangependa.
Mheshimiwa Spika, hii nchi ni kubwa, tuna mtandao mrefu wa barabara zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi ambao wa urefu wa kilometa 37,734.41 hii sio kitu chepesi kwamba tutalala, tuamke tukiwa tumezimaliza barabara zote kwa kiwango cha lami siyo jambo jepesi. Hata hivyo, tunaipongeza Serikali kuona kila sehemu ya nchi ina barabara za lami. Kiasi cha kilometa 12,225.26 zimeshajengwa kwa kiwango cha lami. Hongereni sana.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi ikamilishe barabara kuu zinazounganisha mkoa na mkoa ikiwemo Barabara ya Ipole-Rungwa mpaka Mbeya na Sikonge-Kiloleli-Kipili mpaka Singida. Kujengwa kwa barabara hizo kwa kiwango cha lami unaenda kufungua uchumi wa Mikoa ya Tabora, Singida na Mbeya.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, sasa nilete kilio cha wananchi wa Mkoa wa Tabora na hususani wananchi wa Sikonge.
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Ipole-Rungwa yente urefu wa kilometa 172.4 ni kati ya barabara kuu (truck road) iliyobaki bila kujengwa kwa kiwango cha lami katika Taifa letu la Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa zaidi ya miaka 30 sasa. Aidha, imekuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi zaidi ya ilani tano na kwa nyakati tofauti tofauti viongozi wetu wakuu wametoa maelekezo ya kuitengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya barabara hii bado haijajengwa. Hata hivyo turejee semi za wahenga wetu kwamba; “yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo.” Wana-Sikonge tunampenda sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na yeye anatupenda sana na tunaamini barabara hii ataijenga kabla kipindi chake hakijaisha.
Mheshimiwa Spika, sauti za watangulizi wangu Bungeni; nawashukuru sana watangulizi wangu waliokuwa Wabunge wa Jimbo la Sikonge akuwemo Mheshimiwa Said Juma Nkumba ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tabora. Katika kipindi chake chote cha Ubunge kwa miaka 15 ameisemea sana barabara hii na kuzitamka waziwazi faida za kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa George Joseph Kakunda, katika kipindi chake cha miaka 10 amepaza sauti sana kuhusu ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Spika, ni nani sasa aje aisemee barabara hii ndiyo ijengwe? Mheshimiwa Waziri, nikukumbushe maandiko matakatifu kutoka Kitabu cha Injili ya Luka Mtakatifu Sura ya 16:19 – 31 kwa kifupi; “Ni habari ya Tajiri, Lazaro na Nabii Ibrahimu. Kwamba Tajiri alipoona mbinguni kuna moto mkali sana alimwomba Nabii Ibrahimu atume watu kutoka mbinguni ili wakawaambie ndugu zake waliokuwa duniani kuwa waache dhambi, wasije wakapata mateso kama yeye aliyokuwa anayapata. Nabii Ibrahimu akamwambia wasipokuwasikiliza.” Mwisho wa maneno matakatifu.
Mheshimiwa Spika, Waziri Ulega ni msikivu nina hakika ataitendea haki barabara hii na hana sababu ya kumsubiri malaika kutoka mbinguni kwa ajili ya ujumbe wa barabara hii.
Mheshimiwa Spika, nina imani sana na Mheshimiwa Waziri kwa sababu ameshaahidi kuitembelea barabara hii mara baada ya Bunge hili ili kuwasikiliza wananchi wahanga wa barabara hii wakiwemo Kata za Ngonywa, Kitunda, Kiloli, Kilumbi, Kipili na wenzao wa Singida na Mbeya. Hii inanipa matumaini sana kwamba sasa Rais wetu Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan anaenda kuandika historia nyingine ya kutujengea barabara yetu hii hata kabla ya kipindi chake kuisha.
Mheshimiwa Spika, ninamwomba Mungu wa mbinguni awaongoze katika kutafuta fedha ya barabara hii na barabara zingine za Watanzania wenzangu ili tuzidi kuwakumbuka katika historia ya maisha ya Wanasikonge na Watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, barabara hii ni ufunguo wa uchumi katika mikoa ya Tanzania pamoja na nchi jirani na hususani nchi za Maziwa Makuu. Barabara ya Ipole - Rungwa inaunganisha Mkoa wa Tabora na Mikoa ya Mbeya na Singida. Hivyo kujengwa kwa barabara hii kwa kiwango cha lami itawezesha wafanyabiashara wa Tabora, Mbeya na Singida kufanya biashara zao kwa urahisi na ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, Tabora tuna mazao mengi ya misitu ikiwemo asali na mbao, lakini tuna mazao ya kilimo yakiwemo mahindi, karanga, mpunga na kadhalika ambayo tungependa kuyauza Mikoa ya Kati na ya Nyanda za Juu Kusini na hata nje ya nchi ikiwemo Malawi, Zambia na hata Afrika Kusini. Hii itawezekana tu kama barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo juu kuwa barabara hii (Ipole-Rungwa) inatoa wepesi na kupunguza gharama za usafiri wa wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Shinyanga, Mwanza, Mara, Geita, Kagera na Kigoma. Kwa vile wanaposafiri kwenda Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini nawatalazimika kupitia Dodoma - Iringa hadi Mbeya kwani route hii ina urefu kilometa 970, lakini kama kipande cha Barabara ya Ipole - Rungwa kitajengwa kwa kiwango cha lami umbali wa Tabora hadi Mbeya ni kilometa 562 tu; tofauti ya kilometa zaidi ya 400. Hivyo watapunguza muda, uchovu wa safari na kupunguza gharama za mafuta.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika wasafiri kutoka nchi jirani za Rwanda, Burundi DR Congo na kadhalika wanaosafiri kwenda Kusini mwa Afrika watatumia barabara hii kwa sababu nilizozisema hapo juu. Tunaomba Serikali ione haja ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Sikonge – Kiloleli – Kipili; wananchi wa Sikonge wanatambua majibu ya Serikali wakati wa majibu ya Swali Namba 81 pamoja na swali la nyongeza. Majibu ya Serikali ni kwamba Serikali itaanza kuifanyia barabara hiyo upembuzi yakinifu ili kuona namna ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Wana-Sikonge wanaomba kuona sasa watalaam wanaanza kuifanyia barabara hiyo upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu; kama nilivyosema hapo juu, nchi yetu ni kubwa na inahitaji fedha nyingi kukamilisha ujenzi wa barabara zetu kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Waziri kuna watu huko duniani wana fedha nyingi sana na wanatafuta mahali pa kuziwekeza. Mimi nashauri kaeni na Wizara ya Fedha ili muingie makubaliano na wenye fedha duniani kuwa watujengee barabara zote kwa makubaliano kuwa kila mwaka tutawalipa sehemu ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya barabara; tuseme angalau shilingi trilioni moja kwa mwaka ambazo ni sawa na wastani USD million 400 zinazotokana na bajeti yako, watakubali tu! Hii itafanya changamoto za barabara kuisha na wananchi wetu watakuwa na barabara nzuri na deni lao tutalilipa kwa namna tutakavyokubaliana na wawekezaji.
Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja.