Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kigoma Mjini na Kigoma kwa ujumla, ninaomba tuwe na moyo wa shukrani kwa kazi iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, chini ya Waziri wetu mzee wangu Mheshimiwa Ulega.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka niwahakikishie ndugu zangu Wabunge, Jimbo la Kigoma Mjini tumeteseka sana kwa miaka mingi namna ya kuunganisha kutoka Kigoma Mjini kwenda Tabora, kutoka Kigoma Mjini kwenda Mwanza, kutoka Kigoma Mjini kwenda mikoa ambayo imetuzunguka, lakini Serikali ya Awamu ya Sita imefuta hicho kilio kwa wananchi wa Kigoma Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa ukitoka Kigoma Mjini kwenda Tabora itakugharimu saa 13, lakini sasa hivi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amemaliza hilo tatizo na kutoka Kigoma Mjini kwenda Tabora ni saa nne peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Kigoma Mjini kwenda Mwanza ilikuwa inatugharimu saa 17, lakini sasa hivi Serikali ya Awamu ya Sita imemaliza hilo tatizo na sasa hivi ni saa nane tu peke yake. Lazima tuwe na moyo wa shukrani. Siku zote tumekuwa tunaomba, lakini pale ambapo tumetendewa mambo mazuri, lazima wananchi wangu wa Kigoma Mjini Mbunge wenu ninashukuru kwa niaba yenu hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimwambie mzee wangu Mheshimiwa Ulega, maneno yote yaliyosemwa haya ninaamini yeye ni jembe na anaweza kupambana nayo. Ninauamini uwezo wake alionao na ndiyo maana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alimpa nafasi ya pili kwenye Wizara hiyo hiyo. Ingekuwa ni mtu ambaye hana uwezo wa kutosha angehamishwa hamishwa au angetolewa angewekwa mtu mwingine. Maneno yaliyozungumzwa na Wabunge wengi hapa yachukuliwe kama changamoto ili aende akawasaidie kwa sababu wao wanaongea kwa niaba ya wananchi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi hapa leo hii katika Jimbo la Kigoma Mjini hatuna shida kubwa sana na barabara za TANROADS. Kazi kubwa ameifanya, kazi kubwa ameimaliza. Nimesikia kuna Wabunge hapa wanaomba kilometa 85, kilometa 20, kilometa 30, mimi nina vitu vidogo sana, vichache mno vya kumwambia Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, tumeleta maombi ya kubadilisha barabara mbili ambazo tunataka zitoke kwenye TARURA, tumtue mzigo Mheshimiwa Profesa Shemdoe, nitammaliza. Tumtolee Mheshimiwa Profesa Shemdoe kidogo tukuletee wewe ili tuwe tunapambana vizuri. Barabara ya kutoka Katosho kupitia Kibirizi Sokoni kutokea kwenye ma-tank. Maombi yako mezani kwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya pili, ni barabara kutoka kwa Mkuu wa Wilaya pale Kigoma Mjini kwenda Katonga, tunaomba Waziri atusaidie. Barabara ambayo tumeipa jina la Kasulu Road ambayo itawapunguzia mzigo watu wa Ujiji wasizunguke kwenda mjini wakitaka kwenda kwenye nyumba zao. Tunaomba, ni kilometa chache chache sana hazifiki hata kilometa 13. Tunaomba sana tusaidie apitishe hayo maombi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la mwisho, ninaomba anipe heshima ya kupata barabara ya juu katika Jimbo la Kigoma Mjini. Nimeongea na Waziri wa Uchukuzi, kuna sehemu ambapo SGR inapita. Mama anatuletea SGR Kigoma Mjini, SGR inapita. Mkandarasi wa SGR anataka kujenga tuta, yaani aikate Kigoma Mjini katikati kwa tuta iwe kama ardhi na mbingu. Hatukubaliani na hicho kitu, tunaomba atutengenezee barabara ya juu, magari yapite juu, treni ipite chini ili wananchi wa Kigoma Mjini kwa mara ya kwanza waweze kupata flyover. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, tumeomba; Kigoma Mjini ukienda Ujiji kuna sehemu panaitwa Darajani. Tumeomba tupate Daraja kama lile la Manzese. Maandiko yako ofisini kwake. Tunataka wananchi wapite juu, magari yapite chini kwa sababu imekuwa ndiyo sehemu ambayo wanagongwa mara kwa mara katika Soko la Buzebazeba. Ameniletea engineer mmoja machachari sana, yuko vizuri sana Edward. Ninamkubali sana kwa sababu ya idea alizonazo zinaendana na spidi niliyo nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, engineer aliyekuwepo mzee wangu Choma alikuwa anafanya kazi vizuri sana, lakini huyu wa sasa hivi tutaendana kwa sababu ni kijana mwenzangu. Nikimwambia weeh na yeye anasema weeh! Tunaondoka kwa pamoja mambo yanakuwa mazuri sana. Tunaomba sana Wizara ya Ujenzi waende wakatafute hela kwa ajili ya kutimiza hii miradi ya Wabunge wengine wote walioongea. Kwangu mimi nataka kilometa 13 tu peke yake.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo machache ninaomba nishukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwa Mzee, Mheshimiwa Ulega na ninamuunga mkono wala asife moyo. Mwenyezi Mungu amsaidie tunamuunga mkono kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)