Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Eng. Fadhili Sandali Chilombe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwenye Jimbo la Tunduru Kusini iko barabara moja inayotoka Tunduru – Nalasi – Mtwara Pachani. Nimeongea ndani ya Bunge hili kama mara tatu mara nne kuhusiana na barabara hii na Jimbo la Tunduru Kusini kwa ujumla, kwamba, Jimbo hili ni moja kati ya majimbo machache ambayo hayana lami kabisa.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, amekuwa mkweli. Alipokuja Tunduru kwenye kampeni alitoa ahadi ya kuijenga barabara ile kwa kiwango cha lami na nimeangalia kwenye randama za Mheshimiwa Waziri barabara ile ipo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tunamshukuru Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara. Barabara hii kwetu sisi ni muhimu mimi na mwenzangu Mheshimiwa Dkt. Homera. Ninajua yeye anashindwa kusema kwa sababu alivyo, lakini angeweza kuisemea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kuwa tayari Serikali imeshaamua kuchukua hatua kwenye barabara ile, zetu sisi ni shukrani. Ila ninaomba kidogo; sisi watu wa Tunduru Kusini tuna kipande hicho cha barabara peke yake chenye urefu wa kilometa 300, lakini kuna kipande cha barabara ambacho kinahudumiwa na TANROADS ambacho kinatoka Nalasi kwenda eneo moja linaitwa Chamba, ni kama kilometa 17 hivi.

Mheshimiwa Spika, pia, kuna kipande kingine kinahudumiwa na TANROADS kinaanzia pale Azimio – Lukumbule kina urefu wa kilometa 65. Ombi langu, wakati mpango wa kutengeneza hii barabara ambao unaenda kuanza muda mfupi ujao, ninatamani vipande hivi vingechukuliwa kabisa ili sisi tumalizane na TANROADS moja kwa moja.


Mheshimiwa Spika, ombi langu la pili, nimesikia hapa Wabunge ambao wana barabara za lami kwenye maeneo yao. Iko miradi imekaa muda mrefu sana. Wananchi wa Tunduru wanataka kuona lami ikipita kwenye maeneo yao. Kwa hiyo, ninaomba mradi utakapoanza basi uende kwa spidi itakayowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Tunduru maisha yetu tunategemea sana Dar es Salaam. Bidhaa nyingi au zote zinatoka Dar es Salaam na tuna alternative mbili za kufika Dar es Salaam. Aidha, tupite Mkoa wa Lindi ambako ni kilometa 708 kutoka Tunduru au tupite Songea – Iringa ambako ni kilometa 1,239.

Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida unaona kabisa njia yetu ambayo tunaitumia mara kwa mara ni hii ya Mkoa wa Lindi. Kwa sababu hiyo basi, ninaomba niungane na Wabunge walionitangulia wa Mkoa wa Lindi na Mtwara kuomba Serikali iipe kipaumbele barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, madhara tunayoyapata sisi watu wa Tunduru ni kwamba, bidhaa ikitoka Dar es Salaam kwenye barabara mbovu ile, licha ya kupanda kwa gharama zinazotokana na kupanda kwa mafuta ndani ya nchi, lakini na ubovu wa barabara pia wale watu wanatutoza. Kwa hiyo, barabara hiyo ikiendelea vile, basi mwananchi wa kawaida ambaye yuko mpakani kule anateseka zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kuwa Serikali hii ni sikivu na Wabunge wameongea kwa uchungu mkubwa na wameonesha hisia zao, matumaini yangu ni kwamba Serikali hii inaenda kuchukua hatua. Waziri Mkuu tunamwona yuko hapa na ni mtu ambaye amekuwa akifanya kazi na akitembelea kwenye maeneo hayo yote. Kwa hiyo, tunaamini haya mambo au hiki kilio cha watu wa Kusini kitafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu la tatu, Mji wa Tunduru unakua sana. Tayari Serikali ilishauona kwamba mji ule unakua na unahitaji kuendelezwa. Sisi tunayo proposal ya barabara ya bypass na upembuzi yakinifu ulishafanyika. Ile barabara inaanzia kwenye eneo moja linaitwa Mkapunda, inapita nje kwa nje inaenda kutokea kwenye eneo linaloitwa Masonya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara ile upembuzi yakinifu ulishafanyika siku nyingi, lakini nimeangalia kwenye kitabu cha mtani wangu Mheshimiwa Ulega sijaona akiongea kitu chochote kuhusiana na barabara ile.

Mheshimiwa Spika, ninamwomba, ...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: … anapokuja ku-wind up atueleze kuhusiana na hiyo bypass. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)