Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Isack Joseph Copriano

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Spika, ninachukua nafasi hii kukushukuru kwa kupata nafasi ya kuwa sehemu ya wachangiaji kwenye Wizara.

SPIKA: Jiandae Naibu Waziri.

MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyosema, kwamba madaraja zaidi ya 81 yameshajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninataka nishauri jambo dogo tu. Watu wamelia sana na barabara nyingi na barabara nyingi ni kweli zimeharibika. Ninawaomba kwanza TANROADS, hii biashara ya barabara zilizokufa kuanza kuziba mashimo, hebu iishe. Kama ni hizo fedha chache Mheshimiwa Waziri zinazopatikana, afadhali hata ijengwe kilometa moja kuliko kuziba mashimo ambayo yanaharibu magari ya Watanzania. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, la pili, lazima mrudi kwenye Sheria yetu ya Manunuzi, muiangalie upya Mheshimiwa Waziri. Kwa sababu sheria hizi za kutaja mtu ambaye ni lowest ndiyo apewe kazi, ndiyo inatupelekea sisi Watanzania kupata kazi chafu na ambazo hazina ubora. Lazima turudi tuangalie kwenye upande huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sitaki kusema sana leo kwa sababu kwanza nimepata bahati, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwamba anakwenda kulijenga lile Daraja la Mto Athumani kutoka Selela – Ngaruka; Ngaruka – Oldoinyolengai; na Oldoinyolengai – Loliondo. Wote waliona fika kipindi fulani lile daraja lilichukua mpaka magari ya wananchi. Juzi nilipokuwa jimboni nimepita nimekuta wataalamu wameshaanza kazi yao nzuri ya upembuzi pale kwa ajili ya ujenzi wa daraja lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, ninamwomba Mheshimiwa Waziri, ninajua wameshatangaza tender ile ya kilometa 23 kwenda kwenye ujenzi wa Kiwanda cha Magadi kule Selela na Engaruka, basi mkataba usainiwe, ili ile kazi ikaanze. Tuna Barabara ya kilometa 11 kutoka Monduli Mjini kwenda Mfere, kwenda mpaka Monduli Juu kwa Sokoine, naomba ikaanze.

Mheshimiwa Spika, leo siombi lami nyingi, ninataka nimwombe Waziri; wengi wameomba lami, mimi ninaomba barabara za changarawe. Kwa hiyo, nipo tofauti kabisa, ninaomba barabara ya changarawe. Sasa akininyima tena hiyo Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu ananisikia hapa na TANROADS wote wananisikia. Ninampongeza sana Meneja wangu wa TANROADS, Mkoa wa Arusha, ni meneja msikivu na tunamwomba Mheshimiwa Waziri, tunapomsifia mtu siyo ndiyo umhamishe. Ni meneja msikivu, ukimpigia simu wakati wowote, panapotokea tatizo lolote kwenye barabara zile za vijijini, sekunde amefika. Ni meneja wa mfano sana Ndugu yetu Masawe, salute kwake kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya mkoa wetu.

Mheshimiwa Spika, mimi ninaomba Barabara ya kutoka Monduli Juu – Mfereji; Mfereji – Ol Doinyo Lengai mpaka Engaruka kilometa 123, mimi niwekee changarawe wananchi wangu wapite kwa amani, mimi siombi lami hiyo. Barabara ya kutoka Meserani – Naalarami – NAFCO mpaka Lolkisale na kwenda kukutana na barabara ya kwenda kule kwa wenzetu Simanjiro. Mheshimiwa Waziri aniwekee changarawe ipitike, wananchi wangu waache kupata kero kwa sababu, ndiyo pekee ambayo ninaona wengi hawajaomba.

Mheshimiwa Spika, ninaomba hiyo na ninaamini atakapokuja kusimama hapa ataniambia kilometa 20 hizo ataniwekea changarawe, ili wananchi wangu waendelee kupita niondokane na kero. Mimi lami nitakuja kumwomba huko mbele, kwa sasa ninaomba anitengenezee barabara ya changarawe wananchi wangu wapate access ya kuingia na kutoka kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba kwa Mheshimiwa Waziri, kuna mwananchi wangu amefanya kazi na yeye, hebu amwangalie, tangu 2023; TEMESA, Zawadi Company Limited, hela ndogo sana. Akalipwe hela zake, ni mwananchi, nyumba yake inauzwa na benki!

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninashukuru kwa kunipa nafasi, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ninajua kilometa 22, zinaenda kusainiwa na tunapata lami. Ahsante sana. (Makofi)